Pages

Sunday, December 22, 2013

MAUAJI HAYA MPAKA LINI?? WATOTO WA DIWANI WA CCM HUKO MBEYA WAUAWA KWA KUNYONGWA..SOMA ZAIDI

Diwani wa kata ya Nkangamo Weston Simwelu akifarijiwa na Diwani mwenzake wa Kata ya Tunduma Frank Mwakajoka mara baada ya Bw. Simwelu kufiwa na watoto wake wawili kwa kuchinjwa na kunyongwa
Katibu Uchumi na Fedha wa Kata ya Tunduma akimfariji Diwani wa Nkangamo Weston Simwelu ambaye watoto wake waliuawa kinyama kwa kuchinjwa na kunyongwa mjini Tunduma.
Mke wa Diwani wa kata ya Nkangamo Tumaini Yohana akifarijiwa na ndugu na jamaa mara baada ya kutokea kwa mauaji ya kinyama nyumbani kwake ambapo mwanaye aliuawa kwa kuchinjwa na mfanyakazi wake wa ndani aliuawa kwa kunyongwa.
Jeneza lenye mwili wa msichana wa kazi wa Bw. Simwelu, Sista Nyirenge likiwa tayari kwa kusafirishwa kwa ajili ya mazishi katika kijiji cha Isansa wilayani Mbozi
Diwani wa kata ya Tunduma Frank Mwakajoka (kulia) na kiongozi wa mtaa huo Stanslaus Malekela wakiwa wanamuongoza Diwani wa Nkangamo Weston Simwelu ambaye alipata pigo la kuuawa kwa watoto wawili.
Baadhi ya majirani wa mtaa wa Tazara ambao walifika eneo la tukio kushuhudia mauaji hayo.
Kaka wa marehemu Sista Nyirenge, Mashaka Nyirenge akiwa nje ya chumba cha kuhifadhia maiti kituo cha Afya Tunduma.
Msafara kuelekea kijiji cha Isansa kwa ajili ya mazishi yalyotokana na vifo vilivyotokana na mauaji ya kinyama yaliyofanyika mjini Tunduma mkoani Mbeya.
WATOTO wawili wa Diwani wa Kata ya Nkangamo wilayani Momba mkoani Mbeya Weston Simwelu(55) wameuawa kikatili na watu wasiofahamika kwa kuchinjwa na kunyongwa baada ya kuvamiwa majira ya saa 8:00 mchana Disemba 19 nyumbani kwao eneo la Tazara katika mji mdogo wa Tunduma uliopo mpakani mwa Tanzania na Zambia.
Mauaji hayo ya kutisha yameteka hisia za wakazi wa eneo hilo kwa madai kuwa huenda yanahusishwa na imani za nguvu za giza huku baadhi wakidai kuwa yametokana na mgogoro wa kifamilia.
Taarifa za awali katika eneo la tukio zimedai kuwa Diwani huyo alikuwa akiishi na mke mdogo aliyefahamika kwa jina la Tumaini Yohana(29) ambaye ni mfanyakazi katika halmashauri ya mji mdogo wa Tunduma ambaye wakati wa tukio hilo alikuwa kazini.
Imeelezwa kuwa chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa ni kitendo cha Diwani huyo kuwa mbali na mke mkubwa kwa muda mrefu huku ikidaiwa kuwa mke mkubwa amenyimwa mali za mumewe yakiwemo mashamba na nyumba.
Jeshi la Polisi kupitia Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Barakael Masaki amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja marehemu kuwa ni Kalibu Simwelu(6) ambaye aliuawa kwa kuchinjwa shingoni kwa kutumia kisu na watu wasiofahamika ambapo mtu mwingine aliyeuawa ni mfanyakazi wa ndani aliyetambulika kwa jina la Sista Nyilenda(17).
Kamanda Masaki alisema kuwa Mfanyakazi wa ndani aliuawa kwa kunyongwa  kwa kutumia waya wa televisheni iliyokuwepo sebuleni ambapo wauaji wanadaiwa kuwavamia na kuwaua kinyama ambapo miili ya marehemu ilikutwa sebuleni.
Alisema kuwa wakati wa tukio hilo baba wa watoto hao Bw. Simwelu alikuwa shambani katika kijiji cha Kipaka wilayani humo ilhali mama wa mtoto Tumaini alikuwa kazini kwake ofisi ya Halmashauri ya Mji mdogo wa Tunduma.
Aidha katika tukio hilo Kamanda Masaki alisema kuwa mbali na kufanya mauaji hayo, wauaji waliiba mabegi makubwa mawili yenye nguo mbalimbali ambayo yalikuwa katika chumba wanacholala watoto.
Kamanda Masaki alisema kuwa kufuatia mauaji hayo watuhumiwa watano wametiwa mbaroni ambao ni Gabriel Simwelu(19)Enock Simwelu(23) na Alex Simwelu(16) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari Mpakani ambao wote ni watoto wa mke mkubwa wa Bw. Simwelu.
Wengine waliokamatwa ni pamoja na Mussa Ngoba(19) mkazi wa mtaa wa Mwaka na Patrick Msigwa(18) mkazi wa mtaa wa Majengo na kwamba miili ya marehemu imehifadhiwa katika kituo cha Afya Tunduma.
Picha na habari kwa hisani ya Mkwinda Blog

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII