MAGUFULI AMTAKA RAIS KIKWETE AZIDISHE SAFARI ZA NJE, SOMA ZAIDI HAPA
WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli amemtaka Rais Jakaya Kikwete
kuongeza safari za nje, kwa sababu zinazochochea maendeleo kwa kasi
nchini.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara kwenye
ufunguzi wa Barabara ya Minjingu- Babati-Singida juzi, Dk Magufuli
alisema Rais Kikwete ametekeleza ahadi zilizopo kwenye ilani ya CCM ya
mwaka 2010.
“Wapo wanaosema wewe Rais unatembea sana nje ya
nchi, lakini bila kutembea kwako tusingepata maendeleo tunayopata, hivyo
tunakuomba uendelee kutembea ili tuendelee kupata maendeleo zaidi,”
alisema Dk Magufuli. Pia, aliwataka wananchi hasa wafugaji mkoani hapa kuhakikisha wanaitumia vizuri barabara hiyo, ili kuitunza na wasiiharibu.
Waziri Magufuli alisema vyema wakafuata sheria za
barabarani, ikiwamo kupeleka mifugo maeneo yasiyo na vivuko na kwamba,
hiyo itawaepushia hasara ya mifugo yao kugongwa na vyombo vya usafiri.
Akizindua barabara hiyo, Rais Kikwete alisema
shabaha ya Serikali ni kuwatumikia wananchi wake kwa kutekeleza ahadi
ilizotoa na kwamba, anapenda kila Mtanzania aishi maisha bora. “Sipendi nipige hatua huku wenzangu wakibaki
maskini, wapo waliokuwa wanadai wanatetea haki za Wamasai ili wapate
huduma muhimu za jamii, lakini wakati huohuo wao ndiyo waliokuwa
wakinufaika, huku wenzao wakiwa hawana wanachokipata kwa utetezi wao,”
alisema Rais Kikwete.
Baada ya kufungua barabara hiyo, Dk Kikwete
alisema Serikali yake imelenga kuunganisha mikoa yote kwa barabara za
lami na kuahidi kuwa, kazi iliyobaki hivi sasa ni kuunganisha barabara
ya Mkoa wa Manyara na Mkoa wa Dodoma, ambayo ujenzi wake tayari umeanza. “Nimeahidi kujenga barabara ifikapo mwaka 2015 CCM
ikiingia madarakani iweze kumalizia patakapobaki, kwani nina uhakika
hakuna chama kingine kitakachoweza kushika madaraka nchini zaidi ya
CCM,” alisisitiza.
Pia, alisema iwapo kutakuwa na ahadi
zitakazoshindwa kutekelezwa kipindi cha uongozi wake, hakuna sababu ya
wananchi kuilaumu Serikali kwani yapo mengine ya miaka ya nyuma ambayo
alianza nayo.
“Kama yale niliyoahidi sitaweza kuyatimiza yote,
lakini baadhi nimeshayafanya kwani mengine ni ya miaka 20 iliyopita,”
alisema Rais Kikwete.
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII