Pages

Friday, December 7, 2012

PRECISION AIR YAZINDUA NDEGE YAKE MPYA AINA YA ATR 42-600



 Waziri wa Uchukuzi (wa tatu pichani) kutoka kulia,Mh.Dkt Harisson Mwakyembe akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wakuu wa Shirika la Ndege la Precision,wakati wa uzinduzi wa  ndege yao mpya aina ya ATR 42-600.
 Waziri wa Uchukuzi (wa tatu pichani) kutoka kulia,Mh.Dkt Harisson Mwakyembe akikata keki kuashiria uzinduzi wa  ndege yao mpya aina ya ATR 42-600la fu,kwenye hafla fupi iliyofanyika jijini dar,kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika hilo, Michael Shirima na shoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Alfonse Kioko kwa pamoja wakishuhudia tukio hilo adhimu. 
Baadhi ya wadau mbalimbali walioshiriki uzinduzi wa ndege hiyo mpya aina ya ATR 42-600 wakiipanda.
 =======  ========  ========
Shirika la Ndege la Precision limezindua ndege yake mpya aina ya  ATR 42-600, ikiwa ni hatua ya mwendelezo wa maboresho ya miundombinu ya shirika hilo kwa maslahi ya wateja wake. Hata hivyo uzinduzi huu ni sehemu tu ya mkakati wa miaka mitatu, ambapo katika kipindi hicho, shirika limepanga kuongeza aina kama hii ya ndege za (ATR) hadi kufikia idadi ya ndege 5, mradi utakaogharimu kiasi cha Dola milioni 95.
Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika hilo, Michael Shirima, alipongeza hatua ya uzinduzi huo, ambapo alisema itasaidia kwa kiasi kikubwa kuleta mapinduzi katika sekta ya usafirishaji wa anga. “Ndege hii  mpya na ya kisasa ya ATR 42 - 600 ina zaidi ya viwango vinavyohitajika katika huduma ya usafiri wa anga, ina muundo wa kipekee uliotengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu,  na inaweza kufanya huduma zake hata kwenye maeneo ya miundombinu duni,” alisema Shirima.
Katika mwendelezo wa uboreshaji wa huduma zake, Precision imeendelea kupeleka ndege zake ndogo mikoani na kuahidi kuendeleza azma yake ya kuwa kitovu cha utoaji wa huduma bora za anga nchini.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Alfonse Kioko, alisema upanuzi wa wigo wa huduma za anga katika shirika hilo, ni miongoni mwa mikakati ya kuhakikisha wateja wake wanafurahia ufanisi na huduma za usafiri huo,  sanjari na kupunguza adha na usumbufu kwa wateja .  “Ni fahari kubwa kwa Tanzania kupitia shirika la ndege la Precision kuwa taifa la kwanza katika bara la Afrika kuingiza ndege hii ya kisasa na iliyotengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu,”alisema Kioko.
“ATR 42-600 inakidhi matakwa na mazingira ya ukuaji wa miundombinu katika maeneo mengi barani Africa jambo ambalo linatupa hamasa ya kuongeza masafa na uboreshaji wa huduma zetu katika hali ya ufanisi zaidi.” Precision Air ina wigo mpana na imejiimarisha zaidi katika kuhakikisha inafikisha huduma zake katika mikoa yote. Shirika hilo ni la kwanza kati ya mengi yaliyopo nchini, kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam, DSE.
Aina hiyo ya ndege itasaidia kupanua wigo wa usafiri wa anga unaofanywa ndani ya shirika hilo kwa safari za ndani na nje ya Tanzania. Hata hivyo shirika liko mbioni kuanzisha safari zake katika mikoa inayokua kwa kasi kama Mtwara.

 “Maeneo mengine tunayoyatazama ni mkoa wa Mbeya punde tu uwanja wake mpya utakapozinduliwa mwakani, Bukoba na Kigoma ambapo viwanja vyake bado vipo kwenye matengenezo.”

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII