MBOWE: "TUTASHIKA DOLA 2015 KIRAHISI ZAIDI"...SOMA NA MENGINE ALIYOYASEMA

 
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema sera mpya ya majimbo itakiwezesha chama hicho kushika dola na kuongoza nchi kwa urahisi zaidi.

Akifungua kikao cha kazi za Chadema kilichofanyika jijini hapa jana, Mbowe alisema sera ya majimbo ni mkakati uliobuniwa na chama hicho kwa lengo la kusogeza madaraka kwa wananchi ili kushiriki kufanya maamuzi ya jinsi ya kuongoza nchi.

Alisema utamaduni, ambao umezoeleka hapa nchini na ambao unatumiwa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kuongoza nchi kutokea Dar es Salaam. Mbowe alisema hatua hiyo imeonyesha kushindwa kuboresha hali ya maisha ya Watanzania wengi.
“Kwa zaidi ya miaka 20 sasa Tanzania tumekuwa na utamaduni wa kutawala nchi kutokea Dar es Salaam. Chadema tumeliona hili na tumegundua kasoro zake. Ndiyo maana tumeamua kuja na sera ya majimbo ili kusogeza madaraka kwa wananchi,” alisema.

Alisema kwa kutumia mfumo huo, CCM imeonyesha kushindwa kushughulikia matatizo ya msingi ya wananchi, ikiwamo mgawanyo sahihi wa rasilimali za taifa. “Pamoja na kusogeza madaraka kwa wananchi, sera ya majimbo inalenga kutaka kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zao tofauti na sasa. Maeneo yenye raslimali nyingi kama madini, ndiyo yenye kiwango kikubwa cha umaskini,” alisema.

Alisema pia kwa kufuata mfumo huo, ndiyo sababu serikali ya CCM imekuwa ikijipanga kuwadhibiti viongozi wa Chadema kila wanapojipanga kwenda kufanya shughuli za kisiasa maeneo mbalimbali nchini.

Alisema kwa kufuata sera ya majimbo, serikali ya CCM haiwezi tena kuwadhibiti viongozi wa Chadema isipokuwa watashtukia chama hicho kimeshika dola na kuongoza nchi.


CHANZO: NIPASHE
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs