Mh.zitto Kabwe
Our Ref: ZZK/12/13 10.12. 2013.Mh. Katibu MKuu, Chama Cha Demokrasia Na Mendeleo HSE NO 170,
UFIPA STREET, KINONDONI S. L. P 31191 Dar es Salaam – Tanzania.
YAH: MASHATAKA YA UKIUKWAJI WA KATIBA, KANUNI NA MWONGOZO WA CHAMA.
Rejea
barua yako ya tarehe 26 Novemba 2013 yenye kumbukumbu no
C/HQ/ADM/KK/08/31 Iliyoelezea maamuzi yaliyofikiwa na kikao cha Kamati
Kuu ya Chama cha tarehe 20-22 Novemba 2013, kiliazimia kwamba niachishwe
nafasi zote za uongozi ninazoshikilia katika chama na kwamba Kamati Kuu
iliazimia kwamba hatua zaidi za kinidhamu za kuachishwa ama kufukuzwa
uanachama zichukuliwe dhidi yangu kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji za 6.5.2(d), ningependa kuwasilisha majibu ya mashtaka hayo kama ifuatavyo;
1.0 MAELEZO YA AWALI;Napenda
kuwasilisha utetezi wangu huku nikiwa napinga utaratibu uliotumika
kuandaa na kunifikishia mashtaka husika (Defence Under Protest) kwa
sababu zifuatazo;
1.1.
Hatua za kinidhamu ambazo kimsingi ni adhabu zimeshachukuliwa na Kamati
Kuu kwa mashtaka haya haya ambayo nimepatiwa. Kama barua yako
inavyosema na nanukuu maneno yako “Kamati Kuu kwa kutumia mamlaka
yake kwa mujibu wa Kanuni ya 6.5.2(d) ya Kanuni za Uendeshaji Shughuli
za Chama (‘Kanuni za Uendeshaji’), iliazimia kwamba muachishwe nafasi zote za uongozi mnazoshikilia katika Chama…” (msisitizo ni wangu).Mheshimiwa Katibu Mkuu;Ni
wazi kabisa kwamba adhabu ya kuachishwa nafasi zote za uongozi
imeshatekelezwa. Kamati Kuu imeshanitia hatiani kwa makosa haya haya
ambayo sasa hivi natakiwa nijitetee. Binafsi siamini kwamba kwa
utaratibu huu haki itatendeka na inaonekana kutendeka. Ni vigumu sana
kusema kwamba haki yangu ya msingi ya kusikilizwa na kujitetea imelindwa
wakati tayari adhabu imeshatolewa na chombo kile kile ninachotakiwa
kujitetea mbele yake.
1.2. Kama kiongozi ambaye nimeadhibiwa na Kamati Kuu ninayo haki ya kukata rufaa Baraza Kuu dhidi ya haya yafuatayo; 1.2.1. utaratibu uliotumika na Kamati Kuu kunivua nyadhifa zote za uongozi. 1.2.2. sababu zilizotumika kunivua nyadhifa zote za uongozi.
Mheshimiwa Katibu Mkuu;
Katiba ya Chama pamoja na Kanuni za Uendeshaji zinatoa HAKI hii ya msingi na UTARATIBU kwa maneno haya;
Ibara 6.3.6(d) ya Katiba ya Chama;“Kiongozi aliyechukuliwa hatua za kinidhamu na mamlaka yake ya nidhamu anayo haki ya kukata rufaa ngazi ya juu ya ile mamlaka yake ya nidhamu na uamuzi wa ngazi hiyo utakuwa wa mwisho”.
Ibara 6.3.6(e) ya Katiba ya Chama;“Rufaa yoyote lazima ifanyike katika muda wasiku thelathini tangu tarehe ya kupokea rasmi kwa maandishi maamuzi ya mamlaka iliyotoa adhabu”.Mheshimiwa Katibu Mkuu;Kanuni
za Uendeshaji zinatoa UTARATIBU ambao unatakiwa ufuatwe ili kiongozi
aliyeadhibiwa aweze kutumia HAKI yake ya kukata rufani kwa maneno haya;Kanuni ya 6.5.8 ya Kanuni za Uendeshaji;“Kiongozi aliyeadhibiwa atapewa taarifa ya msingi wa maamuzi ya mamlaka ya nidhamu ili kumuwezesha kuamua kukata rufani au la”
Kanuni ya 6.5.9 ya Kanuni za Uendeshaji;“Mwadhibiwa atakayeamua kukata rufani atatakiwa kufanya hivyo katika muda wa siku thelathini baada ya kuarifiwa uamuzi wa adhabu”Kanuni ya 6.5.10 ya Kanuni za Uendeshaji;“Baada ya kutoa uamuzi kikao husika kinalazimika kuandaa taarifa kamili ya mwenendo wa shauri na kuwasilisha ngazi ya juu. Taarifa hiyo lazima ifike katika muda wa siku kumi na nne baada ya kikao cha mamuzi” Mheshimiwa Katibu Mkuu; Mpaka
tarehe 01/12/2013 siku ambayo nimepokea barua yako ya mashtaka dhidi
yangu sijapokea taarifa ya msingi wa maamuzi ya mamlaka ya nidhamu na
pia taarifa kamili ya mwenendo wa shauri langu haujawasilishwa Baraza
Kuu. Wakati hayo yote hayajafanyika natakiwa kutoa utetezi wangu wa
maandishi kwa mujibu wa Kanuni ya 6.5.2(a) ikisomwa pamoja na Kanuni ya
6.5.6 ya Kanuni za Uendeshaji kwa makosa yaleyale ambayo tayari
nimeshaadhibiwa na Kamati Kuu. Ni wazi kabisa kwamba barua yako ya
mashtaka ni muendelezo wa hatua au maazimio ya Kamati Kuu kama
ilivyoandikwa “Aidha Kamati Kuu iliazimia kwamba hatua zaidi za kinidhamu za kuachishwa ama kufukuzwa uanachama zichukuliwe….”
Mheshimiwa Katibu Mkuu;
Utaratibu
uliotumika na Kamati Kuu sio wa HAKI na ni ukiukaji wa Katiba na Kanuni
za Uendeshaji. Nalazimika kutoa utetezi wangu nikiwa napinga (under
protest) kwa sababu kwa Chama ambacho kinasifika kwa kupigania misingi
ya utawala bora na utawala wa sheria ni lazima kiheshimu haki za
wanachama na viongozi wake pamoja na kufuata utaratibu kilichojiwekea
wakati wa kuchukua hatua za kinidhamu.1.3. Baadhi ya wajumbe wa Kamati
Kuu kwa nyakati mbalimbali wametoa matamko kwamba tumefukuzwa uongozi na
hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yetu kabla hata ya ofisi yako kutoa
Mashtaka dhidi yetu. Mheshimiwa Tundu Lissu na Mheshimiwa John Mnyika walitoa matamko hayo wakati wakiongea na Waandishi wa Habari. Mheshimiwa Katibu Mkuu;
Kitendo
cha wajumbe hao kutoa misimamo kwa niaba ya Chama au Kamati Kuu ni
ukiukwaji wa haki yangu ya msingi ya kusikilizwa. Ni wazi kabisa kwamba
tayari hukumu dhidi yangu imeshapitishwa kabla sijasikilizwa. Sina imani
na wajumbe ambao tayari wameonyesha waziwazi misimamo yao kuhusu tuhuma
dhidi yangu. Mheshimiwa Katibu Mkuu;
Kutokana
na hayo yote ambayo nimeyataja hapo juu naomba ofisi yako isitishe
utekelazaji wa maamuzi au maazimio ya Kamati Kuu mpaka pale ambapo
nitakuwa nimepatiwa taarifa ya msingi wa maamuzi ya Kamati Kuu na kuweza
kukata rufaa ngazi ya juu kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Uendeshaji.
Hatua zozote za Kamati Kuu zitaendelea kukiuka Katiba na Kanuni za
Uendeshaji.
Bila kuathiri hayo niliyoyasema;
1 UTETEZI WANGU DHIDI YA MASHTAKAMheshimiwa Katibu Mkuu;Kwa
ujumla nakanusha na kukataa kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwangu kuhusu
kinachoelezwa kwamba niliandaa mkakati wa mabadiliko 2013, mimi binafsi
sijawahi kushiriki, kuhusika kuandaa au kufahamu kwa namna yoyote ile
kinachoitwa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 kama ulivyoainisha
kwenye barua yako. KOSA LA KWANZA
Kukashifu Chama kiongozi au mwanachama yeyote wa chama kinyume na masharti ya 10.1(xii) ya Kanuni za Uendeshaji. Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa waraka ulioitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013. 2.
Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au
nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kumkashifu Mwenyekiti wa Chama
Taifa kwa njia yoyote ile.
3.
Kuhusu kutoa kashfa kwa Katibu Katibu Mkuu wa Chama na Mbunge wa Arusha
Mjini Mh. Godbles Lema kama ulivyoainisha kwenye barua yako mimi
binafsi sijawahi kutoa kashfa hizo na wala kuhusika kwa namna yoyote ile
kwenye maandalizi ya mkakati huo wa mabadiliko.
Kutokuwa wakweli na wawazi wakati
wote na kushirikiana na vikundi vya majungu na wadanganyifu (rumour
mongers) Kinyume na Kanuni ya Uendeshaji 10.1 (vii) ya Kanuni za
Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana nilianzisha mtandao
wa siri ulioitwa “Mtandao wa Ushindi’ ili kuniwezesha mimi kutwaa
madaraka ya Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa njia zilizo kinyume na Katiba,
Kanuni za Uendeshaji na Kanuni za Kusimamia Shughuli, Mwenendo na
Maadili ya Wabunge wa CHADEMA na Mwongozo wa Kutangaza Kusudio la
Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na Serikali 2012. 2. Nakanusha kuanzisha, kushiriki uanzishwaji au kuufahamu unaoitwa mtandao wa ushindi kama ilivyoelezwa na barua yako. 3.
Siku zote nimekuwa mkweli muwazi kwa yale ninayoyaamini na katika
kutekeleza majukumu yangu kama kiongozi na mwanachama mtiifu wa CHADEMA.
Pia sijashirikiana na kikundi chochote cha majungu au wadanganyifu kama
iliyoainishwa kwenye barua yako.
Kutoa tuhuma juu ya viongozi
wenzenu pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na ngazi
zilizowekwa kwenye Kanuni kinyume na Kanuni ya 10.1(x) ya Kanuni za
Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana nilitoa tuhuma nzito
na za uongo dhidi ya viongozi wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama
Taifa na Katibu Mkuu pasipo kupitia vikao halali na bila kuzingatia
taratibu na ngazi zilizowekwa na Kanuni za Uendeshaji. 2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kwamba nilitoa tuhuma nzito
na za uongo dhidi ya viongozi wakuu wa Chama, yaani Mwenyekiti wa Chama
Taifa n Katibu Mkuu pasipo kupitia vikao halali na bila kuzingatia
taratibu na ngazi zilizowekwa na Kanuni za Uendeshaji.
Kujihusisha na vikundi vyenye
misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambavyo vina makusudi ya kubaguana
ndani ya chama na miongoni mwa jamii kisiasa au kijamii na Kanuni ya
10.1(iv) ya Kanuni za Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1.
Nakanusha kwamba nimejihusisha katika kuanzisha, kushiriki uanzishwaji
au kufahamu kikundi chochote chenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda
ambacho kina makusudi ya kubaguana ndani ya chama na miongoni mwa jamii
kisiasa au kijamii kwa kutumia waraka unaosemekana kuandaliwa nami.
2. Mimi binafsi sio mdini, mkabila au mkanda na sijawahi kujihusisha na kikundi au mtu yeyote mwenye tabia hizo.
Kujihusisha na vikundi na vitendo
vya kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au
wanachama wake na kinyume na Kanuni ya 10.1 (x) ya Kanuni za Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1.
Nakanusha kwamba nimejihusisha na vikundi na vitendo vya kuchonganisha
au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake.
2. Mimi binafsi sikifahamu kikundi chochote ambacho nashutumiwa kujihusisha nacho.
Kutekeleza mpango wa kusudio la
kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Chama Taifa bila kutangaza kusudio la
kugombea nafasi hiyo kinyume na kifungu cha 2(g) cha Mwongozo wa
Kutangaza Kusudio la Kuwania Nafasi za Uongozi Kwenye Chama, Mabaraza na
Serikali 2012.Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1.
Nakanusha kwamba nimetekeleza au kuhusika katika utekelezaji wa mpango
wa kusudio la kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa Chama Taifa bila
kutangaza kusudio la kugombea nafasi hiyo.
2.
Sijatangaza sehemu yeyote kwamba nitagombea nafasi hiyo na pia vile
vile sijatekeleza mpango wowote kama ilivyoelezwa kwenye barua yako.
Kutengeneza makundi au mitandao ya
kuwania uongozi ndani ya chama kwa nia ya kujihakikisha ushindi kinyume
nakifungu cha 2(d) cha mwongozo wa kuwania uongozi.Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1.
Nakanusha kwamba nimejihusisha katika kutengeneza, kuanzisha, kushiriki
uanzishwaji au kufahamu kikundi chochote kwa ajili ya kuniwezesha
kuwania uongozi ndani ya chama na kujihakikishia ushindi kutwaa
Uenyekiti wa Chama Taifa kinyume na taratibu.
Kuwachafua viongozi na wanachama
wengine wenye kusudio/nia ya kutaka kugombea nafasi ya Uenyekiti wa
Chama Taifa kinyume nakifungu cha 2(e) cha Mwongozo wa Kuwania Uongozi.Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa waraka ulioitwa Mkakati wa Mabadiliko 2013. 2.
Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au
nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kumkashifu Mwenyekiti wa Chama
Taifa, kiongozi mwenzangu au mwanachama yeyote Yule.
Kujihusisha na upinzani dhidi ya
Chama na makundi ya majungu ya kugonganisha viongozi na wanachama wakati
wa Uchaguzi wa Chama kinyume na Kanuni ya 10.3(4) ya Kanuni za
Uendeshaji.Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana niliandaa mkakati
wa kugonganisha viongozi na wanachama wakati wa Uchaguzi wa Chama kwa
kuwachafua viongozi wakuu wa Chama yaani Mwenyekiti wa Chama Taifa na
Katibu Mkuu kwa tuhuma nzito za uongo na kunipamba mimi. 2. Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au nikiwa na mtu mwingine yeyote.
Kukashifu Chama au Kiongozi wa
Chama nje ya Bunge kinyume na Kanuni 2(b) ikisomwa pamoja na Kanuni 3(b)
ya Kanuni za Mwenendo na Maadili ya Wabunge.Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1. Nakanusha kwamba mimi pamoja na Dk. Kitila Mkumbo, Bw. Samson Mwigamba na Mtu mwingine ambaye hajajulikana kwa kuandaa na kutumia waraka
uitwao Mkakati wa Mabadiliko 2013 nilitengeneza mtandao haramu ndani ya
Chama na nilitoa kashfa, matusi na uzushi dhidi ya Chama na viongozi
wake wakuu kwa lengo la kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama.
2. ambao ulikashifu Chama na/au viongozi wake wakuu nikiwa Mbunge wa CHADEMA na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni. 3.
Sijawahi kushiriki kwa njia yoyote kuandaa waraka huo peke yangu au
nikiwa na mtu mwingine yeyote. Nakanusha kwamba nimekashifu Chama au
viongozi wake wakuu nikiwa Mbunge wa CHADEMA na Naibu Kiongozi wa
Upinzani Bungeni kwa njia yoyote ile.
Kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama kinyume na Kanuni ya 3(f) ya Kanuni za mwenendo na maadili ya Wabunge.Mheshimiwa Katibu Mkuu;
1.
Mimi kama kiongozi wa Kitaifa sijawahi kutengeneza mtandao haramu ndani
ya Chama wala kutoa lugha ya matusi na uzushi dhidi ya Chama na
viongozi wake wakuu kwa lengo la kuchochea mgawanyiko ndani ya Chama.
HITIMISHO:
Mheshimiwa Katibu Mkuu;
a)
Nakanusha kila tuhuma mojamoja na kwa ujumla wake dhidi yangu. Mashtaka
yote dhidi yangu sio kweli na sijavunja Katiba au Kanuni za Chama. b)
Naiomba Kamati Kuu ijiridhishe kwa kiasi kinachostahili kuhusu mashtaka
yote niliyoshtakiwa nayo kwa kuangalia ushahidi wote uliotolewa au
utakaotolewa dhidi yangu. c)
Utetezi wangu umetolewa bila kupewa nakala ya Waraka unaosemekana
nimeuandaa ilhali kukiwa na maelezo kwamba kuna waraka ‘feki’ na waraka
‘original’ ambao umetumika na Kamati Kuu kufikia maamuzi yake. d)
Ndugu Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba kwa maneno yao wenyewe wametamka
kwamba hawakunishirikisa na sikushiriki kwenye uandaaji wa waraka ambao
ndio msingi wa mashtaka haya. Kamati Kuu inao ushahidi huo.
Wako katika ujenzi wa Chama,
.............................. ......................
Mh. Zitto Zuberi Kabwe (MB).