Pages

Thursday, March 14, 2013

DR SLAA AFUNGUKA KUHUSU SUALA LA VIDEO YA KUPANGA MAUAJI, NA HII NDIO KAULI ALIYOITOA....BOFYA HAPA

 
KATIBU  Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa amezungumzia video aliyorekodiwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama hicho, Wilfred Lwakatare na kusema ni ya kutungwa na vyombo vya dola. 

Dk. Slaa pia amelituhumu Jeshi la Polisi kufanya mchezo mchafu kwa maslahi ya kisiasa.
Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari Makao makuu ya chama hicho kufafanua suala la kushikiliwa kwa Lwakatare. 


Dk. Slaa, alilalamikia jeshi la polisi kuwa limekuwa likitumika kisiasa huku akitoa mfano wa chama hicho kuwa kimekuwa kikitaarifu jeshi la polisi kuhusu mambo hayo lakini halijawahi kuchukua hatua. 

Alisema  jeshi la polisi halijawahi kuchukua hatua stahiki kwa suala la mauaji ya Daudi Mwangosi kumwajibisha Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Iringa aliyesimamia na kufanikisha kifo cha mwandishi huyo wa habari, jeshi la polisi pia halikuchukua hatua za kumhoji Dk. Stephe Ulimboka baada ya kuteswa na mtu anayedaiwa kuwa ni Afisa wa usalama wa Taifa wa Ikulu, hali kadhalika hawezi kushangaa ikiwa jeshi la polisi halitaacha kumhoji Absalom Kibanda. 

Amesema, jeshi la polisi limekuwa likitoa taarifa za kukichafua chama, akikumbushia suala la Mwangosi, alisema kuwa mara tu baada ya tukio la Mwangosi kuuawa, jeshi la Polisi kupitia kwa Kamishna wake lilitoa taarifa kuwa alilipuliwa na kitu kilichorushwa kwake akikimbilia kujisalimisha kwa polisi akitoka kwa wafuasi wa Chadema, jambo ambalo lilikuwa sio kweli. 

Hivyo alisema, Mkurugenzi  wa ulinzi na usalama wa Chama hicho kuhusishwa kwa sakata la sasa la mkanda wa video uliopo katika mtandao na Kibanda ni mwendelezo tu wa kukihujumu chama, unaoratibiwa na Usalama wa Taifa, huku ukitekelezwa na jeshi la polisi. 

“CHADEMA kinafahamu kwa undani, kwamba uzushi huu wa Tape ya “Bukoba Boy”.Tunajua huu umeanzishwa na kuhusisha Usalama wa Taifa, akiwemo Ighondo na wenziwe pale Ada Estate. Huyu  Ighondo ambaye anafahamika pia kwa jina la “Rama” tunamfahamu vizuri sana," alisema.



Dk Slaa aliingiza suala la kufungiwa suala la kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi akiituhumu serikali kutokua makini. 

Akakumbushia kuwa waliwahi kutuma barua mbalimbali polisi zinazothibitisha kuwa wanafanyiwa michezo michafu huku zikiwa zimeandikwa majina ya viongozi wa CHADEMA, au taarifa za Vikao vya Chadema zilizopotoshwa lakini polisi hawakuchukua hatua. 

Aliongeza kuwa wakati wa uchaguzi wa Igunga walisema kuwa kuna mtu anamiliki bastola isisvyo halali, wakataja hadi namba za bastola iliyoingizwa lakini polisi hawajawahi kushughulika nayo. 

Hata hivyo alishangazwa na jeshi la polisi kufanya haraka kumshikilia Lwakatare, kwani vyombo vya habari hivi majuzi vimemtaja kwa majina ya watu kuhusishwa na utekwaji na uteswaji wa Kibanda, lakini jeshi halikusema lolote hadi sasa. 

Akaongeza kuwapo watu aliowataja kwa majina kwamba waliingia kwa ID zao kwenye mitandao kukejeli suala la kuteswa Absalom Kibanda lakini jeshi halikuchukua hatua.
Alishangazwa jinsi polisi walivyofanya haraka kumkamata Lwakatare, akasema ni mbinu tu za kukichafua CHADEMA. 

Hadi tunaenda Mitamboni, Jeshi la polisi lilikuwa halijatoa taarifa kuwa Mkurugenzi huyo wa Ulinzi na usalama wa Chadema angepata dhamana au la, lakini Wakili wake alilithibitishia gazeti hili kuwa wameenda tena kumpekua kwa mara nyingine nyumbani kwake. 

Kutokana na hali hiyo, Dk Slaa alisisitiza kuwa “madai yaliyotolewa mara nyingi na CHADEMA, kwa Rais kuandikiwa barua na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, iundwe Judicial Commission of Inquiry (Tume Huru ya Kimahakama kuchunguza vifo vyote vyenye utata na sura ya kisiasa).
Akahoji ,Serikali inaogopa nini kuunda Tume hii huru ili ukweli Ujulikane? Iweje CHADEMA inayotuhumiwa Kupanga njama wanaishinikiza Serikali kuunda Chombo huru na Serikali ndiyo inayopata kigugumizi?”
Aliongeza kuwa “kwa wale walioumizwa na kujeruhiwa kama kina Ulimboka Kibanda na wengine, tunarudia Tamko letu la kuwa hatuna Imani na uchunguzi unaofanywa na Jeshi la Polisi kwa kuwa viongozi wa Jeshi hilo ni sehemu ya watu tunaowatuhumu kwa kuhusika kwa njia mbalimbali, na Ushihidi wa wazi na Taarifa mbili za Serikali kupingana yaani Taarifa ya Kamati yqa Nchimbi na Tume ya Haki za Binadamu.
"Tutaiaminije Polisi na Serikali kwa Taarifa ya Kamati ya Nchimbi? Hatuwezi kuendelea kuvumilia ukandamizaji huu wa uhuru wa habari, ambao sasa unaelekea kuota mizizi nchini kwetu. Na kweli ninawaomba na kuwataka waandishi wote msimame imara, bila kujadili itikadi, au tofauti zetu zozote zile na kusimamia uhuru wa Habari. Tunataka vivyo hivyo, kwa wanaharakati mbalimbali. Waache hofu, eti wanaogopa kuhusishwa na vyama vya Siasa! Haki ni haki na haina rangi ya bendera ya chama chochote," alisema.
 
Azungumzia Bunge:
Dk Slaa amesema kuwa usalama wa Taifa, unafanya kazi kwa maslahi ya Chama cha Mapinduzi hadi ndani ya bunge, ndio maana sasa wabunge wa Chama hicho wameondolewa katika kamati muhimu ambazo walikuwa wanazisimamia, bila wao kuulizwa, tofauti na walivyojaza katika fomu na nje ya ushauri wa Kiongozi wa upinzani bungeni. 


Dk slaa alisema hiyo yote ni hujuma, Mnyika amepelekwa Ardhi maliasili na Mazingira, huku Msigwa akiondolewa maliasili na utalii kwa kuwa alikuwa anawataja viongozi wa CCM , jeshi la Polisi, jeshi la Wana nchina Ikulu yenyewe kuhusishwa na ujangili wa wanyama. 

Amesikitishwa na wabunge wa Chama chake kuhamishwa kamati muhimu walizokuwa wanazisimamia, huku wengine wakiachwa kuingizwa katika kamati jambo ambalo linawanyima ufuatiliaji wa utendaji wa serikali, ilihali wabunge wengi wa CCM wengine wamewekwa kamati mbili kwa mbunge yule yule.

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII