Ilikuwa Juni 18, mwaka huu katika Uwanja wa Soweto
wanachama na wapenzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
walikukusanyika ili kuwaaga watu wanne waliokufa kufuatia bomu
lililolipuka Juni 15, katika uwanja huo.
Tangu bomu hilo lilipolipuka siku hiyo
(Jumamosi), viongozi wa Chadema akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe
walifanya mikutano uwanjani hapo Juni 17 na 18, Japo tayari polisi
walishazungusha utepe katika eneo lililolipukia bomu.
Siku hiyo, saa 9 alasiri wakati mkutano ukiendelea
na viongozi wa chama hicho wakitoa maelekezo ya jinsi ya kuaga maiti,
polisi waliokuwa wamefurika eneo hilo waliwashambulia kwa mabomu ya
kutoa machozi ili kuwatawanya.
Malisa anayeishi Kata ya Ngarenaro jijini humo
alifika uwanjani hapo kumwokoa baba yake Godwin Malisa ambaye ni
mlemavu, alijikuta akipata kipigo cha mbwa mwizi.
“Nilikuwa namfuata baba yangu ambaye ni kada wa
Chadema. Kutokana na ulemavu wake nilihofu angepata matatizo kama vurugu
zingezuka,” anasema Wema na kuongeza:
“Nilikuta uwanja ukiwa umefurika wananchi
wakiwasikiliza viongozi wa Chadema. Viongozi hao ni Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema ambaye alihutubia na kumwachia Tundu Lissu (Mbunge
wa Singida Mashariki) naye akamwachia Said Arfi (Mbunge Mpanda Kati).
Alipomaliza kuwataka wanachama hao waelekee Hospitali ya Mount Meru,
ndipo mabomu yakaanza kulipuliwa.”
Anaendelea kusema: “Nilimwambia baba tuondoke
lakini tulikuwa tumeshachelewa, kwani polisi walikuwa wametuzingira.
bomu la pili liliangukia mbele yetu. Askari mmoja akasema ‘laleni
chini’, tukalala tukidhani tutakuwa salama. Lakini walikuja askari na
kutupiga marungu mwili mzima mimi na baba,”
“Ghafla akatokea askari mwingine akawakataza
wasitupige, tukadhani tumeokoka. Mara wakatokea askari wengine, hapo
ndipo kilikuwa kipigo kitakatifu. Nilijaribu kuwazuia wasimpige baba kwa
kuwa ni mlemavu, wakanikebehi kuwa huyo ni hawara yangu. Walinipiga
mpaka mkono na mguu ya kushoto ikavunjika.
“Tulikuwa kwenye kibaraza cha nyumba wakati askari
wanatupiga. Askari mmoja alirarua gauni langu chini na juu, hadi
nikabaki uchi mbele ya baba. Mwingine akakoki bunduki na kuielekeza
katikati ya mapaja yangu ili alipue sehemu za siri, wenzake wakamkataza.
Mwingine alisema kuwa atanibaka. Baba alinikumbatia akasema watuue
wote, mimi niliomba wasituue maana nimeacha mtoto mchanga nyumbani.”
Anasema askari walikuwa wakimbeza kwa kumuuliza kwa nini yeye ni mwanachama wa Chadema.
“Walisema ‘unajifanya wewe Chadema, sasa ndiyo
utajua kuwa CCM inatawala. Chezea CCM wewe.’ Mimi niliwaambia sina chama
chochote nimekuja kumwokoa baba yangu. Wakati huo wote walishanivua
hereni, simu wakachukua na fedha zilizokuwa ndani ya pochi na kuitupa
chini ikiwa tupu.”
Maelezo ya baba yake
Kauli ya Serikali
Hata hivyo Wema anasema alikuja askari wa kike aliyekuwa akipiga
picha za matukio na kuwasaidia. Wakati huo watu wote wameshatawanyika
uwanjani hapo na askari wameshaanza kujipanga baada ya kuitwa kwa
filimbi.
“Alitusikitikia na kusema, ‘kwa nini
mnang’ang’ania kuwa Chadema? Angalieni sasa mlivyoumia na viongozi wenu
wamewakimbia.’ Akaokota kanga iliyoachwa uwanjani na kuja kunifunika,”
anasema na kuongeza:
“Kisha likaja gari la polisi tukabebwa na
kuingizwa humo. Mwendo tuliondoka pale ulikuwa wa kasi huku wakiendelea
kulipua mabomu na kutukanyaga bila kujali. Tulishtukia tuko Hospitali ya
Mount Meru, tukabwagwa hapo na gari hilo likaondoka.”
Wema anasema walitibiwa kwa siku kadhaa kabla ya kuruhusiwa ili kuugulia nyumbani.
Maelezo ya baba yake
Baba yake Wema, Godwin Malisa japo hakupata majeraha makubwa, anaendelea kuugulia maumivu makali ya mwili mzima.
“Kilichonisikitisha ni kitendo cha kumpiga na
kumdhalilisha mwanangu mbele yangu. Askari wengine walikuwa wakijaribu
kuvunja hili gongo ninalotembelea kwa sababu ya ulemavu,” anasema Malisa
na kuongeza:
Alalamikia kauli ya Pinda
“Nimesikitishwa na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo
Pinda aliyoitoa hivi karibuni Bungeni Dodoma ya kuwataka askari
waendelee kupiga wananchi. Kwa hali hii sisi wanyonge natuna pa
kukimbilia.”
Akisimulia zaidi, Malisa anasema, siku hiyo licha
ya watu kuwa wengi katika uwanja huo, Jeshi la Polisi halikufuata kanuni
zake za kutoa ilani kwa wananchi kabla ya kuanza kushambulia.
Licha ya Jeshi la Polisi mkoani Arusha kusema
hakukuwa na majeruhi siku hiyo, inaelezwa kuwa wengi walijeruhiwa kwa
kupigwa na polisi.
Kauli ya Serikali
Akijibu maswali ya wabunge hivi karibuni bungeni mjini Dodoma,
Waziri Mkuu Mizengo amewahimiza polisi kuendelea kuwapiga wananchi
wanaokiuka sheria, kwa kuwa nchi inafuata utawala wa sheria.
“Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki wewe
ukakaidi, utapigwa tu...Maana hakuna namna nyingine. Maana lazima wote
tukubaliane kuwa nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria. Sasa
kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba wewe ni imara zaidi, ni jeuri,
watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu kwa sababu hakuna nyingine eh…
maana tumechoka sasa.”
SOURCE : Mwananchi Monday 24 June, 2013
SOURCE : Mwananchi Monday 24 June, 2013
No comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII