HOTUBA YA MH.EDWARD LOWASSA KWA WAANDISHI WA HABARI,MONDULI 19 OCTOBER 2011

Hapo
jana,aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania na Mbunge wa sasa wa
Monduli,Mh.Edward Lowassa,alivunja kile ambacho vyombo vya habari
vimekiita “ukimya wa muda mrefu” na kuongea na waandishi wa habari
kuhusu mambo mbalimbali ili kuweka rekodi sawa(setting the records
straight) kutokea jimboni kwake Monduli.Hii hapa ni hotuba kamili endapo
hukupata nafasi ya kuisikia.Nini maoni yako kuhusu hotuba hii?
NDUGU wana habari
nimewaita katika mkutano huu leo kwa sababu moja kubwa, kutoa ufafanuzi
kuhusu matukio ambayo yamekuwa yakitokea huku yakinihusisha mimi
binafsi kwa namna ambayo sasa yanatishia ustawi na mshikamano wa
kimaadili, kihistoria na kikazi miongoni mwa viongozi na baina ya
wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ndugu wana habari, naamini mmkekuwa mkifuatilia kwa karibu habari
zinazoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari zinazolihusisha jina
langu na harakati kadha wa kadha chafu ambazo hata mimi mwenyewe
ninayehusishwa nazo huwa nazisikia na kuzijua baada ya kuwa
zimesharipotiwa katika vyombo vya habari.
Uamuzi wangu wa kukutana nanyi leo hauna makusudi ya kuzozana na
vyombo vya habari wala kwenda kinyume na utamaduni wa kimaadili wa ndani
ya chama changu unaotutaka viongozi kujadili masuala yanayokihusu chama
chetu ndani ya vikao vyetu rasmi vya kimaamuzi bali kutoa ufafanuzi na
angalizo kwa pande zote hizo mbili ambazo zinaguswa na matukio
yanayoendelea kutokea leo hii.
Moja ya mambo ambayo yameligusa jina langu kwa namna hiyo ni lile
linalonihusisha eti na kundi moja la wanasiasa ambao wamekuwa na
mikakati ya kumhujumu mwenyekiti wetu wa chama, Mheshimiwa Rais Jakaya
Kikwete. Hakuna shaka ni madai ya kipuuzi, kizushi na yenye malengo
machafu.
Hawakuishia hapo sasa wamefikia hatua ya kuvitumia vyombo hivyo hivyo
vya habari kufikia hatua ya kudai kwamba nimeanza kuandaa orodha ya
kile wanachokiita madhambi ya Rais Kikwete ambayo wandai nimepanga
kuyasoma wakati wa kikao kijacho cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
(CCM).
Ninaamini kwa dhati kabisa kwamba, waandishi wa habari wanaofuatilia
kwa karibu na kwa umakini mwenendo wa masuala ya kisaiasa nchini
wanatambua kwamba, watu wanaopenyeza taarifa hizi katika vyombo vya
habari wanafanya hivyo kwa malengo ya kufikirika na kujisafishia njia
kisiasa.
Ni jambo lisiloingia akilini kunihusisha na kile kinachoitwa mikakati
ya kumhujumu rais au chama ambacho mimi ni kada wake wa muda mrefu,
mbunge anayetokana na chama hicho hicho na mtu anayeiongoza Kamati nyeti
ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na zaidi ya yote kiongozi
wa ngazi mbalimbali za kisiasa na kiserikali nilizowahi kushikilia.
Kuhusu hili napenda kusema kwa uwazi kwamba, mbali ya ukweli kuwa
sijapata kufikiria hata mara moja kuhusu hicho wanachokiita mabaya au
madhambi ya rais, sina wala siijui hiyo wanayoitaja kuwa ni orodha ya
mabaya ya namna yoyote dhidi ya Rais Kikwete.
Mbali ya ukweli kwamba huo ni uongo wa wazi, silika yangu kama
mwanasiasa na mtu mwenye dhamana kubwa kwa watu wa Monduli na kwa taifa
langu haiwezi kamwe kunituma nianze kupanga mikakati ya kumhujumu
kiongozi wetu mkuu au chama ambacho kimenilea na mimi mwenyewe
nikakitumikia kwa uadilifu na kwa juhudi kubwa pengine kuliko ilivyo kwa
hao wazushi.
Ndugu wana habari, nitakuwa ni mtu wa mwisho kufikiria au kupanga
kumhujumu mwenyekiti wetu wa chama na rais ambaye nimemuunga mkono kwa
dhati kwa muda mrefu na kushirikiana naye katika harakati nyingi za
kifikra na za kiuongozi katika ngazi mbalimbali na kwa miaka mingi.
Nilipatana kuliesema hili na leo nalirudia tena. Mimi na Rais Kikwete
hatukukutana barabarani.
Tangu serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani kuna kundi la watu
limekuwa likifanya juhudi kubwa kunigombanisha na Rais wakitumia kila
aina ya hoja za kupikwa.
Kundi hilo ambalo sasa limekuja na uzushi mpya, ndilo ambalo mwaka
juzi lilipenyeza ndani ya chama chetu na katika jamii hoja kwamba
nilikuwa nimejipanga kugombea urais kwa tiketi ya chama chetu katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, likidai kwamba nilikuwa na mlango ya
kumpinga Rais Kikwete ambaye wakati huo alikuwa ndiyo kwanza anaelekea
kukamilisha ngwe yake ya kwanza madarakani.
Katika kuthibitisha kwamba watu hao walikuwa na hila, nilipohojiwa na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam miezi kadha kabla ya Uchaguzi
Mkuu nilijibu kwa kifupi nikisema, hatukukutana na Rais Kikwete
barabarani.
Nayasema haya na kurejea baadhi ya mambo
huku nikiwa na imani ya dhati kabisa kwamba, viongozi wenzangu ndani ya
CCM na wale walio na nia njema na chama chetu na taifa hili, akiwapo
Mwenyekiti wetu wa Taifa, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete hawawezi kamwe
kuamini kushawishiwa na propaganda chafu zinazoendeshwa na kikundi
kidogo cha wanasiasa hao kwa zaidi ya miaka mitatu sasa ambayo malengo
yao ya kisiasa yako wazi na yanayojulikana.
Kama hiyo haitoshi, wanasiasa hao hao baada ya kulitumia jina langu
kama ajenda yao ya uzushi wa kila namna, sasa wameanza kunihusisha
hata na matukio ya kisiasa kama yale yaliyotokea majuzi tu hapa Arusha.
Ndugu wana habari baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu sasa, nimeamua
kuanza kuchukua hatua mbalimbali za kisiasa na kisheria ambazo namini
zitatoa majibu sahihi dhidi ya wale wote walio nyuma ya ajenda hizi
chafu kwa lengo la kuweka kumbukumbu sawia ndani ya chama changu na kwa
jamii nzima ya Watanzania ambao kwa muda mrefu wamelishwa mambo mengi ya
kizushi na wakati mwingine ya hatari dhidi yangu.
Tayari nimepanga kuanza kuwasiliana na kuwasilisha malalamiko yangu
kwa mamlaka husika zinazosimamia mienendo ya kimaadili na weledi wa
kitaaluma wa vyombo vya habari kama vile Msajili wa Magazeti na Baraza
la Habari Tanzania.
Kama hiyo haitoshi, baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu nimeshaanza
kufikiria na kujipanga kuanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya
waandishi wa habari na wahariri ambao kwa makusudi wameamua kutumia
vibaya uhuru wa habari ambao serikali imeutoa. Naamini sote
tunakubaliana kuwa; ‘UHURU USIO NA NIDHAMU NI FUJO.’
Ndugu zangu wana habari napenda kutumia furasa hii kutoa wito kwa
viongozi wa chama na wale wa serikali kumsaidia rais na chma chetu kwa
kutimiza ipasavyo wajibu wao badala ya baadhi yao tena wakiwamo wale
wenye dhamana nyeti kuwa vinara wa kutunga mambo ya kufikirika kama haya
wanayofanya leo.
Viongozi wenye mawazo ya namna hiyo wanapaswa kutambua kwamba, muda
adhimu wanaoutumia kubuni na kuzusha uongo kila kukicha mbali ya
kuwavunjia heshima wao weneywe unavidhalilisha vyombo vya dola ambavyo
vinafanya kazi kubwa kuhakikisha hujuma za namna yoyote dhidi ya
viongozi na taifa zinadhibitiwa.
Nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ya
Bunge na mtu aliyepata kuwa Waziri Mkuu ninatambua na kuiheshimu kwa
dhati kazi hiyo kubwa inayofanywa kwa weledi mkubwa na taasisi
mbalimbali za dola zenye wajibu wa kuhakikisha ulinzi na usalama wa
viongozi wetu na taifa kwa ujumla.
Ndugu wanahabari nazungumza nanyi baada ya kurejea nikitokea katika
nchi za Nigeria, Malaysia, Singapore, India, Uingereza, Ufaransa na
Ujerumani ambako nilipata fursa ya kujifunza mambo mengi lakini moja
muhimu likiwa ni namba vyombo vya habari (kwa maana ya waandishi wa
habari) na wanasiasa wanavyotumia muda wao mweingi kujadili amasuala
yanayogusa maisha na maendeleo ya watu wao.
Tofauti na kile wanachofanya wenzetu hapa nyumbani, ninyi wanahabari
na sisi wanasiasa tumekuwa tukitumia muda wetu mwingi kujadili watu na
propaganda za kisiasa zisizo na tija wakati tukitambua kwamba, taifa
linakabiliwa na changamoto nyingi kama zile za kuhamasisha uwezekazji wa
ndani na nje ya nchi, kuimarisha mifumo ya utawala bora, kuporomka kwa
thamani ya shilingi kila kukicha, mdororo wa uchumi, tatizo kubwa la
ajira kwa vijana, kushuka kwa kiwango cha elimu na ugumu wa maisha kwa
ujumla.
TUNAPASWA KUJISAHIHISHA.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII