Pages

Monday, February 11, 2013

JK AMJIBU LOWASSA TATIZO LA AJIRA...SOMA ZAIDI HAPA


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete katika hali inayoashiria kumjibu rafiki yake, Edward Lowassa ameponda makada wa chama hicho ambao wamekuwa wakipanda jukwaani kuhubiri kuwa ajira ni tatizo pasipo kupendekeza suluhisho la tatizo hilo.
Rais Kikwete ambaye alikuwa akifungua semina ya siku mbili ya Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM mjini Dodoma jana, alisema kusimama jukwaani na kusema kwamba ajira ni tatizo hakuna maana ikiwa mhusika hatoi pendekezo la jinsi ya kumaliza tatizo hilo.
Ingawa hakutaja majina ya wanasiasa ambao wamekuwa wakizungumzia suala hilo lakini Lowassa, ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008,  amenukuliwa mara nyingi akiitaka Serikali kuchukua hatua za kukabiliana na tatizo la ajira kwa maneno kwamba ‘ni bomu linalosubiri kulipuka’.
Lowassa, ambaye ni Mbunge wa Monduli kupitia CCM,  aliwahi kuingia hata kwenye malumbano makali na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka.
Kabaka akiwa bungeni mjini Dodoma, Machi 21, 2012 alilazimika kutoa takwimu za namna Serikali ilivyokuwa inatengeneza ajira kwa nia ya kumjibu Lowassa, ambaye alikuwa ameeleza tatizo la ajira linavyowaathiri vijana kwenye moja ya hafla.
Lowassa ameendelea kuzungumzia suala hilo mara kwa mara kila anapopata fursa ya kuhutubia.
“Ndiyo ajira ni tatizo, hapa mkakati ni ajira itapatikana vipi? Ni tatizo kweli, tunafanyaje na tunalitatua vipi? Tunataka mtu anayesema kwamba ni tatizo na apendekeze pia suluhu yake,” alisema Rais Kikwete, ambaye aliwahi kutamka kuwa Lowassa ni rafiki yake na anafahamika kuwa alishirikiana naye katika harakati zake za kuwania urais mwaka 2005, na baadaye akamteua kuwa Waziri Mkuu.
Lowassa, ambaye ni miongoni wa makada wa CCM wanaotajwa kuwania urais mwaka 2015, alikaririwa akisema Oktoba 19,  2011 kuwa; “Sijakutana na Rais Kikwete barabarani, watu waache kunichonganisha naye.” Ilikuwa katika mkutano na waandishi wa habari jimboni kwake Monduli.
Suala la ajira nchini ni moja ya mada zinazotarajiwa kuwasilishwa kisha kujadiliwa katika semina hiyo ya CCM, na Rais Kikwete aliwataka wajumbe kupendekeza jinsi ya kuongeza ajira nchini wakati mjadala husika utakapowadia.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema hivi sasa ajira katika sekta ya umma ni kama hakuna, kwani zimebaki sekta za afya na elimu na kwamba hivi sasa suluhu ni kukuza sekta binafsi ili kuongeza ajira.
Alitoa mfano kwamba wakati yeye alipohitimu kidato cha nne, cha sita na chuo kikuu hakukuwa na tatizo la ajira kwa kuwa idadi ya wasomi ilikuwa ndogo ikilinganishwa na mahitaji ya sasa ya soko hilo.
Kikwete alisema wakati huo Serikali ilikuwa haijajitosheleza, tofauti na sasa ambapo imefikia ukomo wa kuajiri isipokuwa kwa sekta mbili tu.
“Kwa sasa Serikali haina uwezo tena wa kuajiri, ilifika mahali kila kiongozi anaenda kuomba serikalini na kupeleka watu wake, unakuta anatoka Kikwete anaomba mtoto wake aajiriwe, mara Katibu Mkuu naye anapeleka watu wake, ikafika mahali mashirika yakajaa tukapata kazi ya kuwapunguza,” alisema Rais Kikwete.

SOURCE: MCL

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII