Pages

Monday, October 29, 2012

WABUNGE WAITUHUMU TAKUKURU KUWA INANUKA RUSHWA......SOMA ZAIDI HAPA

 

BAADHI ya wabunge wameishutumu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) kutokana na kujihusisha na vitendo vya rushwa jambo ambalo limesababisha kuongezeka kwa rushwa nchini.
Wakizungumza  katika semina ya wabunge wanaopambana  na rushwa iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, walisema  kuwa, Takukuru wamekuwa wakipokea rushwa kutoka kwa wananchi jambo ambalo limesababisha kukithiri kwa vitendo hivyo huku watuhumiwa wakishindwa kufikishwa kwenye mikono ya sheria.

“Takukuru inapaswa kujisafisha yenyewe kwanza kutokana na baadhi ya watendaji wake kujihusisha moja kwa moja na vitendo vya rushwa, jambo ambalo limechangia kuongeza kwa mambo hayo,”alisema Ally Kessy Mbunge wa Jimbo la Nkasi.
Aliongeza kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo masuala hayo kumesababisha kukithiri kwa matendo hayo, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa, wameshindwa kutimiza majukumu yao.

“Hakuna asiyejua kama Takukuru ni chanzo cha kuongezeka rushwa, kwa sababu wapo baadhi ya watendaji wao wanachukua, jambo ambalo limesababisha kupindisha ukweli hasa kwa kesi za rushwa au kutofikishwa mahakamani kabisa,”aliongeza.
Naye Mbunge wa Jimbo la Nkenge,  Assumpter Mshama alisema kuwa, kumekuwa na malalamiko  kutoka kwa wananchi juu ya watendaji hao kujihusisha na rushwa, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa, Takukuru ina matatizo.

“Ndani ya Takukuru hakuna usalama,kwa sababu ni sehemu ya tatizo, hii inatokana na kufunika kesi nyingi zinazohusishwa na rushwa,jambo ambalo limesababisha wananchi kutokuwa na imani nao,”alisema Mshama.
Aliongeza kutokana na hali hiyo wanapaswa kuacha kuwakumbatia wala rushwa na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa ajili ya hatua zaidi.

Hata hivyo,Mkuu wa Kitengo cha Sheria na Mashtaka wa Takukuru, Donisiana  Kessy alisema kuwa amewataka wabunge hao kusimamia kikamilifu  marekebisho ya sheria ili waweze kufanya kazi ipasavyo.

“Kuna baadhi ya vipengele vina matatizo, jambo ambalo limesababisha kesi nyingi kuchelewa kusikilizwa, au kufanyiwa kazi, kutokana na hali hiyo wabunge wana nafasi kubwa ya kuhakikisha kuwa marekebisho hayo yanafanikiwa,”alisema Kessy. Aliongeza kuwa uchunguzi wa kesi kama hizo ni ngumu, kwa sababu anayefanya kosa anajua anachokifanya, jambo ambalo linawafanya wajifiche ili wasiweze kubainika, kutokana na hali hiyo wanapaswa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha watuhumiwa wanapatikana na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII