Pages

Wednesday, December 26, 2012

HUYU NDIYE NUSRA, DEREVA MWANAMKE WA MABASI YA SHABIBY....SOMA ZAIDI STORY YAKE HAPA

*Ana ndoto za kufungua Chuo cha mafunzo ya udereva kwa wanawake ili waweze kuendesha magari makubwa.


*Basi lake hugombaniwa na abiria popote anapopakia, hujaza kwanza na kuondoka kisha mabasi mengine

Nusra akiwa kazini

NUSRA Maguluko (28) ni msichana jasiri na anayependa kujaribu na kupata mafanikio ya majaribio yake bila woga wala kujali ni aina gani ya kazi anayotakiwa kufanya yeye kama mwanamke na ipi asiyostahili kufanya yeye kama mwanamke.

Ni ujasiri wake hasa ndiyo ulimuwezesha kumfikisha hatua aliyonayo kwa sasa, ambaye ni miongoni mwa wanawake wachache na hasa kwa Tanzania waliopata kuifikia na kujiamini hadi kuwa na ujasiri wa kubeba roho za watu zisizopungua 40 kila safari moja ya kwenda Dodoma ama kotoka Dodoma kuja Dar.

Nusra ni mzaliwa wa Mkoa wa Manyara katika wilaya ya Kiketo, na ni mtoto wa nne kuzaliwa kati ya 12 wa familia ya baba yake mzazi mzee, Maguluko na Elimu yake ni Kidato cha pili tu.

Alimaliza elimu ya Msingi mwaka 1997, katika Shule ya Msingi Matui iliyoko Wilayani Kiteto, baada ya kuhitimu elimu ya msingi alijiunga na elimu ya Sekondari ambayo kwa bahati mbaya hakuweza kumaliza na kuishia Kidato cha pili baada ya kusumbuliwa na maumivu ya kichwa mara kwa mara.

 

Nusra, alishauriwa na madaktari kupumzika kwa muda wa miaka mitatu bila kusoma ama kuwa akiangalia karatasi nyeupe mara kwa mara, jambo ambalo lilimfanya kuamua kumsumbua Baba yake mkubwa, Hamis Mang'endi aliyekuwa ni fundi wa magari ili amfundishe ufundi na udereva wa gari.

Baada ya kumsumbua sana baba yake mkubwa, kwa kuwa akiripoti katika gereji yake kila asubuhi na kushinda hapo huku akimfuatilia kila analofanya katika magari, Mzee Hamis, baada ya kuona kuwa Nusra alikuwa na moyo wa kweli wa kujifunza ufundi, aliamua kuanza kumfundisha ufundi hatua kwa hatua
 .

Baada ya kumudu kidogo kushika Spana, Mzee Hamis, mwaka 1998, alianza kumfundisha udereva, tena kwa kumfundishia katika gari aina ya CombVolkswagen, ambapo baada ya miezi sita tu Nusra tayari alishamudu kuendesha gari na kutulia barabani.

Nusra alipomudu kufanya vurugu za barabarani, alikabidhiwa na baba yake mzazi, Canter ya Tani 3 na robo ili aweze kufanyia kazi ya kubebea mizigo, huku akikodishwa ambapo alifanya kazi hiyo kwa muda wa miaka miwili.

Hatimaye mwaka 2001, Nusra, aliamua kuachana na kazi ya kuendesha Canter ya kubeba mizigo na kuamua kuanza kazi ya kulima kwa Treka, ambapo alikuwa akikodishwa na wakulima na alimudua kulima hadi Heka 10 kwa siku kwa ujira wa Sh. 10, 000 kwa kila heka moja.

Mwaka 2003, Nusra alianza kuendesha Min Bus, huku akiwa na Leseni ya Class C baada ya wakati huo kudanganya umri ili aweze kupata uhalali ya kufanya kazi anayoipenda ya udereva.

Basi analoendesha Nusra
 
Alifanya kazi hiyo ya kutoa huduma usafiri kwa abiria kutoka Wilaya ya Kiteto kwenda Vijijini hadi mwaka 2006, alipokabidhiwa Basi aina ya Fuso lenye uwezo wa kubeba abiria 40, nakutoa huduma hiyo ya usafirishaji wa abiria kutoka Wilaya ya Kiteto hadi Dodoma, kazi aliyoifanya hadi mwaka 2011.
Baada ya kuchoshwa na njia za Vijijini na kile alichodai kuaua kutafuta maslahi zaidi, Nusra, aliamua kuvaa, Mbunge wa Gairo, he Shabiby, na kumuomba kazi jambo ambalo lilimshangaza na kumuhoji kama anaweza kweli kuendesha gari kubwa tena la abiria.

''Baada ya kuniuliza swali hilo, mimi nilimjibu Mheshimiwa samahani wewe nisaidie unipe kazi, halafu ndiyo utaniona nikiwa kazini kama naweza ama siwezi, kwani najiamini na ndiyo maana nimekuja kwako''. alisimulia Nusra

 
Baada ya maongezi marefu ya maswali na majibu juu ya ujasiri wa Binti huyo, aliyeonekana mdogo akiwa na maelezo ya mambo makubwa, Mhe. Shabiby, aliamua kumwajiri, Nusra ambapo hadi sasa anapiga mzigo katika kampuni hiyo ya Shabiby, akiburuza Basi linalofanya safari zake Dar-Dom.

Hivi Sasa Binti huyo, anandoto za kufungua Chuo cha Mafunzo ya Udereva kwa wanawake, akiwa na lengo la kuwafikisha mbali wanawake wenzake ili waweze kuwa na ujasiri wa kuendesha magari makubwa na si gari ndogo pekee.

Kwa hatua hiyo sasa Nusra, ameanza kusaka wafadhili, ili aweze kutimiza ndoto zake hizo, ambapo amewamba wadau mbalimbali pamoja na Serikali kujitokeza kumsapoti, ili kufanikisha kufungua chuo hicho chenye lengo la kuwainua Kinamama.

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII