Dodoma.
Jana, Bingwa wa Dunia wa uzani wa kati (super middle), unaotambuliwa na Shirikisho la Ngumi Duniani (WBF), Francis Cheka alitembelea Bunge baada ya kutwaa taji hilo karibuni na jana hiyohiyo, Bunge hilo lilishuhudia ngumi kavukavu katika vurugu kubwa pengine kuliko zote zilizowahi kutokea katika ukumbi wake.
Katika masumbwi hayo yasiyo rasmi, Mbunge wa Mbeya
Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ anadaiwa kumpiga kichwa Askari
wa Bunge na kumchania sare na kung’oa kipaza sauti.
Mbilinyi jana alisema alikuwa anatafutwa na polisi
huku akisema hilo limemshangaza akidai kwamba yeye ndiye
aliyeshambuliwa na askari huyo.
Vurugu hizo zilitokea baada ya Naibu Spika, Job
Ndugai kuamuru kutolewa nje kwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, Freeman Mbowe.
Katika vurugu hizo Mbilinyi alibebwa juujuu na polisi hadi nje ya ukumbi huku akiwa hana viatu.
Pamoja na tafrani hiyo, Ndugai alisema wakati
akihitimisha kikao cha Bunge kipindi cha asubuhi kuwa amewasamehe
wabunge wote waliohusika na kosa hilo la utovu wa nidhamu na kuwaruhusu
kurejea kipindi cha jioni kuendelea na Muswada wa Marekebisho ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba. Hata hivyo, wabunge wote CUF, NCCR-Mageuzi na
Chadema ambao baada ya tukio hilo walitoka nje ya ukumbi, hawakurejea na
baadaye walitoa msimamo wa pamoja wakisema hawatashiriki katika mjadala
huo.
Msimamo huo ulitolewa na Mbowe ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Chadema, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia na
Mbunge wa CUF, Habib Mnyaa.
Mbowe alisema wameamua kususia majadiliano hayo kuonyesha msimamo wao wa kupinga kupitisha mambo yasiyo na masilahi kwa nchi.
“Hatuko tayari kushiriki katika uchakachuaji wa
Katiba... Matumizi ya nguvu ya polisi kamwe hayatatupatia Katiba nzuri,”
alisema. Alisema kambi rasmi ya upinzani inalaani vikali kitendo cha
Ndugai kuruhusu Bunge kunajisiwa kwa kuruhusu polisi kuingia ndani
kinyume na kanuni.
Mnyaa alisema kitendo cha wadau wa Zanzibar
kutoshirikishwa katika kutoa maoni yao katika muswada huo wa marekebisho
ni dharau kubwa.
Mbatia alisema Tanzania haiwezi kuingia Uchaguzi
Mkuu wa 2015 kwa kutumia Katiba ya sasa kwa sababu tayari kuna mgongano
wa kikatiba kati ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu
Lissu alimtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kuu, (Sera, Uratibu na
Bunge), William Lukuvi kutoa ushahidi kama Rais aliteua wajumbe wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba kulingana na mapendekezo ya taasisi zao.
Kuanza kwa tafrani
Sakata hilo lilianza saa 6:45 mchana muda mfupi
baada ya kukamilika kwa kura kuamua kama Bunge liahirishwe au la
kutokana na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Mkoani (CUF), Ali Hamisi Seif
(CUF). Waliotaka liahirishwe walipata kura 59 na waliokataa 159.
Baada ya Ndugai kutangaza matokeo hayo na kutaka
shughuli za Bunge ziendelee, Mbowe aliposimama na kusema ana hoja Naibu
Spika alimwamuru akae chini.
Baada ya Mbowe kusisitiza ana hoja na kumwomba
Spika amsikilize ndipo Ndugai alipomwamuru atoke nje na alipokaidi
alisema:” Naomba askari wote waliopo katika mazingira haya (ya Bunge)
waingie ndani ya ukumbi wa Bunge”.
Baada ya kitambo kifupi, Mbowe akiwa bado amesimama alitoa maagizo atolewe nje: “Kiongozi wa upinzani atolewe nje.”
Polisi waliingia ndani ya Ukumbi wa Bunge lakini
Wabunge wa Kambi ya Upinzani kwa umoja wao, walimzinga Mbowe asifikiwe
na askari hao.
Baada ya kuona polisi wanaelekea kushindwa, Ndugai
alitoa maagizo mengine: “Askari hamjaletwa humu ndani kufanya
majadiliano mnatakiwa kuhakikisha kiongozi wa upinzani anatolewa nje”.
Alisema yeye ndiye anayeendesha kikao hicho hivyo lazima Mbowe atolewe nje.
Hapo ndipo wabunge hao wa upinzani walipoanza
kuimba: “Hatutaki kuburuzwa hatutaki kuburuzwa… hatutaki kuonewa,” huku
wakiendelea kumzinga Mbowe.
“Askari wote mliopo humu ndani naomba mnisikilize… Sasa naagiza kwa mara ya mwisho... nasema kiongozi wa upinzani atolewe nje.”
Ngumi zarushwa
Baada ya kauli hiyo ya Ndugai, ndipo polisi walipotumia nguvu
hasa kwa Mbilinyi na Mbunge wa Maswa Mashariki (Chadema), Silvester
Kasulumbai.
Katika patashika hiyo, inadaiwa kwamba Mbunge wa
Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali alipigwa ngumi ambayo
ilimfanya apepesuke hadi sakafuni.
Kilichomponza Mbilinyi ni hatua yake ya kusogelea Siwa. Polisi waliokuwa karibu, walimbeba juujuu hadi nje ya ukumbi.
Wakati akitolewa nje ya ukumbi, alijaribu kujizuia kwa kushika kipaza sauti kinachotumiwa na upande wa upinzani hadi kikang’oka.
Mbunge wa Viti Maalumu (CUF), Mozza Abeid,
alivuliwa hijabu katika vurumai hizo wakati polisi walipokuwa wakitumia
nguvu ili kumfikia Mbowe.
Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya, Mbowe
aliamua kutoka nje huku akisindikizwa na polisi pamoja na wabunge wa
vyama hivyo na alipofika nje ya ukumbi alipokewa na polisi wa kawaida
waliomweka chini ya ulinzi kabla ya kumwachia baada ya ombi la Mbunge wa
Rombo (Chadema), Joseph Selasini.
Kutokana na hali ya mambo kuwa tete, askari wa
Bunge waliwaondoa wageni waliokuwa wamekaa katika kumbi za wageni
wakiwamo wanafunzi wa shule mbalimbali za sekondari huku baadhi ya
wabunge wa CCM waliokuwa na simu za kisasa za mkononi na kompyuta
mpakato (Ipad) wakichukua picha za tukio zima.
Inadaiwa kwamba baada ya kutoka nje ya ukumbi,
Mbilinyi alimtwanga ngumi mmoja wa askari waliomtoa kwa nguvu kabla ya
kuamuliwa na wabunge na polisi.
Wakati wote huo, wafanyakazi wa Bunge na wageni
walionekana wakiwa wamejikusanya katika makundi wakitafakari na
kushangaa yaliyokuwa yakitokea.
Balaa lilivyoanza
Akitumia Kanuni ya 69(1), Mbunge wa Mkoani (CUF),
Ali Hamisi Seif, alitaka kuahirishwa kwa mjadala wa Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013 kutokana na
ukweli kuwa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala ya Bunge ilipaswa
kukusanya maoni ya wadau mbalimbali nchini ikiwamo upande wa Zanzibar
jambo ambalo halikufanyika wakati wa maandalizi ya muswada huo.
Source Mwanachi
Source Mwanachi
No comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII