KOCHA ROBERTO DI'MATEO ATIMULIWA CHELSEA.....SOMA SABABU ZILIZOPELEKEA KIBARUA CHAKE KUOTA NYASI




 


LONDON, England
TAJIRI wa Chelsea, Roman Abramovich amemtimua Kocha Roberto Di Matteo baada ya mfululizo wa matokeo mabaya ya timu hiyo. Kutimuliwa kwa Di Matteo kulitegemewa na wengi hasa kutokana na utamaduni wa Abramovich kushindwa kuvumilia matokeo mabaya.

Di Matteo, amedumu kwa siku 262, na anaingia kwenye orodha ya makocha watano waliotimuliwa kabla hata ya kufikisha mwaka mmoja.
Makocha wengine ni Guus Hiddink siku 105, Felipe Scolari siku 223, Avram Grand siku 247 na Andre Villas-Boas siku 256.

Abramovich alichukizwa na matokeo mabaya ya timu hiyo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa, hasa kipigo cha aibu mabao 3-0 kutoka Juventus, usiku wa kuamkia Jumanne mjini Turin, Italia.

Uongozi wa juu wa Chelsea ulitarajia kukutana jana kumweleza Di Matteo kwamba siku zake za kuishi Stamford Bridge zimefika mwisho, miezi sita kupita tangu kuingoza timu hiyo kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Ulaya.

Akili ya Abramovich sasa iko katika kumnasa kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola, lakini atalazimika kutumia nguvu nyingi kumshawishi kocha huyo aliyekuwa nje ya soka kwa mwaka mmoja sasa.
Kama jaribio lake litashindwa, basi ataelekeza macho kwa kocha wa zamani wa Liverpool, Rafa Benitez.

Abramovich amechukizwa baada ya kuona timu yake iliyoanza msimu ikiwa na uwezo wa kushinda mataji saba, ikipoteza mwelekeo.

Ingawa alipotezea matokeo ya kipigo walichopata kutoka Manchester City kwenye mechi ya Ngao ya Hisani, lakini alichukizwa zaidi kipigo cha mabao 4-1 walichopata kutoka Atletico Madrid katika mchezo wa Kombe la Super.
Kipigo cha mabao 4-1 kutoka Atletico mjini Monaco kilikuja siku chache baada ya kutwaa taji la FA kwa kuichapa Liverpool.

Chelsea sasa inahitaji miujiza kusonga mbele hatua ya mtoano michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kutoka Kundi E.

Wako nyuma kwa pointi nne dhidi ya Manchester City katika michuano ya Ligi ya Barclays, na hawako tayari kupokea kipigo kingine baada ya wiki iliyopita kunyukwa mabao 2-1 na West Bromwich.

Mwenyewe Di Matteo amekiri kuwajibika na kipigo hicho kikubwa mjini Turin.
Alisema: Nawajibika kwa matokeo haya na kiwango kilichoonyeshwa na timu. 

Ni jioni mbaya kwetu, na kama kuna yeyote atahitaji kutoa lawama, basi ni mimi nayestahili kubeba.
Nilichagua timu ambayo niliamini usiku ule ingeweza kushinda mbele ya Juventus au angalau kupata sare. Hivyo, lawama zije kwangu.
Aliongeza: Sijaongea na kiongozi yeyote mkubwa, na naamini mimi siye mtu sahihi nayepaswa kuuliza hatima yangu ya baadaye hapa.

VIPIGO VILIVYOMCHUKIZA BOSI:
Oktoba 23: Shakhtar Donetsk 2 Chelsea 1 (Ligi ya Mabingwa)
Oktoba 28: Chelsea 2 Manchester United 3 (Ligi Kuu)
Oktoba 31: Chelsea 5 Manchester United 4 (Capital One Cup)
Novemba 3: Swansea 1 Chelsea 1 (Ligi Kuu)
Novemba 7: Chelsea 3 Shakhtar Donetsk 2 (Ligi ya Mabingwa)
Novemba 11: Chelsea 1 Liverpool 1 (Ligi Kuu)
Novemba 17: West Bromwich 2 Chelsea 1 (Ligi Kuu)
Novemba 20: Juventus 3 Chelsea 0 (Ligi ya Mabingwa)
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs