CCM YAJIPANGA KUFANYA ZIARA KWENYE MIKOA MNNE LENGO LIKIWA NI KUPAMBNANA NA CHADEMA ...!
VIGOGO WAPYA, MAWAZIRI KUANZA ZIARA MIKOANI
KATIKA
mikakati yake ya kupambana na nguvu za operesheni za CHADEMA mikoani,
Chama cha Mapinduzi (CCM), kimelazimika kuwatumia viongozi wake wapya
wakiongozana na mawaziri ili kwenda mikoani kufafanua kwa wananchi jinsi
serikali ilivyotekeleza ilani yake.
Hii
itakuwa ni mara ya pili kwa chama hicho kujaribu kukabiliana na
upinzani wa CHADEMA mikoani, ambapo mwaka jana baada ya mkutano wao wa
maazimio ya kujivua gamba, walijitahidi kuzunguka baadhi ya mikoa bila
kufua dafu.
Operesheni
zinazofanywa na CHADEMA za Sangara na sasa Vuguguvu la Mabadiliko
(M4C), zimeitikisa CCM na hivyo wajumbe wake kutumia muda mwingi kwenye
mkutano mkuu wao uliomalizika mjini Dodoma, kujitapa kuwa lazima wafanye
mashambulizi ya kuwasambaratisha.
Akitangaza
mkakati huo mpya jana kwa waandishi wa habari wa kuchanja mbunga kwa
kutumia anga kwa helikopta kama CHADEMA, Katibu wa Halmashauri Kuu ya
Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema wameanda ziara ya
siku nne katika mikoa minne.
Alisema ziara hiyo itaongozwa na sekretarieti mpya chini ya Katibu wake
Mkuu, Abdullahman Kinana, na kuwashirikisha baadhi ya mawaziri.
Nape alisema kuwa ziara hiyo ni ya chama na sio ya kiserikali na kwamba
itaanza kesho hadi Novemba 24 katika mikoa ya Mtwara, Arusha, Geita na
Rukwa.
Akifafanua zaidi alisema Kinana ataanzia Mtwara ambako atakuwa na
mawaziri husika wanaoshughulikia masuala ya kilimo ili kuzungumzia zao
la korosho na waziri wa uchukuzi atakayezungumzia bandari na
miundombinu.
Nape aliongeza kuwa wakiwa Sumbawanga watazungumzia miundombinu na kwa
Geita watafuatilia migogoro ya migodi na kumalizia Arusha kwa kuangalia
harakati za kufufua viwanda kwani vinaathiri ajira.
Nape
alisema kuwa lengo la kuongozana na baadhi ya mawaziri ni kutoa maelezo
ya papo hapo hasa kwa mambo yanayosuasua ikiwemo kuwawajibisha bila
kusubiri Bunge kufanya hivyo.
“Lengo
tunasukuma spidi ya utekelezaji wa maendeleo na ilani ya uchaguzi na
tunajikita kwa baadhi ya mambo na kuendeleza mageuzi ndani ya chama na
ndio azimio tuliloondoka nalo katika mkutano mkuu wa nane,” alisema.
Akizungumzia
kung’atuka kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama,
Nape alisema kiongozi huyo ameondoka ili akasimamie uanzishwaji wa chuo
cha uongozi cha CCM, ambacho kitasaidia makada kuwa na nidhamu na
uwajibikaji.
Akijibu hoja za CHADEMA zinazodai CCM imetekeleza ilani ya chama hicho
hususan katika suala la elimu na kupunguzwa kwa bei za vifaa vya ujenzi,
Nape alisema kuwa suala la elimu bure ni la CCM.
“Suala hilo lilianza wakati wa TANU chini ya Mwalimu Julius Nyerere na
hata hao kina Dk. Slaa wamesomeshwa bure na TANU,” alisema.
CHADEMA wajiimarisha
Wakati CCM ikianza ziara mikoani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA), kimeanza kujiimarisha kwa kuendesha mafunzo ya darasani na
vitendo, kwa lengo la kuwajengea uwezo wenyeviti na makatibu wa mikoa 32
ya kichama.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi
wa Mafunzo na Oganaizesheni wa CHADEMA, Benson Kigaila, alisema kuwa
mafunzo hayo yatafanyika Novemba 22 hadi 23, mwaka huu, wilayani
Karagwe, mkoa wa Kagera.
Kigaila alisema baada ya mafunzo hayo wataingia kwenye vitendo ambapo
makatibu na wenyeviti hao watasambaa kushambulia vitongoji na vijiji
vyote vya wilaya ya Karagwe, kwa kufanya mikutano ya hadhara katika
maeneo hayo.
Alibainisha kuwa mafunzo hayo ya vitendo ni sehemu ya utekelezaji wa
mikakati mbalimbali ya ujenzi na uimarishaji wa chama, hususan
operesheni ya M4C ambayo imesaidia viongozi kuzungumza na wananchi
kupitia mikutano ya ndani na hadhara.
Kuhusu M4C, Kagaila alisema wakati viongozi hao waliopata mafunzo
wakiendelea, chama kitatoa ratiba ya operesheni hiyo kubwa
itakayoendelea kufanyika kwa nchi nzima.
Habari hii imeandaliwa na Happiness Mnale na Shehe Semtawa
Chanzo: Chadema.blog
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII