NIMEIPENDA HII, HEBU SOMA THEN UTOE MAONI YAKO PIA
FAHAMU HISTORIA YA DIAMOND, NA UJUE KWA NINI DIAMOND NI TAJIRI KUSHINDA GURUMO, JAPOKUWA GURUMO KAANZA KUIMBA KABLA DIAMOND HAJAZALIWA
MWAKA 2005 nilikuwa nikipanda daladala na Naseeb Abdul (Diamond) katika kituo cha Shule Tandale Magharibi jijini Dar es Salaam. Wakati huo, sikuwa hata na wazo kwamba atakuja kuwa mtu maarufu katika muziki hata kushughulisha watu kutaka kujua zaidi kuhusu maisha yake.
Baada ya hapo nikaanza kuona
wimbo wake wa kwanza kwenye video, ‘Nenda Kamwambie’ kilikuwa kibao
kizuri kilichompa umaarufu, ndipo alipoanza kunivutia kusikiliza nyimbo
zake. Baada ya video ile sikumuona tena kituoni kama ada yetu, nikaanza kusikia anaendesha gari aina ya Toyota Celica.
Kutoka mwaka 2006 mpaka sasa ni mfululizo wa mafanikio aliyoendelea
kuyapata kijana huyu aliyezaliwa Septemba 28, 1988 mpaka kuwa
mwanamuziki wa kwanza Tanzania kulipwa pesa nyingi kutokana na shughuli
hiyo.
Kutokana na utafiti uliofanywa na tovuti inayozungumzia masuala ya
vijana inasemekena ‘Diamond Platnamz’ anapata kiasi cha Sh Mil 16 kwa
matamasha mawili anayofanya katika mwezi.
Mbali ya mikataba minono aliyoingia na makampuni mbalimbali
yanayonufaika kwa taswira ama sauti ya mwanamuziki huyo kijana, Diamond
anaingiza fedha nyingi kila anaposafiri nje ya Tanzania na bara la
Afrika kufanya matamasha ya muziki.
Wakati Diamond, ambaye hajatimiza hata miaka kumi kwenye tasnia ya
muziki kuna mtu mmoja anaitwa Muhidini Gurumo, amejishughulisha na
muziki kwa takriban miaka 45 lakini kila alipokutana na swali hili
kutoka kwa wanahabari kuwa kwa kipindi chote hicho muziki umemsaidia
nini, jibu lake ni: “Bado hakuna ninachoweza kujivunia kupitia muziki,
hali ya maisha ni ngumu.”
Gurumo ambaye alizaliwa 1940 alianza muziki mwaka 1959 akiwa na bendi ya
Kilimanjaro Chacha Band. Sasa ni takriban miaka 45, umri wa baba mwenye
wajukuu lakini alichofanikiwa ni kujenga nyumba mbili na kupata shamba
moja. Gari lenyewe alizawadiwa na Diamond mwaka huu baada ya kulalamika
sana kwenye vyombo vya habari.
Nini Tatizo
Maalim Gurumo (Kamanda), analalamika kuwa wanamuziki wa kizazi kipya
wanasifiwa sana na vyombo vya habari. Akisisitiza kuwa hawana ubunifu,
nyimbo zao hazina athari katika jamii na hudumu chini ya mwaka mmoja
zinapoteza taswira.
Lakini amesahau kuwa wanamuziki wa sasa wengi wamejiajiri, kipindi hicho
bendi nyingi zilimilikiwa na kampuni, taasisi ama mtu ambaye anapenda
sanaa hiyo ya muziki.
Lakini sasa wanamuziki wameamka, wanajimiliki wenyewe pesa wanazopata zinaingia mifukoni mwao.
Mathalan tangu Diamond aanze kuimba ameshaingia zaidi ya mikataba kumi
tofauti ambayo ilimnufaisha yeye kama Diamond, matamasha yake
yanamnufaisha yeye, kikundi anachomiliki anakilipa kiasi
wanachokubaliana kutokana na uwezo wa mwanakikundi.
Mwaka jana, 2012, Diamond aliingia mkataba na kampuni ya I-View Studios
wa kusimamia kazi zake zote kwa miaka miwili. Huu ni mkataba ambao
umemjengea heshima kubwa sana. Ingawa kiasi cha malipo kilifanywa siri
lakini inaonekana ni mkataba mnono.
Kampuni nyingine ya One Touch, ilifunga naye mkataba wa kuwa wasemaji
wake. Yaani kila anachotaka kufanya ama kuzungumza kwenye jamii, ikiwa
kuna kampuni inataka kufanya naye mazungumzo ya kibiashara, One Touch
Company ndio watakaofanya kazi hiyo.
Hilo tu linamfanya Diamond awe na uwezo mkubwa wa kupata fedha kutokana
na muziki. Mara nyingine msanii anashindwa kujua thamani yake, anaweza
kutaja kiasi kidogo cha fedha katika ‘dili’ kubwa. Lakini kwa kupata mtu
wa kukusimamia kwenye mazungumzo ya kifedha lazima uwe tajiri.
Aidha, bendi ambazo Maalim Gurumo amehama kutokana na sababu za
kimaslahi hazipungui kumi, alianza na Kilimanjaro Chacha Band, Kilwa
Jazz Band, NUTA Jazz Band, Mlimani Park, Safari Sound Ochestra, Rufiji
Jazz, na nyingine nyingi kabla ya kumalizia muziki kwenye bendi kongwe
ya Msondo Ngoma Music Band.
Kote huko alizunguka kwa kutumia kichwa kitupu kujadili thamani ya sauti
yake, hakuwa na mshauri wa masuala ya muziki ambaye atamwambia kutokana
na thamani yako usikubali kuhama bendi hii ili kuenda bendi nyingine
bila kupewa kiasi fulani cha fedha.
Aliweza kuitwa baa akawa anakunywa bia na nyama choma huku anajadili
mustakabali wa maisha yake na mkurugenzi wa bendi pinzani na anayofanyia
kazi.
Katika mazungumzo yake na wanahabari Maalim Gurumo aliwahi kutamka kuwa
anatamani siku zirudi nyuma ili anufaike na muziki wake. Lakini nakataa,
hata awe vipi kutokana na mfumo anaoutumia hawezi kuwa tajiri kama
Diamond.
Leo hii, Maalim Gurumo akiandaa tamasha na kuingiza Sh Mil 50, basi
atakachoambulia ni asilimia 10 ya mapato ambayo ni Sh Mil 5, ambacho
kitakuwa ni kiasi kikubwa kuwahi kukipata kwa tamasha moja tangu aanze
kuimba.
Lakini siku hiyohiyo Diamond akialikwa katika tamasha hilo la Gurumo
ataondoka na Sh Mil 8 taslimu bila kupungua senti. Bado tofauti ipo
kubwa.
Aidha, mbali ya mapato ya stejini lakini Diamond ana mikataba minono na
makampuni ya simu ambayo yanatumia nyimbo zake kama miito ya simu, ana
mkataba mwingine mnono na kampuni ya Vodacom, ana mkataba na kampuni ya
vinywaji baridi ya Coca Cola hata kufikia kujiita Coke Boy.
Tukiwakusanya wanamuziki wa zamani kuanzia Mbaraka Mwinshehe mpaka
kufikia Maalim Gurumo, bado hawawezi kufikia mafanikio ya muda mfupi
aliyoyapata kijana mdogo Naseeb Abdul ‘Diamond’ ambaye hata ladha ya
ndoa hajaionja kutokana na umri wake kuwa mdogo.
Wakati Gurumo akijisifia nyumba mbili alizojenga kwa tamu, Diamond ana
nyumba zaidi ya mbili ambapo moja amemjengea mama yake yenye thamani
inayofikia zaidi ya Sh Mil 50.
Pengine Gurumo ni mwanamuziki bora zaidi kuliko Diamond lakini mwenziye amemzidi kwenye ujanja wa kutafuta fedha
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII