Pages

Friday, December 14, 2012

TCU yakibana Chuo Kikuu cha Kampala


TUME ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU) imeiagiza menejimenti ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU) Dar es Salaam kuwasilisha sifa za wahadhiri wanaofundisha chuoni hapo kwa ajili ya kuwafanyia ukaguzi.
Agizo hilo la TCU limekuja baada ya wanafunzi kuhoji sifa za baadhi ya wahadhiri wanaowafundisha, wakati walipokuwa kwenye mgomo wa kutoingia madarasani wakitaka kusikilizwa kwa matatizo mbalimbali likiwamo la sifa za wahadhiri.

Katika taarifa iliyotolewa kwa umma na Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Sifuni Mchome, orodha hiyo ya wahadhiri inatakiwa iandaliwe kwa kushirikisha viongozi wa wanafunzi na Kitengo cha Udhibiti wa Ubora cha Chuo (KIU Quality Assurance Unit).

Profesa Mchome ametaka orodha hiyo iambatane na nakala za vyeti vya wahadhiri wote wanaofundisha katika chuo kikuu hicho na kuwasilishwa TCU kabla ya Desemba 31 mwaka huu.

Hoja hiyo ya wanafunzi kuhoji ubora wa walimu wao ni moja ya matatizo mengine 22 waliyoyalalamikia na kusababisha kufunga barabara ya Pugu mwanzoni mwa wiki hii, wakishinikiza matatizo hayo kupatiwa mwafaka.

Katika matatizo hayo yaliyowafanya wagome kuingia madarasani, wanafunzi pia walitoa malalamiko kuhusu utoshelevu finyu wa mafunzo wanayopata katika masomo ya shahada za udaktari wa binadamu na uhandisi.

Katika tatizo hilo, TCU imeahidi kuunda timu ya wataalamu itakayoshirikisha wataalamu wa kutoka Chama cha Madaktari Tanzania (Mat) na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) ili kufanya uchunguzi wa kina kuhusu malalamiko yaliyojitokeza na kutoa mapendekezo yake.

“Zoezi hili linatakiwa likamilike ifikapo Januari 15 mwakani na hatua stahiki zianze kuchukuliwa baada ya hapo’’ alisema Prof. Mchome katika taarifa aliyoitoa juzi.
“Sambamba na hili, Tume inaandaa utaratibu wa kufanya tathmini ya masuala mbalimbali katika chuo hiki ili kujiridhisha kama masuala mbalimbali yanatekelezwa kwa mujibu wa sheria,” aliongeza Profesa Mchome.

Kuhusu wanafunzi kulazimishwa kwenda kufanyia mahafali nchini Uganda na kugharamikia kiasi cha Sh300,000 kwa ajili ya kushiriki mahafali hayo, Profesa Mchome alisema chuo hicho kimeelekezwa kuanza kufanya mahafali yake hapa nchi kuanzia mwakani.

Aidha alisema kuwa mwanafunzi ana haki ya kupatiwa Cheti, Stashahada au Shahada endapo amehitimu na kufaulu masomo yake na halazimiki kushiriki katika mahafali.

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII