SOMA MAHOJIANO ALIYOFANYA ESTHER WASIRA NA GAZETI LA TANZANIA DAIMA HAPA....VERY INTERESTING

Yafuatayo ni mahojiano maalum kati ya Esther Wasira na Tanzania Daima Jumapili tarehe 18/11/2012 Na Happy Katabazi

Swali: Naomba kufahamu historia ya maisha yako?

Jibu: Nilizaliwa 1987 hapa hapa Dar es Salaam; nikasoma shule ya Msingi Muhimbili (1992-1998). Elimu ya Sekondari (O-level) pale Loyola High School (1999-2003) na (A-level) pale Shaaban Robert Secondary School (2004-2006). Kisha nikaingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule ya Sheria (Zamani Kitivo cha Sheria) (2006-2010)

Swali:Kwanini umeamua kujiingiza kwenye ulingo wa siasa wakati wewe ni mwanasheria?

Jibu: Siasa ni kitu kisichoepukika. Kila kinachonizunguka ni siasa. Haki na wajibu wa kila mtu kwenye jamii unategemea na siasa ya nchi yake. Sasa kuliko kukaa pembeni, kunyamaza kimya na kuangalia jinsi siasa zinavyoendeshwa na kuathiri maisha yangu na ya watanzania wenzangu nimeona ni bora zaidi kuongea panapo fursa ili kuwaamsha na wenzangu kutoka kwenye usingizi mzito wa kutokufikiri. Nadhani kama nilivyosema kwenye hotuba yangu siku ya Kongamano la kumuenzi mwalimu Nyerere, Elimu tunayoipata haitakiwi itengeneze “Robots” bali watu watakaoiuliza maswali serikali yao ili iwajibike.Kuwa mwanasheria, kwangu nakuona kama ni Nyongeza “added advantage” kwasababu kunanifanya niwe muangalifu zaidi katika kunena, kutenda na kutetea maslahi ya watu kwa ujumla bila kuvunja sheria za nchi au kukiuka maadili yaliyowekwa kwasababu najua uhuru wangu unapoanzia na mipaka yake,na haki na wajibu wangu.

Swali:Kwanini usingejiimarisha kwanza kwenye fani yako ya sheria ndipo kwanza ukajiingiza kwenye siasa?

Jibu: Siasa kwa mtazamo wangu sio mtaji wala sio hobby!! Kwangu ni jambo la msingi sana ambalo litaamua hatma ya maisha ya watu kwenye ardhi yao. Katika vitu ambavyo sio vya kuhairisha ni utetezi wa maisha ya mwanadamu na maslahi yake kwa ujumla. Na kwa hali ya nchi ya Tanzania ilipofikia, kwangu ni kama “State of Emergency”. Kila mwenye “silaha” aingie vitani. Umahiri wa sheria hautanifaa kitu kama sitashiriki mapema harakati za kuleta mabadiliko kwenye nchi yangu na kumkomboa mtanzania wa hali ya chini ambaye dira ya maisha yake imefutika na kesho yake ni kama ndoto. Sihitaji Shahada ya pili ya Sheria kujua kuwa viongozi wengi wa kizazi cha sasa wamepotoka na wanahatarisha maisha yetu na nchi yetu kwa ujumla. Wakati uliokubalika ni sasa.

Swali:Kwanini umeamua kujinga na chama cha Chadema?

Jibu: Jibu liko wazi. Mpaka sasa Chadema ndiyo chama pekee kinachoonesha dhamira safi ya kuiongoza Tanzania na kuleta matumaini ya kujenga Tanzania mpya yenye Neema. Itikadi zake na falsafa zake na nia ya dhati ya kiutendaji kwa viongozi mbalimbali wa chama hiki ni sehemu ya mambo yaliyopelekea mimi kukichagua Chadema. Lakini nilishawahi kusema na nitarudia haya, Chadema ni chama cha watu makini sana, kuanzia vijana mpaka akina mama; ni fahari kubwa sana kujiunga na Chadema na tena ni Ushahidi wa mtu kujitambua na kuondokana na ushabiki wa kihistoria usio na tija wala manufaa kwenye nchi yetu wa kung’ang’ana na dhamira ya “chama kikongwe”. Ogopa sana mtu anayeshindana na mabadiliko mahali ambapo hayana budi kuja.

Swali:Utawezaje kufanya kazi ya uanasheria wakati huo huo ni mwanasiasa?

Jibu: Sheria hainizuii kufanya shughuli za kisiasa, lakini pia ratiba yangu itabadilika kufuatana na majukumu husika. Changamoto hazina budi kuja lakini ndiyo mwanzo wa kukua na kupanuka fikra na kiutendaji zaidi.

Swali:una mahusiano gani na mzee wasira?

jibu: Mzee Wasira yupi? Wapo Wazee Wasira Wengi (hahaha). Ila utashi unaniongoza kuwa ni Mzee Stephen Wasira (MP) (Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Mawasiliano na Uratibu); huyo ni baba yangu mdogo aliyenyang’anyana ziwa na baba yangu mzazi, Wakili George Wasira, ambaye pia ni mmoja kati ya waasisi wa Chadema

.
Swali:Una ujumbe gani kwa watoto wa kike hapa nchini?

jibu: Watoto wa kike nina mengi ya kuwaeleza, ila kwa leo nitasema hivi: Katika dunia ambayo nguvu ya misuli haitumiki sana na badala yake nguvu ya akili ndiyo inatakiwa zaidi, basi nafasi ya mwanamke kwenye jamii ni kubwa sana. Angalia jinsi Michelle Obama wa Marekani kuanzia mwanzo wa safari ya Barack Obama ya kisiasa anavyochukua nafasi kubwa kumsaidia mumewe kwenye campaigns mpaka Obama anakiri kuwa mke wake amekuwa msaada mkubwa sana. Wanawake tuna nafasi kubwa sana ya kuleta mabadiliko ya kweli kwenye nchi yetu kama tukiacha uoga na tabia ya kupenda kusubiria chini ya ngazi ili tupewe vitu kwenye visahani vya dhahabu. Mwenye fursa ya kusema amuongelee aliyekosa jukwaa la kujielezea; tusijipende wenyewe kwasababu tumefanikiwa kuwa na “Vitz” na kuvaa dhahabu. Inasikitisha mwanamke anapokosa huruma na kuamua kujiingiza kwenye tafrani za rushwa!! Pia wale wamama wanaopewa kanga na Madera na shilingi elfu kumi kumi ili kuingiza madarakani utawala mbovu, jaribuni kufikiria mbali na muone ni mazingira gani mnawaachia watoto wa watoto wenu. Aibu gani hii?? We are the mothers of this nation!! Hiyo siyo tabia ya mama! Wote tunaweza kulikomboa Taifa letu kama tukiamua kwa dhati kusimama pamoja.

Swali:Tueleze mtazamo wako kuhusu mwenendo wa siasa hapa nchini?

jibu: Kwa ujumla, siasa ya sasa inaendeshwa kwa mabavu, ubabe, hisia, hofu, hujuma, rushwa, mapambano, udini, ukabila, mipasuko na huku sauti ya mabadiliko ikisikika kwa mbali. Aliyeshika mpini anatumia kila mbinu anayoweza ili kuendelea kulima, na aliyedhani ameshika makali yangemsaidia anajikuta kafungwa mikono. Ndio maana siasa wanaiita mchezo mchafu. Huwezi kumuondoa jabali kwenye milki yake bila kupambana nae, jabali ana dola, jabali ana fedha, jabali ana sauti, lakini mwisho wa siku, jiwe moja tu litamuangusha Shujaa, maana lina “Sauti ya Watu” nyuma yake.

Swali:Ni kitu gani ambacho kiliwahi kukufurahisha au kukusikitisha katika maisha yako?

Jibu: Kutekwa na kujeruhiwa vibaya kwa Dr. Steven Ulimboka na kisha kutelekezwa katika msitu wa Mwabwepande; pamoja na utata uliojitokeza kuhusu suala hilo, na namna uchunguzi ulivyoendeshwa na hatua zilivyoshindwa kuchukuliwa dhidi ya wale “wote” waliodaiwa kuhusika. Inaleta mashaka sana juu ya hali ya Usalama wa nchi yetu na usalama wa watetea haki na usawa.


Swali:Nini matarajio yako ya baadaye katika medani ya siasa na sheria?

Jibu: Matarajio yangu kisheria ni kujiendeleza zaidi kwasababu ndio career yangu na kutafuta maarifa zaidi kulingana na malengo yangu niliyojiwekea.
Lakini pia, kisiasa, kikubwa ni kutumia fursa mbali mbali ili kutimiza azma ya kuiona Tanzania mpya inakuja na mabadiliko yanakuwa halisi na sio dhana tena. Kwa sasa, ni kushawishi watanzania kwamba Chadema imekomaa na iko tayari kushika dola na kufanya sauti ya mtanzania wa kawaida isikike tena. Hapo baadae, nitaendelea na kazi ya ujenzi wa chama na kufanya yale majukumu ambayo viongozi watanipangia kufanya; ikiwemo kushauri, kujitolea, kuelimisha, na kuhamasisha watanzania kuhusu mambo mbalimbali yahusuyo chama na taifa kwa ujumla.

(Nyongeza)- Mwandishi mmoja wa gazeti la Raia Mwema alitoa makala yake ambayo pamoja na mambo mengine alisema kuwa kwa hotuba yangu niliyoitoa siku ya Kongamano la kumuenzi Mwalimu Nyerere, nimedharau na nimeonesha dhahiri kutoheshimu mchango wa Wazee katika jamii; kitu ambacho hakikuwa sahihi. Nataka nitoe ufafanuzi kuwa, Vijana ni chachu ya mabadiliko na ndio maana mifano yote aliyoitoa yeye alionesha kuwa kila “Revolutionary Attempts” yaani hatua za kimapinduzi zilifanywa na vijana na baadae wazee ndio waliongoza nchi, yaani watu wa makamo.
Kilio chetu ni kwamba,vijana ni lazima waamke kwani wao ni nguvu kazi ya taifa lolote; wao wakilala basi na harakati zote zitalala. Wazee wanaweza kubaki kuwa ngazi shauri lakini watendaji siku zote ni vijana.
Lakini pia, kwenye ajira, vijana wapewe nafasi za kazi pale ambapo wanastahili na hii itafanikiwa pale watakaporekebisha sera za uajiri zenye kutaka uzoefu wa miaka 6 au 10 maana hiyo inawapa tabu vijana wengi waliosoma kupata kazi.


By Esther Wasira Mobile: 0784 999911
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs