Pages

Sunday, June 16, 2013

WAFUASI WA CCM NA CHADEMA WAKATANA MAPANGA HUKO IRINGA...BOFYA HAPA KUSOMA HABARI KAMILI

MWENYEKITI wa Baraza la Wazee wilayani Kilolo, Lunyiliko Nyaulingo amelazwa katika Hospitali ya mkoa Iringa na Mwenyekiti wa CHADEMA Mgololo amelazwa Hospitali ya wilaya ya Mufindi baada ya kujeruhiwa vibaya na watu wanaodaiwa ni wanachama wa CCM katika kampeni za mwisho za kuwania nafasi ya udiwani.

Sambamba na hiyo Katibu wa CCM kata ya Ng’ang’ange wilayani Kilolo, Wilhad Ngogo (40) na Yohana Mchafu anayedaiwa kuwa ni mwanachama wa CCM wanashikiliwa na Polisi kwa kuhusika na matukio hayo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema watu hao walikamatwa jana kufuatia 
vurugu zilizojitokeza kwenye mikutano ya kampeni ya mwisho katika wilaya hizo mbili.

Alisema kufuatia mzozo huo wanachama wa CHADEMA walizuia barabara ya Iringa-Mbeya kwa kuweka magogo ili kuzuia magari kupita na kuwa Polisi wanamtafuta Rabart Sam maarufu kwa jina la Kideri kwa kuongoza vurugu hizo.

Kamanda Mungi alisema wanafanya uchunguzi wa kina juu ya matukio hayo na uchunguzi ukikamilika watafikishwa mahakamani.

Aidha alitoa wito kwa viongozi wote wa vyama vya siasa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kuepusha vurugu ambazo zinaweza kutokea.

Leo Uchaguzi wa udiwani katika kata ya Ng’ang’ange wilayani Kilolo na Mbalamaziwa wilayani Mufindi ulifanyika ambapo Zuberi Nyomolelo (CCM) na Ezekiel Mlyuka (CHADEME) walipambana kwa kata ya Mbalamaziwa na kwa upande wa Ng’ang’ange Kilolo Nafred Chahe (CHADEMA) na Namgalesi Msuva (CCM) walipambana.

--
via Mjengwa

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII