KUTOKA CHADEMA:TAARIFA KWA UMMA – KUUNGA MKONO MAANDAMANO YA TAREHE 25 MACHI 2013

 
 Amani Golugwa Katibu wa Chadema – Kanda ya Kaskazini
 
Kufuatia tamko lililotolewa jana tarehe 11 Machi 2013 huko musoma na Mwenyekiti wa chama Mhe Freeman A. MBowe (MB), ambalo ni msisitizo wa tamko lililotolewa wiki kadhaa zilizopita huko mbeya la azimio la kutaka waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi na naibu wake kuwajibika kufuatia matokeo mabaya ya mitihani ya kidato cha NNE, CHADEMA kanda ya Kaskazini inaunga kwa mkono tamko hilo ambalo limebeba utashi wa wananchi ambao ni wazazi wa vijana wetu ambao kwa sababu ya mfumo mbovu wa elimu, umeendelea kupelekea matokeo kuwa mabaya na hasa ya mwaka na yenye kuleta fedheha na kilio kikubwa sana kwa taifa letu. 
 
Ieleweke kuwa hili ni janga na serikali kwa ukiziwi wake wa kutosikiliza sauti za watu itajikuta ikiingia kwenye gharama kubwa ya kukabiliana na kundi kubwa la vijana waliopo mtaani ambao hawana jambo la kufanya kwa sababu mfumo wa elimu umewafanya kuwa washindwaji kwa kiwango ambacho hawataweza kujimudu kimaisha.
 
Hili si jambo dogo hata kidogo, tafsiri ya matokeo mabaya haya inawalenga moja kwa moja mawaziri wenye dhamana na pasifanyike masihara wala mizaha kuhusu jambo hili la kufeli huku kwa vijana wetu. Kauli zao za awali zimeonyesha wao kutojali na kulitia umaanani kwa kutoa vijisababu visivyo na mashiko wakati wao ndio wenye dhamana. Ni dhahiri kuwa takwimu za elimu zimeshuka kutoka aslimia 89.3 ya mwaka 2005 hadi kufika asilimia 34.5 kwa mahesabu haya kiwango cha elimu kimeporomoka kwa asilimia 54.8 (Chanzo: Hotuba ya Waziri Mkuu akizungumza na waandishi wa habari tarehe 2 Machi 2013). 
 
Takwimu hii inazungumza mambo mengi, maana yake ni kuwa mfumo mbovu unaosimamiwa na Chama Chama Mapinduzi kwa asilimia hii 54.8 ya vijana wetu watakuwa wamewezeshwa tu kujua kusoma kwa mashaka, kuandika na kuhesabu kwa shida kitu ambacho hakitawasaidia kupambana na changamoto za kimaisha iwapo hawataweza kupata fursa za kujiendeleza kwa ziada. Hili ni janga kubwa na wahusika ni lazima wawajibike maana ni dhahiri kwa mfufulizo wa kuporomoka huku ni dhahiri wameshindwa kusimamia elimu ya Tanzania.
 
CHADEMA kanda ya kaskazini, tunawaalika wazazi wote na vijana wetu wote ambao wamekuwa wahanga wa matikeo haya mabovu siku ya tarehe 25 Machi 2013 kushiriki katika maandamano haya ya kushinikiza kuwajibika kwa waziri elimu na mafunzo ya ufundi stadi na naibu wake. Zaida ya hapo ni kuitaka pia serikali kufanya utaratibu wa kuwajibika kuwasaidia vijana hawa katika kushughulikia janga hili. Aidha katika kuanzisha vituo vya masomo kuwawezesha kusoma ili kurudia mitihani au lolote litakaloonekana lenye msaada. Maamuzi mabaya ya hamaki na yasiyo ya kujali katika jambo hili yataweza kuzaa kizazi kibovu ambacho kitakuwa ni mavuno ya matunda ya maamuzi yetu yasiyoonyesha utashi wa kujali ya sasa.
 
Nawaomba wazazi wote katoka mikoa ya Tanga, Kilmanjaro, Arusha na Manyara wafike katika ofisi za chama za wilaya zilizopo katika mikoa yao au ofisi za wabunge (CHADEMA) kuandikisha majina yao na ya watoto wao ili kupata idadi kamili. Siku ya tarehe 25 Machi kuanzia SAA NNE asubuhi kuanzia mahali ambao tutawajulisha kutakuwa na maandamano makubwa katika JIJI la Arusha yatakayokuwa na ujumbe huu na yatawashirikisha viongozi wote wa chama, wabunge wote kutoka mikoa ya kanda ya kaskazini, wadau wa elimu, taasisi zisizo za kiserikali zenye kujishughulisha na masuala ya elimu pamoja na watanzania wote ambao kwa dhati ya moyo wameguswa na matokeo haya mabaya ya elimu, wazazi na vijana wote waliopatwa na janga hili.
 
Taarifa nyingine zitawajia kama ambavyo tutawajulisha kupitia vyombo vya habari na ofisi za wabunge na makatibu wa majimbo.
 
Niwaombe Watanzania wote wakazi wa kanda ya Kaskazini tujitokeze kwa wingi katika maandamano haya ya AMANI yatakayofanyaika katika JIJI la Arusha na tuonyeshe Utanzania wetu na tuonyeshe kuwajali watoto wetu.
 
SIKU YA MAANDAMANO NJOO NA KITAMBAA CHEUPE MKONONI.
 
 
Imetolewa leo tarehe 12 Machi 2013.
Ofisi ya Kanda ya Kaskazini
 
Amani Golugwa
Katibu – Kanda ya Kaskazini
+255 754 912 914
golugwa@gmail.com
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs