Pages

Tuesday, May 28, 2013

HUU NDO UKWELI KUHUSU UJUMBE ULIOENEA SANA KATIKA MSG ZA SIMU ZA WATU KUHUSIANA NA HII NAMBA YA FREEMASON HUU HAPA

Na Makongoro Oging'
HOFU imezuka nchini baada ya namba ya simu inayotajwa kuwa ni ya jamii ya watu wasiomwamini Mungu, Freemason kuhusishwa na umwagaji damu na kafara kutumika kuwapigia watu mbalimbali, Uwazi lina taarifa hii kwa ukamilifu.
Taarifa ambazo Uwazi limezipata, zinaeleza kwamba namba hiyo ni ya Freemason na kwamba, mpigiwaji akijaribu kupokea na kuzungumza, atakuwa ameunganishwa kwenye kafara hiyo.
Baada ya namba hiyo ya kutatanisha kuzuka na kuwapigia watu mbalimbali, inaelezwa kwamba iligundulika kuwa ni ya jamii hiyo na hivyo kusambazwa meseji ya kuwaonya watu wasipokee simu hiyo.
NI NAMBA GANI?
Namba hiyo ni 0800226655 ambayo Uwazi limejiridhisha kuwa si namba ya mtandao wowote wa simu nchini wala nje ya mipaka ya Tanzania, maana hakuna namba kama hiyo.
Ukiachilia mbali kujichanganya kwake, kwa kawaida namba za nje ya nchi huja na alama ya jumlisha, ikifuatiwa na namba za utangulizi za nchi husika, tofauti na namba hiyo.
ONYO LATOLEWA
Kutokana na hofu hiyo, watu wengi wanasambaza ujumbe wa onyo wa kuwataka watu wasijaribu kupokea namba hiyo kabisa ili wasijiunganishe na kafara hiyo.
Uwazi limeambiwa kwamba, ujumbe huo umeanzia makanisani baada ya wachungaji kuwataka waumini wao wasipokee namba hiyo ya kishetani.
Ujumbe wenyewe unasomeka: “Naomba uwe makini kupokea simu. Usipokee endapo utaona namba usiyoijua hasa hii 0800226655 kuanzia leo yaani siku uliyopata ujumbe huu hadi Agosti 17, mwaka huu kwani Freemason wanatoa kafara kwa kusikia sauti tu endapo utapokea simu yao. Siyo utani, tafadhali wajulishe na  wengine uwapendao.”
Uwazi na lenyewe limepata kutumiwa ujumbe huo.
VINGOZI WA DINI
Baada ya yote hayo, mwandishi wa habari hizi aliwatafuta viongozi mbalimbali wa dini akitaka kusikia maoni yao ambapo walitoa ushirikiano wa kutosha.
Sheikh Jumaa wa Dar es Salaam (ameomba msikiti wake usitajwe) alikuwa na haya ya kusema: “Nimesikia kuhusu huo ujumbe na sisi kama viongozi tumewakataza waumini wetu si tu wasipokee hiyo namba bali waache kabisa kupokea namba wasizozijua.
“Tumesema hivyo kwa sababu hawa jamaa wanaweza kubadilisha na kutumia inayofanana na za mitandao ya hapa kwetu Tanzania. Hata hivyo, kubwa zaidi tumewataka kuzingatia zaidi ibada, hiyo ni njia kubwa zaidi ya kukabiliana na madhara hayo.”
ASKOFU JOHN SAID
Askofu wa Kanisa la Victoria lililopo Mabibo External, John Said alisema: “Freemason ni dini ya nguvu za giza, wakati Ukristo ni nuru hivyo hawataweza...kwanza wanaogopa namba zetu kwa kuwa wanajua hawana uwezo wa kutudhuru.”
NABII FLORA PETER
“Ni namba ambazo ni za mashetani, hazina nguvu kwa wale wanaomwamini Mungu. Kikubwa ni kusimama katika imani. Siku zote Mungu ana nguvu kuliko shetani. Ni vyema watu wakabaki kwenye imani sahihi.”
PAROKO KAGABA
Paroko wa Kanisa Katoliki Tabata, Cyprian Kagaba alisema: “Huo ujumbe haujatumwa kwenye simu yangu lakini hata kama ukitumwa, nitapuuza kwa sababu najua ni mambo ya kibiashara tu. Wenyewe wanajua kama ukiwatumia na wengine watanufaika.”

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII