MAAJABU YA MSIBA WA MANDELA NDIO HAYA

RAIS wa zamani wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela, mweusi wa kwanza kushika wadhifa huo katika taifa lenye uwezo mkubwa kiuchumi na kijeshi barani Afrika, alifariki dunia Alhamisi iliyopita akiwa nyumbani kwake jijini Johannesburg.
Nelson Mandela.
Kifo chake kimeushtua ulimwengu na kwa mara ya kwanza katika historia, dunia nzima imesimama nyuma ya jemedari huyo, kila mmoja akionesha masikitiko yake.
Wakati dunia ikisubiri mazishi yake ambayo pia yatavunja rekodi ya mazishi yote yaliyowahi kufanywa tokea kuumbwa kwa uso wa dunia hapo Desemba 15 mwaka huu, Uwazi limebaini maajabu kumi yanayoambatana na msiba huo.
AIR FORCE ONE KUBEBA MARAIS WATANO WA MAREKANI
AIR Force One ni ndege inayombeba Rais wa Marekani aliye madarakani na kumpeleka popote duniani. Lakini katika hali ya kushangaza, Idara ya Usalama ya Marekani imetoa ruhusa kwa marais wastaafu wakiwa na wake zao, kuandamana na Rais Barak Obama kuhudhuria mazishi ya shujaa huyo wa dunia.
Hii ni mara ya kwanza katika historia ya taifa hilo lenye nguvu kubwa duniani kuwapakia katika ndege hiyo yenye kila kitu ndani yake, marais wake kwa wakati mmoja.
Marais hao ni Obama mwenyewe na mkewe Michelle, George Bush na mkewe Laura, Bill Clinton na mkewe Hillary, Rais wa 39 wa Marekani, Jimmy Carter naye atakuwepo ila baba yake George W. Bush, George Bush senior huenda asiende kutokana na urefu wa safari hiyo.
QUNU; KIJIJI KITAKACHOLNDWA KULIKO VYOTE DUNIANI
Mandela alizaliwa katika Kijiji cha Qunu, kilichopo katika Jimbo la Eastern Cape, kilometa 32 Kusini Magharibi mwa mji wa Mthatha.
Kutokana na tukio hilo kubwa la mazishi, Jeshi la Afrika Kusini ambalo ni bora zaidi barani Afrika, limechukua jukumu la kusimamia ulinzi wote. Lakini uwepo wa Rais Obama na watangulizi wake wanne, utaifanya nchi hiyo kuchukua tahadhari zaidi ya kuhakikisha hakuna dosari yoyote ya kiusalama inayoweza kujitokeza.
Ulinzi huo umeimarishwa zaidi kutokana na ukweli kwamba viongozi wakubwa karibu wote wa dunia watahudhuria mazishi hayo, akiwemo Papa Francisco, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon. Hakuna uwezekano wowote wa Al shaabab kusababisha rabsha kwani wameshadhibitiwa kwa ulinzi mkali.
MANDELA ALIKUWA  ‘GAIDI’ PEKEE ALIYEGEUKA KUWA SHUJAA
Kwa miaka mingi, mataifa ya magharibi pamoja na Marekani walimchukulia Mandela na harakati zake kama gaidi. Wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, chama cha ANC kilikuwa na jeshi lake lililofahamika kama Umkhonto we Sizwe. Wazungu wa Magharibi na Marekani ambao walikuwa wakiwaunga mkono Makaburu, waliiona ANC kama kikundi cha kigaidi na hivyo Mandela naye akawekwa katika orodha ya magaidi duniani.
Hata hivyo, baada ya kutoka jela na kuchaguliwa kuwa Rais wa Afrika Kusini, Mandela aligeuka kuwa kipenzi cha watu hao ambao walilazimika kumuondoa katika orodha ya magaidi na leo hii akiwa amefariki dunia, anapewa heshima kubwa kuliko aliyowahi kupewa mzungu yeyote duniani.
MWEUSI PEKEE ALIYENYENYEKEWA NA WAZUNGU
Hayati Mandela ndiye mtu mweusi pekee duniani aliyewahi kupewa heshima zisizo na mfano tokea kuumbwa kwa dunia. Mara baada ya kutangazwa kwa kifo chake, viongozi wa mataifa yote makubwa duniani walionesha masikitiko yao na kila mmoja alimsifu kama mtu wa aina ya pekee kuwahi kuwepo chini ya jua (ukiachia mbali mitume na manabii).
JENGO LA SERIKALI NEW YORK LAPAKWA RANGI YA BENDERA YA SAUZI
Jengo moja la serikali jijini New York, Marekani limebadilishwa taa za kulipamba na kuonesha bendera ya taifa la Afrika Kusini.
WENYEJI WAHAMA, WAGENI WAMILIKI NYUMBA QUNU
Kijiji cha Qunu, sehemu ambayo yatafanyika mazishi ya Mandela, kuna eneo dogo kulingana na ugeni mkubwa unaotarajiwa kuwepo. Taarifa kutoka huko zinasema wenyeji, pamoja na machungu waliyonayo kutokana na kifo cha mzee huyo, pia watafaidika kiuchumi kutokana na wageni wengi kutaka kupata nyumba za kukaa wakati wakiendelea na maombolezo.
Wanaotafuta nyumba kijijini hapo ni pamoja na watu kutoka vyombo mbalimbali vya habari, mashirika ya kimataifa na wageni binafsi.
Inadaiwa kuwa wenyeji wanasogea katika vijiji vya jirani ili kupangisha nyumba zao kwa muda.
MECHI ZA LIGI KUU ENGLAND ZAANZA KWA SALA
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Chama cha Soka cha England (FA) kiliamuru mechi zote za ligi kuu zilizochezwa wiki iliyopita, lazima zianze kwa sala maalum ya kumuenzi mzee Mandela.
Hii ni mara ya kwanza kwa agizo hilo kutolewa kwa heshima ya kiongozi mstaafu aliyefariki dunia asiye Mwingereza, tena akitokea barani Afrika. Tukio kama hilo pia limefanywa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambalo limeamuru bendera yake iliyo katika mataifa yote wanachama duniani, ishushwe nusu mlingoti kwa heshima ya Tata Madiba!
NASA YATOA ZAWADI YA  PICHA YA SAUZI KUTOKA ANGANI      
Taasisi ya utafiti wa anga za juu nchini Marekani (NASA) kwa kutambua mchango mkubwa wa Mandela katika amani ya dunia, imetangaza kutoa zawadi kwa watu wa Afrika Kusini, itakayoonesha picha ya nchi hiyo inavyoonekana kutoka angani.
UINGEREZA YAAGIZA BALOZI ZOTE KUSHUSHA NUSU MLINGOTI
Serikali ya Uingereza imeziagiza balozi zote za kigeni zilizopo nchini humo kushusha bendera zao nusu mlingoti kama moja ya heshima na maombolezo ya kifo cha Mzee Nelson Mandela.
Hili ni agizo la aina yake kuwahi kutolewa kuhusiana na msiba wa kiongozi yeyote, kwani suala la kushusha bendera mara nyingi ni uamuzi wa serikali husika na si kwa shinikizo kama ilivyotokea Uingereza.
AMSAFIRISHA PAPA MAZISHINI
Historia ya utumishi wa kiongozi mkuu wa Madhehebu ya Romani, papa haioneshi kama aliwahi kuhudhuria mazishi ya rais au rais mstaafu, kitendo cha Papa Francisco kuhudhuria mazishi hayo kumeongeza ajabu katika mazishi ya Mandela, wengi wakisema hakina hakuwa mtu wa kawaida.

SOURCE : GPL
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs