Pages

Wednesday, November 14, 2012

VIONGOZI WA CHADEMA MWANZA WAHUKUMIWA.....SOMA ZAIDI HAPA


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, imemhukumu kwenda jela miezi mitano Katibu wa Chadema Wilaya ya Ilemela, John Anajus huku ikiwatoza faini ya Sh620,000 viongozi wengine akiwamo Mkurugenzi wa Oganaizesheni wa Chadema Taifa, Benson Kigaila na madiwani wawili.
Hukumu hiyo ilitolewa kufuatia watuhumiwa hao kudharau amri ya mahakama iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi mkoani Mwanza, Angelo Rumisha kufuatia kesi namba 69/2012. Kesi hiyo ilifunguliwa na Henry Matata aliyekuwa Diwani wa Chadema Kata ya Kitangiri, baada ya kuvuliwa uanachana kwa kukiuka katiba ya chama, ambaye aliweka pinganizi la kuteua mgombea umeya Wilaya ya Ilemela.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Rumisha alisema mahakama haiwezi kudharauliwa pale inapotoa maagizo yake, hivyo imewatia hatiani kwa kukaidi agizo lake ili iwe fundishi kwao na wengine. Hakimu Rumisha aliwatoza faini ya Sh155,000 kila mmoja watuhumiwa, huku John Anajus ambaye hakuwapo mahakamani akihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela atakapopatikana.

Watuhumiwa ambao walilipa faini ni Kigaila, Katibu wa Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Ilemela, Kalod Majura, Diwani wa Kata ya Kirumba, Dan Kahungu na aliyekuwa Meya wa Mwanza ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya chama hicho, Josephat Manyerere.
Katika kesi hiyo, Matata anayetetewa na Wakili Salum Magongo, aliweka pingamizi mahakamani baada ya Kamati Tendaji ya Chadema kutangaza kumvua uanachama kinyume cha taratibu na kudai kwamba, viongozi hao kwa pamoja walishiriki kuvunja sheria kwa kumtangaza kumfukuza udiwani.
Hivyo, kudaiwa kupuuza amri halali ya mahakama iliyotolewa Septemba 15, mwaka huu.
Hata hivyo, Diwani huyo alivuliwa uanachama na Kamati Kuu ya Chadema Septemba 9, mwaka huu kutokana na madai ya kuvunja katiba ya chama hicho, mpaka kuchaguliwa kuwa Meya wa Manispaa ya Ilemela alikuwa amefungua kesi mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza akiomba mahakama imrejeshee uanachama wake.
Hata hivyo, katika hatua ya kuwanusuru madiwani hao kufungwa, wananchama wa chama hicho ambao walikuwa wamefurika mahakamani hapo walichanga Sh250,000 na Sh370,000 zingine zililipwa na Mbunge wa Ilemela,Samson Kiwia.

SOURCE: MCL

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII