BRANDTS WA YANGA AIPA SIMBA WIKI SITA, ASEMA YANGA HAITASHIKIKA...SOMA ZAIDI HAPA

 KOCHA wa Yanga, Ernest Brandts amecheka baada ya kusikia Mnyama wa Msimbazi kapigwa bao na Mtibwa Sugar lakini ameitamkia Simba kwamba ndani ya wiki sita tu baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza timu yake haitashikika.

Ingawa amefurahi kwamba vijana wake wamepenya kibabe mpaka kutua kileleni amesisitiza kuwa baada ya matizi magumu ya wiki sita aliyopanga kuwapa wachezaji hakuna timu itaweza kuwababaisha kwani watakuwa wameiva.

Brandts ametamka kwamba anahitaji kuwapigisha zoezi kali sana tena kwa wiki sita mfululizo baada ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza, Jumapili ijayo.

Yanga ndiyo timu pekee kuishusha Simba kileleni ilipokuwa imepiga kambi tangu kuanza kwa msimu huu, kwani Azam ilijaribu mara kadhaa ikashindwa.

Yanga imekalia usukani ikiwa na pointi 26 ikiwa ni pointi tatu juu ya Simba ambayo juzi Jumapili ilifungwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar mjini Morogoro huku Yanga ikiichapa Azam idadi hiyo hiyo ya mabao.

Brandts baada ya kusikia matokeo ya Simba aliiambia Mwanaspoti kauli hii: "Safi. Hayo matokeo ni mazuri kwetu tunaongoza ligi vizuri kabisa na timu imeanza kukaa kwenye fomu na ukiangalia mechi hizi nne zilizopita tumekwenda vizuri sana kiuchezaji na hata matokeo.

"Sijapata muda wa kuitengeneza timu kwa kuwa tunafanya mazoezi tukiwa tunacheza ligi sasa hilo ni tatizo, baada ya mechi dhidi ya Coastal Union nitahitaji wiki sita mfululizo za mazoezi ya nguvu ili kuiweka timu fiti zaidi," alisema kocha huyo ambaye huenda akawakosa wachezaji kadhaa watakaoitwa Kilimanjaro Stars, Rwanda, Burundi na Zanzibar Heroes zinazoshiriki Kombe la Chalenji jijini Kampala, Novemba 24 mpaka Desemba 8, mwaka huu.

"Timu haina mazoezi ya kutosha ingawa ukiangalia unaona inacheza vizuri. Ninachotaka kufanya sasa ni kuhakikisha tunaendelea na morali hii ili tuishinde kwanza Coastal tumalize vizuri mzunguko wa kwanza.

"Tunajua ni timu ngumu na mechi ngumu hasa ukitegemea tutakuwa ugenini lakini tuna ubora stahiki wa kushinda mechi kiufundi," alisema.

Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu unamalizika Novemba 11 wakati Simba itacheza na Toto Africans jijini Dar es Salaam huku Coastal Union na Yanga zikiwa Mkwakwani, Tanga.

Mbali na mechi hizo, Prisons itakipiga na JKT Ruvu, Mbeya wakati Kagera Sugar itaikaribisha Polisi Morogoro mjini Bukoba na wanajeshi wa JKT Oljoro na Ruvu Shooting watacheza Arusha.


TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs