STAA wa filamu na muziki wa Bongo Fleva, Zuwena Mohammed ‘Shilole’ ameingia matatani akidaiwa kuingia mitini na simu tatu za mkononi alizoaminiwa nchini Afrika ya Kusini alikokwenda kufanya shoo.
Mfano wa aina ya simu anazo daiwa kuiba Shilole
Msanii huyo alikumbwa na kasheshe hilo Julai 19, 2013 nyumbani kwa
mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’, Sinza Mori, Dar.Siku hiyo Diamond alikuwa akifuturisha na aliwaalika watu mbalimbali wakiwemo mastaa lakini nusura futuru iingie doa kufuatia zogo hilo.
ISHU ILIKUWAJE?
Ndugu wa Diamond aitwaye Majaliwa Majuto ‘Q Boy’ alidai ndiye mwenye simu hizo. Alisema miezi kadhaa iliyopita, Shilole alikwenda nchini humo kufanya shoo ya muziki. Wakati wa kuondoka alimpa simu tatu, Ipad, Samsung Galaxy na Blackberry ili akifika Bongo ampe Diamond lakini msanii huyo hakufanya hivyo.
“Alikuja Sauzi kufanya shoo, wakati wa kuondoka nilimpa simu tatu amletee Diamond lakini nashangaa hakufanya hivyo na mimi tangu nirudi Bongo simpati, kila nikimpigia simu hapokei, leo ndiyo tumekutana hapa kwa Diamond,” alilalama Q Boy.
DIAMOND ALIAMBIWA SIMU ANAZO SHILOLE
Alisema awali akiwa nchini humo baada ya kumkabidhi mali hizo, alimpigia simu Diamond na kumtaarifu kuwa ‘mzigo’ anao Shilole, akashangaa staa huyo kujibu kwamba hajazipata wala hajamwona Shilole.
SHILOLE AJITETEA
Katikati ya mzozo huo, Shilole alijitetea kwa kusema: Mi namdai rafiki yake fedha yangu ya shoo iliyobaki, kama shilingi laki nane hivi ndiyo maana nikaamua kuzizuia simu za huyu (Q Boy) hadi nimaliziwe pesa yangu.
Hata hivyo, katika sakata hilo ilielezwa kuwa Shilole na Q Boy hawakuwa na makubaliano yoyote kuhusu shoo hiyo na simu hizo hivyo madai ya mwigizaji huyo ni ‘usanii’ tu.
MAMA DIAMOND AINGILIA KATI KUOKOA
Zogo hilo lilipopamba moto na kuashiria kuvurugika kwa amani, mama mzazi wa Diamond, Sanura Kasim ‘Sandra’ aliamua kuingilia kati na kuagiza suala la kudaiana simu lifanyike kesho yake (Jumamosi) kwa vile siku hiyo haikuwa muafaka.
“Jamani! Jamani! We nani, Shilole na we Majaliwa, naomba kwa leo muepusheni shetani kwani hapa si mahali pake, ila kesho tutaitana na kumaliza suala hili, mimi mwenyewe nitalisimamia,” alisema bi mkubwa huyo na kumaliza henyahenya iliyoibuka.
JUMAMOSI YAFIKA, KIKAO VIPI?
Jumamosi, mapaparazi wetu walifuatilia ishu hiyo nyumbani kwa akina Diamond na kuulizia ili kujua kama kikao cha usuluhishi kilifanyika kama mama Nasibu alivyoagiza.
“Mh! Sijaona kikao chochote, kwanza Shilole mwenyewe akipigiwa simu hapokei,” alisema ndugu mmoja wa Diamond huku akiomba hifadhi ya jina lake.
MSIKIE DIAMOND
Juzi, Diamond alipopigiwa simu na kuulizwa kama anaijua ishu ya simu, alikubali.
Staa huyo alisema anashindwa kuingilia kati sakata hilo kwa sababu wahusika wote ni watu wake wa karibu kikazi.
“Yeah! Ishu ni kweli ipo, lakini mimi nilijiweka kando mapema, nikamwambia dogo (Q Boy) afuatilie mwenyewe baada ya kuona Shilole haeleweki.
“Unajua Shilole ni mwanamuziki mwenzangu, dogo yupo ndani ya Kampuni ya Wasafi Entertainment (ya Diamond), sasa kukomaa na ishu za simu tu nahisi itanishushia hadhi, napiga shoo za hela nyingi halafu leo nakomaa kwa hela ndogo, inakuwa siyo,” alisema Diamond.
SHILOLE TENA
Baada ya kuzungumza na Diamond, Shilole alipigiwa simu na kuomba kufafanua kwa undani ishu hiyo ambapo katika hali isiyotarajiwa, alimlalamikia paparazi wetu akidai anapendelea katika sakata hilo.
“Nyiye mnamtetea tu yule dogo, mimi sina tatizo, kama rafiki yake (aliyemuitia shoo Afrika Kusini) akinilipa hela yangu nawapa simu zao,” alisema Shilole.
Msanii huyo alikwenda mbele zaidi kwa kumwambia paparazi kuwa atatia timu kwenye Ofisi za Global Publishers ili kuzungumzia suala hilo na viongozi.
Baadaye Shilole alifika ofisini kwetu na kufafanua juu ya sakata hilo ambapo alirudia kukiri kuzuia simu hizo akidai kwamba anamdai Q Boy hivyo mpaka atakapomlipa ndiyo atampa simu zake.
Q BOY NAYE TENA
Kwa upande wake, Q Boy alipozungumza na paparazi wetu siku hiyo alisema amekusudia kwenda kufungua kesi kituoni ili apewe msaada zaidi wa kisheria kwa vile simu hizo zinamuuma hasa ukizingatia kuwa yeye siye aliyempeleka Shilole Afrika Kusini kufanya shoo.
“Mimi leo (Jumatatu) nimebanwa sana, kuna sehemu nakwenda na Diamond, nadhani nitamaliza jioni. Lakini kesho (Jumanne) nitaamkia polisi kufungua kesi nione watanisaidiaje?” alisema Q Boy.
POLISI AGUSIA ISHU
Risasi Mchanganyiko lilizungumza na askari mmoja kutoka Kituo cha Polisi cha Oysterbay na kummegea mtiririko wote, kisha kumuuliza kama kuna kesi ambapo alijibu:
“Japokuwa mimi si msemaji wa jeshi (la polisi), lakini ishu kama hiyo shitaka lake lipo, ni wizi wa kuaminiwa. Unajua wengi wanadhani kuibiwa lazima mtu uwe hujui, lakini mtu akifanya kama hivyo alivyofanya huyo msanii nani sijui (Shilole), kama ni kweli, kosa linakuwa wizi wa kuaminiwa endapo atafikishwa polisi.”
DIAMOND, Q BOY WALIFANYA MCHEZO?
Hata hivyo, baadhi ya watu walioshuhudia sakata hilo walikuwa na maswali kibao yaliyokosa majibu.
Swali la kwanza: Shilole alikwenda kufuturu kwa mwaliko wa Diamond na alijua staa huyo na Q Boy ni wamoja na simu alizopewa ilikuwa amletee msanii huyo, kwa nini alikwenda huku akijua ana msala?
Swali la pili: Kama Shilole alikwenda akijua Q Boy hayupo Bongo, je! Si kwamba ulikuwa mpango wa wawili hao kumwita ili wampe kibano ateme simu zao?
Swali la tatu: Je, ni kweli Shilole alizuia simu ili amaliziwe deni lake kwa mtu aliyemuitia shoo Afrika Kusini au shetani alimwingia baada ya kutua Bongo na kuamua kuzitumia hasa ikizingatiwa kuwa siku hizi mambo ya Instagram ndiyo habari ya mjini?
No comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII