Pichani ni washiriki walioiwakilisha
Tanzania ndani ya Jumba la Big Brother Africa tangu shindano hilo
lilipoanza mwaka 2003 hadi leo. Nani atachukua hiyo sehemu yenye alama
ya kuuliza?
Ungefika katika Hotel ya Alantis (zamani OysterBay Hotel) wiki
iliyopita, bila shaka ungeshikwa na butwaa kuona utitiri wa vijana, wa
kike na kiume waliojitokeza katika audition ya kumtafuta mwakilishi wa
Tanzania katika shindano la Big Brother Africa 8. Bila kuuliza pengine
ungedhani kuna mtu kasimama anagawa hela kwa vijana. Hapana.
Kila aliyekuwepo pale alikuwa anajaribu kutimiza kitu kimoja; kuingia
ndani ya jumba la Big Brother Africa tarehe 26 Mei, 2013 (siku ambayo
shindano la mwaka huu linatarajiwa kuanza) akiwa mwakilishi wa Tanzania.
Isitoshe, dau limeongezeka. Mshindi wa mwaka huu atatoka pale akiwa na
$300,000 (Approximately: Tshs Milioni 486). Kulikuwa na kila sababu kwa
vijana wengi namna ile kujitokeza kwa nia ya kuwashawishi majaji
waliokuwa wanafanya zoezi gumu la “uchaguzi” kwamba yeye ndio anafaa
kuelekea “bondeni” kwa ajili hiyo.
Tangu kampuni ya MultiChoice Tanzania ilipotangaza kwamba ule wakati
wa show maarufu ya Big Brother Africa umewadia, gumzo mtaani lilianza.
Radioni, kwenye migahawa na hata vijiwe vya watu wazima, gumzo likawa ni
Big Brother Africa. Watu kadhaa wenye majina makubwa kama vile
mwanadada Wema Sepetu na mwimbaji/ mwanamuziki TID sio tu walitajwa bali
kukawa na kampeni kutoka kwa mashabiki wao kuwasihi wachukue fomu. Sina
uhakika kama Wema na TID waliitikia wito. Nasubiri kwa hamu kuona au
kusikia.
Yote tisa, Kumi limebaki swali; Nani ataiwakilisha Tanzania katika Big Brother Africa 8?
Swali la nani ataiwakilisha Tanzania, linavuka mipaka mpaka kwenye
nchi zote ambazo zimewahi kutuma wawakilishi katika Big Brother Africa.
Tanzania ni tishio. Ina rekodi ya kuwa imeshatoa mshindi. Richard Dyle Bezuidenhout
aliibuka mshindi katika shindano la Big Brother 2. Kabla ya hapo,
Mwisho Mwampamba alitoka akiwa wa 2 siku ya mwisho na hivyo kushindwa
kidogo tu na Cherise Makubale kutoka Zambia ambaye ndiye aliibuka
mshindi kwa Big Brother Africa 1. Bila shaka unakumbuka jinsi watanzania
walivyoimba Fagilia Bongo (enzi za Mr.Nice) wakati wa mapokezi ya
Mwisho Mwampamba aliporejea nchini.
Mwisho Mwampamba mpaka leo ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwa amekaa
kwa siku nyingi zaidi ndani ya jumba la Big Brother Africa kwa kufikisha
jumla ya siku 197 ambazo mpaka leo hazijafikiwa na yeyote. Mwisho
alishiriki shindano la kwanza (Big Brother Africa 1) na baadae akaenda
tena wakati wa Big Brother Africa 5 (All Stars).
Mwaka huu shindano litakuwa linafanyika kwa mara ya 8 tangu shindano
la kwanza liliporushwa hewani kuanzia tarehe 25 Mei, 2003 mpaka tarehe 7
September 2003.
STAY TUNED FOR BIG BROTHER AFRICA 8.
Credits : Bongocelebrity.com
No comments:
Post a Comment
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII