HUU NDIO UKWELI KUHUSU UTATA ULIOTOKEA KANISA KUU LA DODOMA BAADA YA KUHISI UAMSHO WAMEINGIA KANISAN NA KUTAKA KUFANYA YAO
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, kijana mmoja juzi alizua taharuki katika Kanisa Katoliki baada ya kuingia ndani ya kanisa akiwa amevaa kanzu. Tukio hilo lilitokea juzi asubuhi wakati waumini wa kanisa hilo wakiwa kwenye ibada.
Kijana huyo aliyefahamika kwa jina la Hassan Said (27), maarufu kama Magido, aliingia katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo la Dodoma.
Baada ya kuingia kanisani humo, waumini walihamaki wakidhani Said ni kati ya wafuasi wa Kikundi cha Uamsho na na ameingia kanisani kwao kwa lengo maalum la kufanya uharifu.
Kutokana na hali hiyo, waumini hao walijikuta wakiacha mafundisho waliyokuwa wakiyapata kwa wakati huo na hivyo kutaka kumpiga Said kabla hajaleta madhara kanisani hapo.
Hata hivyo, waumini hao hawakufanikiwa kumpiga baada ya wao wenyewe kuanza kupingana.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Jeshi la Polisi, Mkoa wa Dodoma ilisema kwamba, kijana huyo hakuwa mfuasi wa Kikundi cha Uamsho bali ana matatizo ya akili.
“Machi 9 mwaka huu wakati ibada ikiendelea katika kanisa hilo, aliingia kanisani kijana mmoja akiwa amevalia mavazi ya kiislamu jambo ambalo si la kawaida na akakamatwa na waumini na kufikishwa polisi.
“Baada ya kuhojiwa, alijitambulisha jina lake na ili polisi kujiridhisha, walikwenda kumpekua anapoishi na bibi yake eneo la Chinangali hapa hapa Dodoma mjini ambapo alikutwa na vyeti vya Hospitali ya Mirembe.
“Vyeti hivyo vinaonyesha kwamba, Said aliwahi kulazwa katika hospitali hiyo mara tatu ikiwa ni kuanzia mwaka 2008.
“Kwa hiyo, kijana huyo aliyeingia katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba Mkoa wa Dodoma, hakuwa mwanauamsho kama ilivyovumishwa bali aliingia kanisani humo kutokana na matatizo yake ya akili,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya polisi, mbali na polisi kuona vyeti vya Said, walimpeleka katika Hospitali ya Mirembe ambako alitambuliwa na wauguzi wa hospitali hiyo.
“Kwa sasa kijana huyo yuko katika Hospitali hiyo ya Mirembe na anaendelea na matibabu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Dodoma, David Misime.
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII