DIAMOND AMPA MAKAVU BABA AKE
SIKU chache baada ya kuibuka kwa baba aliyemlea Nasibu Abdul ‘Diamond Platinumz’ aitwaye Abdul Juma na kudai kuwa mwanaye huyo amemtelekeza na hamjali, mwanamuziki huyo amemchana mzazi wake huyo, Ijumaa lina kitu kamili.
Akizungumza redioni kupitia Clouds FM, Jumatatu wiki hii, Diamond alidai kushangazwa na mzazi wake huyo huku akimtaka kuacha kusema maneno hayo kwani siyo mazuri.
“Kiukweli ni vitu ambavyo mimi vimenishangaza sana kwa sababu sijui chochote na nisingependa nisikie suala la mzazi wangu kusema mimi ni mtoto wake, sijui nini na nini kwamba mimi nafanya starehe sihusiki na yeye, siyo kauli nzuri kiukweli, ina maana ananijua kwamba mimi ni mwanaye baada ya kuwa Diamond?
“Siku zote kama alijua mimi ni mtoto wake, basi angenisomesha na kunipa elimu nzuri, lakini nilihangaika na mama yangu mzazi (Sanura Khassim ‘Sandra’) akanikuza na kunisomesha kwa shida na tabu zote mpaka leo nimekuwa hivi nilivyo, nisingependa kumsikia mtu yeyote anaongea kwamba mimi ni mtoto wake au yeye ni nani kwa sababu siku zote hawakuonekana, wasitake kuonekana kipindi cha masilahi, mtu ndiyo anajifanya anahusika sana na mimi kama mtoto wake.
“Haya mambo nilianza kuyasema toka nilipotoa single (wimbo) ya Binadamu, sikujua hata kama leo ningekuja kuwa na Prado (gari alilonunua juzikati la zaidi ya Sh. milioni 60), makazi (anajenga nyumba Tegeta, Dar na tayari imetumika Sh. milioni 69) au kuwa na haya mafanikio mengine, baba yangu ataendelea kuwa baba yangu tu ila siwezi kumpa kipaumbele kama ninachompa mama yangu kwa sababu kama angetaka hilo angenijali toka mapema.
“Mimi nilikuwa napenda kusoma na nilikuwa nafanya vizuri kwenye masomo yangu, lakini sikuwa na uwezo wa kifedha kuendelea kusoma, mzazi wangu alikuwa na fedha, ina maana angenijua mimi angenisomesha, leo ningekuja kuwa hata mbunge au waziri kwa sababu mimi najua nina upeo mkubwa sana wa kielimu na vitu vingine, sasa nimesota na muziki halafu leo ndiyowanajitokeza.
“Sitaki, naomba waniache na mama yangu mzazi,” alitiririka Diamond.
Baada ya kutoa maneno hayo makali kwa mzazi wake huyo, Ijumaa lilizungumza na mzee Abdul ambapo alisema kwa kifupi bila kufafanua: “Basi sawa siyo mwanangu.” Wiki mbili zilizopita, mzee Abdul aliibuka na kusema kuwa Diamond ni mwanaye lakini hamjali na badala yake amekuwa akiponda starehe.
Hata hivyo, wiki moja baadaye ndugu wa Diamond waliibuka na kudai kuwa mzee Abdul siyo baba halisi wa msanii huyo bali baba halisi ni Idd Salum, ambaye alifariki mwaka 2004 ambapo Platnumz hakufafanua suala hilo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI



0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII