Dr. Slaa alipua bomu, Mnyika awatolea uvivu Nape na Mwigulu....SOMA ZAIDI HAPA
KATIBU Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa,
amesema kuwa amebaini kuwapo mpango wa serikali na Chama Cha Mapinduzi
(CCM), kuingiza mtambo wa kuingilia mawasiliano ya wapinzani kwa ajili
ya kuhujumu uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Dk. Slaa ambaye ni mara yake ya pili kutoa tuhuma za CCM kuingiza mtambo
wa kuingilia mawasiliano ya CHADEMA, alisema tayari ameshapata e-mail
yenye kuonyesha thamani ya mtambo huo na kwamba utagharimu dola 850,000
za Marekani, karibu sawa na sh bil. 1.3.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua kongamano la vijana wa
vyuo vikuu wa CHADEMA (Chaso), jijini Dar es Salaam, lililokuwa na lengo
la kujitathmini na kupanga mikakati ya kuelekea uchaguzi mkuu mwaka
2015 pamoja na kuwaapisha viongozi wapya wa shirikisho hilo.
Alisema tayari ameshaandika barua kwa mamlaka husika kuwajulisha hilo, lakini hadi sasa hawajajibu.
“Tuna ‘details’ na nyaraka nyingi zinazoonesha namna mtambo
utakavyotumika kwa ajili ya kuwahujumu wapinzani na kwa kuwa
tumeshaandika barua kwa mamlaka husika na hawajatujibu, kwa sasa
sitaenda kwa undani zaidi juu ya hili. Subirini siku ifike nitaweka kila
kitu hadharani,” alisema Dk. Slaa.
Alisema CCM kwa kushirikiana na Idara ya Usalama wa Taifa, wamekuwa
wakitengeneza propaganda mbalimbali za kutaka kumchafua yeye pamoja na
CHADEMA, lengo likiwa kuwaondoa Watanzania katika ajenda za msingi za
kupigania ukombozi.
Aliongeza kuwa, awali mahasimu wake kisiasa walikuja na propaganda kuwa
amechukua mke wa mtu, kisha wakasema amedhulumu viwanja huko Mabwepande
na sasa wameanzisha suala la kukopa sh milioni 140 ambalo alifafanua
kwamba halina ukweli wowote.
“Wanawalisha maneno wale wanaokubali kununulika, msifikiri yale yanatoka
midomoni mwao hapana, lakini watambue leo hakuna Mtanzania
atakayehangaika na uongo unaotengenezwa kwa ajili ya kuwafanya wazidi
kutawaliwa,” alisema Dk. Slaa.
Akizungumzia tuhuma za CCM na serikali kushirikiana kuingiza mtambo wa
kuhujumu mawasiliano ya wapinzani, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nauye alisema madai hayo ni ya uongo.
Akizungumzia vita dhidi ya ufisadi nchini Dk Slaa, alisema
wanaojidanganya kwa kusema kwamba kwa sasa siyo agenda ya Watanzania,
wamefilisika kimawazo kwa kuwa suala hilo halitanyamaziwa na CHADEMA
mpaka wahusika watakapotiwa mbaroni.
“Kama wanataka tunyamaze kuhusu ufisadi basi waturudishie twiga
waliowatorosha, fedha za EPA, mabilioni ya Uswisi na pia watuambie ni
kina nani wanawaua tembo walio katika hifadhi zetu na kisha kusafirisha
pembe kupitia bandari zinazolindwa na watu wanaolipwa kwa kodi za
Watanzania… vinginevyo hakuna wa kutunyamazisha zaidi ya Mwenyezi
Mungu,” alisema Dk. Slaa.
Akielezea sera ya majimbo na mafanikio ya mikutano ya chama hicho kwa
mwaka 2012, Dk. Slaa, alisema imekuwa na mafanikio makubwa hasa baada ya
wananchi kuzinduka na kuamua kudai haki za kutaka kunufaishwa na
rasilimali zinazowazunguka.
Alisema miaka minane iliyopita wakati CHADEMA waliposema rasilimali za
nchi zianze kunufaisha eneo husika kwanza, watu wengi hawakuelewa,
lakini leo baada ya kufikiwa na ufahamu kupitia Operersheni za CHADEMA,
maarufu kwa jina la M4C, kila eneo limezinduka na sasa serikali inaanza
kuwaona watu hao kuwa maadui kwa kuwa wanadai kuthaminiwa.
“Nchi yetu kila eneo kuna rasilimali na hatusemi ziwanufaishe watu wa
eneo husika tu, bali tunataka waanze wao na ziada ndiyo iende maeneo
mengine, leo mnawaona Mtwara na Lindi wanapigania haki hiyo na maeneo
mengine hivyo hivyo, kwa hiyo tuna haki ya kujivunia mafanikio ya
kuwaelewesha wananchi juu ya kudai haki zao,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa, mwaka huu watahakikisha suala la mauaji holela ya raia
wasio na hatia, halijirudii ikiwa ni pamoja na kuishinikiza serikali
iunde tume huru ya kimahakama kufuatilia matukio yote ya mauaji yenye
utata yanayohusishwa na harakati za kisiasa mwaka 2012.
Akizungumzia suala la kufukuzana ndani ya CHADEMA, Dk Slaa alisema
hawataogopa kumfukuza mwanachama yeyote msaliti anayeenda kinyume na
katiba ya chama hicho na kutolea mfano madiwani waliofukuzwa mkoani
Arusha na wanachama wengine.
Alisema licha ya madiwani wa Arusha kujua walifukuzwa kwa mujibu wa
Katiba ya CHADEMA, waliamua kwenda mahakamani kutaka kukisumbua chama,
hali aliyosema mahakama haikuweza kukubaliana nao na sasa wanawajibika
kulipa gharama za kesi na wakishindwa wataenda gerezani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika,
aliitaka CCM imshauri Rais Jakaya Kikwete aunde tume huru kuchunguza
mauaji mbalimbali ya kisiasa yanayotokea nchini badala ya kupanda
jukwaani na kusema CHADEMA ndio wauaji.
Alisema kuwa kila siku Nape Nnauye, Mwigulu Nchemba na viongozi wengine
ndani ya chama chao wamekuwa wakitaka kuwaaminisha wananchi kuwa CHADEMA
inahusika na mauaji ya kisiasa.
“Nape anasema CHADEMA wanahusika na mauaji ya kisiasa, Mwigulu naye
hivyo hivyo, viongozi wengine ndani ya chama chao nao wanapiga kelele
hizo hizo, sisi CHADEMA tunasema iundwe tume huru ya kimahakama wao
wanaogopa, wanajua wataumbuka juu ya ufedhuli wao,” alisema Mnyika.
Aidha, alisema wamebaini CCM inachapisha kadi za CHADEMA na kisha
kuwagawia wanachama wao ili kuwahadaa wananchi kuwa chama hichi
kinakimbiwa.
“Unajua ukiona mtu anajidanganya mwenyewe, huyo inabidi umsikitikie kwa
kuwa kila njia ya udanganyifu wao sasa imeshabainika katika mioyo ya
Watanzania, na sasa wameona wajaribu kujiridhisha katika nafsi zao
wakiwa katika mikutano ya hadhara kwa kupeana kadi walizochapisha
wenyewe huku wakishangiliana,” alisema Mnyika.
Source:
Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII