Mbuge
wa Viti Maalum (CCM), Sarah Msafiri, amekiri kwenda kuonana na
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanzania), kufuatilia
mkataba wa Kampuni ya M/S Sharrifs Services & General Supply
inayohusishwa kufanya biashara yenye utata ya matairi na shirika hilo.
Sarah, alisema alifanya hivyo baada ya kuombwa na mwenye kampuni hiyo, Heri Sharrif, amsaidie kufuatilia mkataba wake Tanesco.
Alidai mbele waandishi wa habari bungeni jana kuwa ameshitushwa na
taarifa za kuhusishwa na kampuni hiyo, na inadaiwa aliisimamia malipo
yenye utata kutoka Tanesco.
Alidai kuwa hana mahusiano yo yote ya kibiashara na kampuni ya Sharrifs
na kwamba siyo mmiliki na wala sio mkurugenzi, na hana hisa wala
hajaajiriwa kwa kazi yo yote na Sharrifs.
Lakini alisema: “ninachojua kuhusu kampuni ya Sharrifs ni kupitia
mkurugenzi wake Heri ambaye mimi kama mbunge alikuja kwangu kunieleza
matatizo yake kwamba aliomba zabuni Tanesco kupitia kampuni yake na
wakashinda, wakapewa barua na Tanesco kujulishwa wameshinda kisha
wakapewa barua ya kwenda kufanya majadiliano pande mbili yaani Tanesco
na Sharrifs.”
Alisema baada ya kukamilisha mchakato huo, walipewa mkataba ambao
kimsingi unabeba makubaliano ya mazungumzo waliokaa pande zote mbili.
“Kama mbunge ambaye nina wajibu wa kushughulikia kero za wananchi
nilienda kwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco na kumweleza madai hayo ya
Sharrifs, nakumbuka alimwita Mkuu wa Idara ya Manunuzi ambaye alikiri
kuifahamu Sharrifs na mkataba wake na mkataba wake alishaushughulikia na
kuupeleka kwa mwanasheria wa shirika,” alisema.
Alisema mwanasheria alipoitwa alikwenda na mkataba huo ukiwa umefungwa
kwenye bahasha ya kaki na hapo ndipo mkurugenzi mkuu alipomhoji kwanini
anakaa na nyaraka ambazo anatakiwa kuziwasilisha sehemu husika.
“Tukiwa wote nilimpigia simu Heri na kumweleza kuwa nipo Tanesco na
mkataba wake uko tayari kwa mwanasheria hivyo aje kuuchukua, lakini Heri
alinijibu yeye yuko mbali ila kama kuna uwezekano nimchukulie ataupitia
nyumbani kwani ni jirani yangu maeneo ninapoishi,” alidai.
Hata hivyo, alidai hakuwa na haja ya kujua walichokubaliana kwenye mkataba kwani kwanza hayamhusu.
Alidai kuwa tuhuma zinazoelekezwa kwake ni mkakati uliowekwa wa
kummaliza kisiasa na kuchafua jina lake, mkakati ambao alisema
umefanikiwa kwa kiasi fulani.
Aliyataka magazeti yaliyoripoti habari hizo bila kumpa nafasi ya
kumsikiliza yamwombe radhi haraka iwezekanavyo na kama yakishindwa basi
atayafikisha mahakamani.
Kuibuka kwa Sarah ambaye alikuwa mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika Anne Makinda kumekuja baada ya
Kikao cha Bunge la Bajeti 2012/13 kuibua tuhuma mbalimbali zikiwemo za
baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati hiyo kutuhumiwa kuomba
rushwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.
Tuhuma zingine kwao ni kuwepo kwa makampuni ya mafuta kuhonga wabunge wasipitishe Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bungeni.
Katika kikao hicho, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu,
alisema kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge na Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma ya mwaka 1995, wabunge hao walipaswa kutaja maslahi yao
kibiashara kwenye shirika hilo.
“Sasa wabunge hawa hawajawahi kufanya hivyo na wameendelea kuwa wajumbe
wa Kamati ya Nishati na Madini na wengine kufanya biashara na Tanesco,”
alisema Lissu na kuwataja kuwa ni Munde Tambwe, Sarah Msafiri, Mariam
Kisangi wa Viti Maalum, Yusuf Nassir (Korogwe Mjini) na Charles Mwijage
Muleba Kaskazini.
Lissu alifafanua kuwa Tambwe na Msafiri wana zabuni ya kuiuzia Tanesco
magurudumu na kwamba hawajawahi kutangaza maslahi yao katika jambo hilo
kwenye kamati zao.
“Mwijage ni mtaalam mwelekezi wa Kampuni ya Puma Energy iliyopewa tenda
na Maswi kuiuzia mafuta Tanesco, hivyo kama mjumbe wa Kamati ya Nishati
ana mgongano wa kimaslahi. Nassir na Kisangi hawa wanafanya biashara ya
mafuta wanamiliki vituo vya mafuta na wana mgongano,” alisema.
Kuhusu Christopher ole Sendeka, Lissu alidai amekuwa akizipigia debe
kampuni tatu zilizonyimwa zabuni ya kuiuzia mafuta Tanesco akiwashawishi
wajumbe wa kamati kuwa serikali ilikiuka kanuni kuipa tenda Kampuni ya
Puma Energy.
Mwingine aliyetajwa ni Vicky Kamata wa Viti Maalum (CCM) ambaye alidaiwa kuwa na mgongano wa kimaslahi na Maswi.
Baada ya kamati hiyo kuvunjwa, Spika Makinda aliunda Kamati Ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuchunguza tuhuma hizo.
Julai 28 mwaka huu, Spika Makinda alivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na
Madini kutokana na baadhi ya wajumbe wake kutuhumiwa kuhongwa na
kampuni za mafuta nchini.
Kamati hiyo iliyovunjwa ilikuwa ikiundwa na wajumbe zaidi ya 20 ambao ni
pamoja na Mwenyekiti wake, Selemani Zedi na Makamu mwenyekiti, Diana
Chilolo, Profesa Kulikoyela Kahigi, Yusufu Haji Khamisi, Mariam Kisangi,
Catherine Magige, Dk. Anthony Mbassa, Abia Nyabakari, Charles Mwijage,
Yusufu Nassir, Christopher Ole Sendeka na Dk. Festus Limbu.
Wengine ni Shafin Sumar, Lucy Mayenga, Josephine Chagulla, Mwanamrisho
Abama, David Silinde, Suleiman Masoud, Kisyeri Werema Chambiri, Munde
Abdallah, Sara Msafiri, Vicky Kamata na Ali Mbaruk Salim.
Kuvunjwa kwa kamati hiyo kulifuatia Mbunge wa Namtumbo (CCM), Vita
Kawawa, kuomba Mwongozo wa Spika, akitaka jambo hilo lijadiliwe na Bunge
na kupendekeza kuwa Kamati za Bunge zinazotuhumiwa kwa rushwa zivunjwe.
Bunge likubali kuivunja na kuiunda upya Kamati ya Nishati na Madini na
kamati na baada ya hoja hiyo kuungwa mkono, Spika Makinda alisimama na
kukubali hoja hiyo ya Kawawa na kutangaza kuivunja Kamati ya Nishati na
Madini.
Spika Makinda alisema ameiagiza Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya
Bunge kutengeneza kanuni za kuwadhibiti wabunge wenye tabia ya kupokea
rushwa kutoka kwa watu mbalimbali ili kutimiza matakwa yao binafsi.
Baadaye Spika aliunda kamati ndogo ya Haki, Maadili na Madaraka ambayo
Mwenyekiti wake ni Ngwilizi. Wajumbe wengine ni John Chiligati
(Manyoni-CCM); Gosbert Blandes (Karagwe-CCM); Riziki Omary (Viti
Maalum-CUF) na Said Arfi (Mpanda Mjini-Chadema).
Kitendo cha Sarah kuzungumza hadharani na kujitetea kimatafsiriwa kuwa
ni kukiuka agizo la Bunge kwamba suala hilo lisijadiliwe na mtu au
chombo chochote.
Wiki iliyopita Naibu Spika, Job Ndugai, alisema ripoti Ngwilizi
itawasilishwa bungeni iwapo Spika ataridhika taarifa hiyo kutolewa ndani
ya Bunge.
Alisema baada ya kukamlika kwa kazi hiyo, baadhi ya wananchi na
wanasiasa wameanza kuizungumzia pamoja na vyombo vya habari kuchambua na
kuchapisha maudhui ya taarifa hiyo kinyume cha sheria na kuingilia
uhuru, haki na madaraka ya Bunge.
Alisema sheria hiyo inamkataza mtu yoyote kuchambua na kuchapisha taarifa ya kamati kabla ya kuwasilisha bungeni.
“Natoa rai kwa umma kuwa tuache Bunge lifanye kazi yake kwa mujibu wa Katiba, Sheria na Kanuni,” alisema Ndugai.
Ngwilizi naye aliwahi kusema kuzuia kujadili suala hilo hadi ripoti itakapowasilishwa bungeni.
Hadi jana wabunge hawakuelezwa chochote kama ripoti hiyo itawasilishwa na kujadiliwa katika mkutano uanoendelea.
Hata hivyo, habari ambazo NIPASHE ilizipata, zinaeleza kuwa msimamo bado uko pale pale kwamba suala hilo litaamuliwa na Spika.
Kumekuwepo na taarifa kuwa huenda ripoti hiyo isijadiliwe bungeni kwa ajili ya kulinda heshima ya serikali.
Habari zinadai kuwa uamuzi huo unatokana na kuwepo kwa makundi mawili
yanayokinzana. Kundi moja linalotaka ijadiliwe linataka ukweli wa tuhuma
hizo ujulikane na haki itendeke kwa waliotuhumiwa.
Kundi linalotaka isijadiliwe ni lile linaloiunga mkono serikali ambalo
linaona kuwa kujadiliwa kwake kunaweza kuwatia hatiani viongozi
waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini, Waziri Prof. Sospeter
Muhongo na Katibu Mkuu, Eliakim Maswi.
Vigogo hao wanadaiwa kuipatia Puma zabuni ya kuiizia serikali mafuta
mazito ya muendesha mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura kwa upendeleo
na kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma.
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII