TAMKO LA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUFUATIA SHAMBULIO LA KIKATILI DHIDI YA MWENYEKITI WA JUKWAA LA WAHARIRI BW. ABSALOM KIBANDA
Mwenyekiti
wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda
---
TAMKO LA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUFUATIA SHAMBULIO LA KIKATILI DHIDI YA MWENYEKITI WA JUKWAA LA WAHARIRI BW. ABSALOM KIBANDA
---
TAMKO LA MTANDAO WA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUFUATIA SHAMBULIO LA KIKATILI DHIDI YA MWENYEKITI WA JUKWAA LA WAHARIRI BW. ABSALOM KIBANDA
Machi
07, 2013
--
Mtandao wa
watetezi wa haki za binadamu ambao ni kusanyiko la zaidi ya asasi 70 za
kiraia zinazotetea haki za binadamu (THRD-Coalition)
, kwa kushirikiana na Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habati Tanzania (UTPC)
pamoja na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini kwa Africa (MISA-Tan) tunalaani
vikali shambulio la kinyama alilofanyiwa mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri
Absalom Kibanda usiku wa kuamkia jana Jumatano tarehe 6 Machi, 2013.
Bw. Kibanda
alivamiwa wakati alipokuwa anarudi nyumbani kwake Mbezi juu. Watu hao walimteka
na kisha wakamtesa kinyama kwa kumng’oa meno, kucha, kidole na kuliharibu vibaya sana jicho la
upande wa kushoto. Huu ni ukatili, unyama dhidi ya utu wa binadamu. Baada ya
kutekeleza azma yao walimtupa umbali wa mita 30 toka alipokuwa amepaki gari
lake.
Uchunguzi tulioufanya
bado haujatujapatia habari za undani zaidi na za uhakika wa tukio hilo. Lakini
kwa taarifa za awali kwa asilimia kubwa linahusiana na kazi yake ya utetezi wa haki za
binadamu kupitia katika taaluma yake ya uandishi wa habari. Hii ni kwa sababu pia
tayari alishafunguliwa kesi mahakamani inayohusu uandishi wake.
Tunasema hivyo
kwa sababu vitisho dhidi ya wanahabari na watetetezi wengine wa haki za
binadamu vinataka kuzoeleka sasa hapa nchini jambo ambalo halikuwapo katika
miaka ya nyuma. Takribani ndani ya miezi 10 sasa zaidi ya watetezi wa haki za
binadamu 10 wakiwamo waandishi wa habari
wameshajeruhiwa, wamepata
vitisho au kuuwawa.
Matukio haya
yanaashiria lengo la kutaka kuzima sauti za watetezi wa wanyonge kwa visingizio
mbali mbali huku matukio ya aina hii wakati mwingine yakipewa sura tofauti
tofauti ikiwamo uhalifu wa kawaida, visa vya kudhulumiana na visasi vya kimapenzi. Ni dhahiri wanaofanya
hivyo wana malengo mabaya ya kuchafua jina na taswira nzuri ya nchi yetu katika
Jamii ya Kimataifa kwa malengo binafsi.
Wakati tukio
hili linapojitokeza sasa, bado Mtandao wetu unafuatilia kwa karibu kufungiwa
kwa gazeti la Mwanahalisi na mazingira ya kukamatwa na kuhojiwa kwa waandishi
wa gazeti la Tanzania Daima
kulikofanywa na Jeshi la Polisi hivi karibuni kwa kile kilichoitwa kwamba ni
kuandika habari za uchochezi.
Tunajiulia je
nini Jeshi la Polisi na Serikali kwa ujumla wamelifanya kuhusiana na kutekwa na
kuteswa kwa Dkt Ulimboka zaidi ya Kulifungia Mwanahalisi ambalo lilijitoa
mhanga kuchunguza suala hili? Ndugu Kibanda katekwa na kufanyiwa kile kile
alichofanyiwa Ulimboka, Je tume iliyoundwa
itaanzia kwa Ulimboka ama itarukia moja kwa moja tukio hili ambalo ni
muendelezo wa matukio lukuki dhidi ya watetezi wa haki na waandishi kwa ujumla.
Hatupendi
kuingilia wala kukwamisha utendaji kazi wa jeshi hilo, lakini pia hatupendi
wanahabari na watetezi wengine wafanye kazi yao katika mazingira ya woga.
Tunaamini kwamba zipo njia muafaka zaidi za kushughulikia masuala yanayohusu
taaluma ya habari. Kwa mfano lipo Baraza la Habari Tanzania (MCT) ambalo
linajukumu ya kusuluhisha migogoro inayohusiana na taaluma hiyo na iwapo
itashindikana basi mhusika au wahusika bado wanakuwa na nafasi ya kwenda
mahakamani.
Kinachoshangaza
ni kuona kwamba Jeshi la Polisi limefikia mahali pa kwenda kuwakamata waandishi
na wahariri wa Tanzania Daima ndani
ya chumba chao cha habari na kuwakagua
hadi katika makazi yao na kuchukua nyaraka kadhaa kama ilivyotokea kwaa Bw.
Josephat Isango.
Hali hiyo ya
mahojiano ya kushtukiza na kuogofya imefanyika pia kwa wahariri Charles Misango
na Edson Kamukara wote wa gazeti hilo, ambapo hatima yao bado haifahamiki mpaka
sasa. Hali hii inaweza kusababisha woga kwa wanataaluma wengine na hivyo kuleta
athari kubwa katika sekta ya habari nchini.
Waandishi hao
kwa sasa wanaishi kwa woga. Je kwanini tufikie hatua hii ya kufanya wenzetu
waishi kwa hofu kama swala kwenye mbuga
iliiyojaa simba?. Je ulinzi wa vyombo vya usalama upo kwa ajili ya nani?
Kwanini wengine wauawe, watekwe, wateswe na kudhalilishwa huku vyombo vya usalama vikichukulia ni jambo
la kawaida na kutupiana mpira?
Rai
Yetu
1.
Tunawataka
watu wote wanaotumika au wanaoendeleza
wimbi la mashambulizi kwa wanahabari na watetezi wote wa haki za binadamu kwa
ujumla, waache kufanya hivyo kwani wataliingiza nchi katika machafuko makubwa.
2.
Tunalisihi
Jeshi la Polisi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kubeba jukumu
lao la kuhakikisha usalama wa watetezi wa haki za binadamu, na raia na watu
wote waliomo ndani ya mipaka ya nchi hii kwa ujumla bila ubaguzi.
3.
Tunaomba
uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini wahusika wa mtindo huu wa kuteka kutesa
na kutelekeza kwani tukio hili la Kibanda linashabihiana kwa kiwango kikubwa na
lile la Dkt Stephen Ulimboka.
4.
Tunaiomba
jamii yote ya watu waliostaarabika, makundi mbalimbali kutuunga mkono katika
jitihada zetu la kupigania amani, haki na uhuru kwa watu wote hasa hasa
watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari.
5.
Tunawakumbushia
waandishi wa habari kujitahidi kupata mafunzo ya usalama ambayo yanaratibiwa na
kutolewa na Mtandao huu wa watetezi.
6.
Vyombo
vyote vya habari na waandishi kwa ujumla wazidi kuwa pamoja
katika kipindi hiki kigumu cha kuelekea chaguzi za serikali za mitaa mwakani
pamoja na uchaguzi mkuu 2015. Pia wajieupushe na makundi ya kisiasa ili
kujiweka vizuri katika kufanya kazi zao kwa kufuata misingi ya taaluma zao.
Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania!
Imeletwa kwenu na
Onesmo Olengurumwa
Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa
Haki za Binadamu
Tanzania (THRD-Coalition)
K.n.y Watetezi
Wote wa Haki za Binadamu Tanzania
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII