Mnajimu Maalim Hassan Yahya Hussein.
JANA
Mnajimu Maalim Hassan Yahya Hussein alitoa utabiri wake ambao magazeti
mengi leo yameundika. Tunawaletea utabiri huo kama alivyousoma mbele ya
wana habari ofisini kwake jana.
PRESS RELEASE UTABIRI 2013
Ndugu wanahabari wa vyombo vyote vya habari hapa nchini
Assalaam Aleykum,
UTANGULIZI:
Tarehe kama ya leo, mwaka 2012 ambayo ilikuwa
siku ya Ijumaa nilikuiteni hapa kuzungumzia Utabiri wa mwaka 2012 ambao
kinyota bado unaendelea. Utabiri huo utakoma Machi 20, Mwaka huu 2013
kwa maana tarehe 21 Marchi ndio mwaka mpya wa kinyota na ambapo ndipo
Utabiri rasmi wa mwaka 2013 utakapoanza.
Wengi wenu mmeona na Ni imani yangu na yetu
kwamba asilimia 95 ya Utabiri tulioutabiri Januari 13 mwaka 2012
umefanikiwa na yaliyotabiriwa yametokea kama tulivyouweka hadharani.
(Nakala ya Utabiri huo nimeambatanisha)
Bila kujisifu, hali hii inaoonesha wazi kuwa
Muasisi wa kazi hizi katika Afrika ya Mashariki na Kati na Dunia nzima
kwa ujumla, Sheikh Yahya Hussein ambaye kwa sasa ni Marehemu,
alirithisha kazi zake hizi kwa mtu Jadidi, Mweledi na Makini kama
alivyokuwa akimuomba Mwenyezi Mungu siku zote katika uhai wake.
Kabla sijatangaza rasmi Utabiri wa Mwaka huu, kwanza kabisa nitazungumzia namna mwaka 2013 ulivyoingia.
Mwaka wa 2013 umeanzia siku yaJumanne, siku hii inatawaliwa
Na Sayari ya Mars au Mariikh ambayo nyota zake ni mbili nazo ni nyota ya Punda au Aries na Nge ambayo ni Scorpio
Kinyota hii nyota ya Punda ni nyota ya mwanzo ambayo ndio kichwa na kama nyumba ya Mwanzo na maana yake ni Mwanzo wa jambo, Anza jambo,Tangaza jambo au kupata mafanikio.
Nyota ya Pili ni NGE au Scorpio ambayo Kinyota
ni nyota ya Nane au Nyumba ya Nane, nyota hi iinaashiria, Hasira,
kupotea, Kuachana, kukimbiwa, Maziko,Vifo na Wasiwasi.
Kwa kawaida Mwaka ukianzia siku ya Jumanne
unaashiria Matatizo makubwa, ikiwa ni pamoja na kuongezeka Vita sehemu
mbali mbali za dunia, Viongozi wa kidini, kisiasa, na kijamii kuugua
sana na wengine kufa, kutokea moto katika miji mikubwa, ukame, ukosefu
wa Maadili, wafanyakazi kuwapiga mabosi wao, uongo kuwa mwingi kwa maana
propaganda, umbeya, masengenyo, mashujaa kufariki, mazao kupungua,
ajali kuwa nyingi za bara na baharini na angani, watu kuwa na khofu na
watu wengi kuuwawa.
Kwa upande mwingine inaashiria biashara kuongezeka na neema kuwa kubwa na watu kufaidika katika biashara.
Pamoja na hayo kutakuwa na Matatizo ya maradhi
kwa watoto hasa kuugua vifua na maradhi ya kichwa, wanawake wajawazito
kupoteza maisha kwa wingi au kuzaa kwa matatizo makubwa.
Kwa upande wa Siasa Mwaka ukianzia siku ya
Jumanne basi hutokea kwamba Viongozi wa Kidini na kisiasa kutoa matamshi
ya utatanishi na kusababisha khofu kubwa na hata watu kupigana lakini
hali hiyo hudumu kwa muda mfupi, baadhi ya viongozi hukaa pamoja na
kukubaliana mambo baina yao na kurejesha hali ya utulivu na amani.
Mwaka huu wa 2013 Mwezi utapatwa mara tatu
tarehe 25/4/2013 ambayo itakuwa siku ya Alkhamisi, tarehe 25/5/2013
ambayo itakuwa siku ya Jumapili na tarehe 18/10/2013 siku ya Ijumaa.
Jua lenyewe nalo lipatwa mara mbili tarehe
10/5/2013 ambayo itakuwa siku ya siku ya IJumaa na tarehe 3/11/2013
itakuwa siku ya jumapili.
Siku hizi za Alhamisi, Ijumaa na Jumapili ambazo
Jua na Mwezi utapatwa zina athari ya moja kwa moja kwa maisha yetu,
Alkhamisi inatawaliwa na Sayari ya Jupite r ambayo inahusika na
Serikali, Wizara. Safari, na Magomvi.
Siku ya Ijumaa inatawaliwa na Sayari ya Venus au
Zuhura ambayo inahusika na Muafaka, Urafiki,, Mapenzi, Ndoa,
Masikilizano, Mapatano, Mambo ya Muziki, Wasanii, na Michezo.
Siku ya Jumapili inatawaliwa na Sayari ya Jua
ambayo inahusika na Kiburi, Nguvu, Ufahari, Kuona haya, wanasiasa,
madereva, mafundi wa mambo ya moto na magari.
Huu Mwaka wenyewe 2013 namba mbili za mwisho 13 ukizijumlisha unapata 4 ambayo ni nyota ya Kaa au Cancer
ambayo inahusikana ,Kilimo, Mapenzi, Unyonge, Kufanya vitu kwa
vishindo, Siri na kuvumbuka kwake, Kuvunjika biashara na kutimia kwa
haja, Mvua na Mafuriko na Majanga ya asili.
KUTOKANA NA HAYO MAELEZO:-
Hali ya Kijamii:
Natabiri: kwamba katika Mwaka huu wa 2013
Ndoa nyingi zitavunjika. Watu wengi, wakiwemo Mawaziri na Viongozi
Waandamizi wake kwa waume, watajikuta katika kashfa ya Ngono, Kufumaniwa au kufumania na kupigana kiasi cha baadhi yao kuuawa.
Natabiri; Kuwa maisha katika mwaka huu yatakuwa mazuri, lakini kwa Watanzania watakaojifunga mikanda kuelekea katikati ya mwaka 2013.
Natabiri: Maradhi ya watoto kuongezeka
katika Mwaka huu wa 2013 na hasa ya kifua na kichwa. Wanawake wengi
wajawazito watapoteza maisha kwa kujifungua na au kuzaa kwa matatizo
makubwa ambayo hayajawahi kuonekana.
Natabiri: Ajali zitakuwa nyingi, kuchafuka kwa bahari kutakuwako kwa wingi na kutakuwa na hofu ya watu wengi kuuawa.
Natabiri: Kutokea kwa mioto mikubwa
kwenye miji mikubwa, Njaa kuongezeka, ukosefu wa maadili, wafanyakazi
kuwapiga mabosi wao, uongo mwingi kwa maana ya propaganda.
Natabiri: Umbeya utakua kwa kiwango kikubwa mwaka huu wa 2013, pamoja na masengenyo.
Natabiri vifo vya Mashujaa au wale watakojiona ni mashujaa.
Natabiri: wingu zito la vifo vya ghafla kwa
watunzi wa hadithi na vitabu, Waandishi wa habari, Wanasiasa na Wasanii
na muda huu itakuwa mbaya zaidi ya mwaka jana.
Hali ya Kisiasa:
Natabiri: Viongozi wengi wakiwemo
Wabunge, Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wenyeviti wa vyama na Makatibu wao
watatoa matamshi ya utatanishi na kusababisha khofu na mitafaruku
mikubwa itakayowafanya watu kupigana.
Hata hivyo, hali hiyo itadumu kwa muda mfupi.
Kwani baadhi ya viongozi watalazimika kukaa pamoja na kukubaliana mambo
baina yao na kurejesha hali ya utulivu na amani.
Natabiri: Wabunge wengi katika Bunge la
Jamhuiri ya Muungano wa Tanzania wataungana katika masuala yatakayohusu
Utaifa bila kujali itikadi zao za kivyama au kimajimbo. Hata hivyo,
nyota zinaonesdha kuna baadhi ya wabunge wataanguka Bungeni wakati wa
majadiliano.
Kinyota haionekani kuwa kutakuwa na athari lakini itapaswa kufanyika juhudi za ziada kuokoa maisha yao.
Natabiri Rais Jakaya Kikwete maarufu
kama “JK” kufanya mambo ya ajabu na yasiyotabirika na ataungwa mkono
kwa asilimia 100 na wananchi wote wa Bara na Visiwani.
Natabiri JK atatenda maamuzi magumu katika mwaka 2013 kiasi cha dunia kushangaa.
Natabiri: JK ataendelea kupata wasaidizi
sadifu hasa kwa upande wa Uwaziri. Vile vile nyota za Mawaziri Harrison
Mwakyembe, John Pombe Magufuli na Khamisi Kagasheki zitazidi kungara
Mwaka huu na kuungwa Mkono na Wananchi.
Natabiri JK ataunganisha nchi na kuwa
moja yenye uimara wa Utaifa kuliko watangulizi wake. na atashirikiana
zaidi na Wanasiasa na viongozi wa dini kuondoa mtikisiko wa uvunjifu wa
amani uliokuwapo nchini mwaka jana.
Natabiri Chama kimoja cha siasa hapa
nchini kuchochea kujitenga na kuunda Taifa lake. Hata hivyo, kusudio
hilo halitafanikiwa. Kwani litapingwa na Watanzania wote kwa kauli na
vitendo.
Natabiri:. Natabiri Tanzania kushinda kwa kishindo kwenye mgogoro wake na Malawi kuhusu Ziwa Nyasa bila kupigana vita.
Hali ya Kibiashara:
Natabiri: Mauzo ya bidhaa yataongezeka
na kuongeza neema na watu kufaidika katika biashara. Pia mwisho wa mwaka
huu wa 2013 mvua zitaongezeka na mazao yatakuwa mengi.
Natabiri: Wafanyabiashara wengi na hasa wajasiriamali kufanikiwa katika kazi zao.
Natabiri: Neema itawaangukia wajasiriamali wa aina zote hapa nchini kwa mwaka huu.
Natabiri wawekezaji wengi zaidi mwaka huu watajikita kwenye biashara ndogondogo kuliko ilivyokuwa katika miaka iliyopita.
Natabiri: Sakata la gesi ya Mtwara
litatulia na kumalizika kwa amani katika mwaka huu wa 2013 kwa wananchi
wote kuungana na kuunga mkono matumizi yake kwa faida zaidi ya Taifa
badala ya jimbo au majimbo.
Natabiri: Nchini Kenya ambao ni Majirani zetu Muungano wa CORD
ukiongozwa na Raila Odinga kushinda uchaguzi wa Kenya ambao utakuwa wa
amani na utulivu na kuwashinda Kina uhuru Kenyatta na Ruto na Muungano
wao wa JUBILEE na ule wa Musalia mudavadi unaoitwa AMANI.
Maalim Hassan Yahya Hussein
13/1/2013 Jumapili
No comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII