Pages

Friday, March 15, 2013

HIKI NDICHO ALICHOKISEMA BENARD MEMBE BAADA YA KUHUSISHWA NA KUMJERUHI ABSALOM KIBANDA

 
Katika gazeti la Mtanzania toleo namba 7255 la tarehe 13 Machi, 2013 ilitolewa taarifa yenye kichwa cha habari “SAKATA LA KUTESWA KWA KIBANDA: Membe atajwa” na kwamba eti mimi ninahusika na vitendo vya kikatili na unyama alivyofanyiwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa kampuni ya New Habari, Bw. Absalom Kibanda.

Nimeshangazwa na kusikitishwa sana na habari hizo na ningependa kuwahakikishia Watanzania wenzangu kwamba sijahusika, sihusiki na sina sababu ya kuhusika kwa namna yoyote ile. Sina nia, genge wala fedha za kufanya shughuli kama hiyo. Katika maisha yangu yote, sijawahi kugombana naye na hajawahi kunifanyia ubaya wowote. Kwa kifupi, sina uhasama na Bw. Absalom KIbanda.

Taarifa iliyotolewa na Mtanzania ni taarifa ya uongo, ni habari za kuunga-unga maneno na habari za kughshi. kwa vyovyote vile, mwandishi wa habari hii na wenzake wana malengo ya kisiasa anayoyajua yeye na wenzake wanaomtumia. Huu ni mwendelezo wa mkakati wa kisiasa wa kunichafua ambao umekuwa ukiendelezwa na wale wasionitakia mwema. Wanajaribu kuwaondoa Watanzania katika kiu yao ya kutaka kufahamu ukweli wa jambo hili.

Nawashukuru sana wananchi wenzangu, jamaa na marafiki walioniletea salamu za kunitia moyo. Naungana nao katika kujiuliza, hivi kiburi hiki, dhihaha hii na ujsriri huu wa kusema uongo hadharani wanautoa wapi!? Jeuri na kiburi cha nmana hii hakiwezi kutokana na sheria za nchi, haki ya kikatiba wala hofu ya Mwenyezi Mungu. Naomba Watanzania wenzangu mnisaidie kutegua kitendawili hiki. Naamini kwa dhati kwamba ukweli kuhusu suala hili utajulikana na yeyote mwenye ushahidi wa kweli aonyeshe uzalendo wake kwa kutoa taarifa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama.

Mwisho, wakati nashauriana na wanasheria wangu kuona hatua ya kuchukua dhidi ya kuchafuliwa huku, nawaomba Watanzania wenzangu tuvute subira na tuache vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi zake ili Watanzania hatimaye wajue ukweli wa kilichotokea.

No comments:

Post a Comment

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII