DK SLAA AMWAGA SIRI ZA SAMWEL SITTA


SIRI iliyokuwa imefichwa kwa zaidi miaka miwili sasa, baina ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Urambo Samwel Sitta, imefichuliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa hoteli ya MR mjini hapa jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa alisema ilikuwa Mei mwaka 2010, Sitta ambaye hivi sasa ni Waziri wa Afrika Mashariki alipokutana na viongozi wa Chadema na kuonesha dhamira ya kujitoa CCM na kujiunga na chama chao.
Katika mazungumzo hayo yaliyoendelea kufanywa katika kipindi chote cha bunge la bajeti lililokuwa la mwisho kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dk Slaa alisema katika masharti yake ya kujiunga na Chadema, Sitta ambaye kwa wakati huo alikuwa Spika, alitaka apewe nafasi ya kuwania urais kupitia chama hicho.
Alisema ameamua kutoa siri hiyo baada ya kiongozi huyo (Sitta) kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari juzi akidai kwamba Dk Slaa ni mtu pekee ndani ya Chadema ambaye ni tishio kwa urais katika uchaguzi ujao, huku akimponda Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwamba ni mchezesha disco.


“Chadema haipendi kuzungumza habari za watu, inazunguma maendeleo. Kwa muda mrefu tumemuhifadhi Sitta lakini baada ya kupeleka mashambulizi sehemu isiyohusika sasa tunampiga ngumi za tumbo na uso,” alisema.
Alisema wakati akitaka aandaliwe mazingira ya kujiunga na Chadema na kupewa nafasi ya kuwania urais, Sitta alidai ana kundi la wabunge zaidi ya 55 waadilifu kutoka katika chama hicho ambao angetoka nao pamoja CCM na kuhamia Chadema kabla ya bunge kuvunjwa. Alisema kwa kuwa Chadema haina ubinafsi, ilihadi kuyafanyia kazi maombi yake ya kuwania urais kwa uzito mkubwa hata hivyo katika mazingira ya kushangaza aliwatelekeza. Dk Slaa alisema Sitta ambaye uzoefu wake katika siasa na umakini wake katika kushughulikia maendeleo ya nchi umeanza kuwatia shaka watanzania, alisahau jinsi alivyowatelekeza kabla ya Uchaguzi Mkuu na baada ya uchaguzi huo akaja na hoja mpya kitaka Chadema wampe nafasi ya kuwania uspika kwa kile alichodai kuwepo kwa mizengwe ndani ya CCM.


Katika mazingira ya kushangaza badala ya kufikia uamuzi wake wa kuhamia Chadema kama dhamira yake ilivyomtuma, Sitta aliwatelekeza tena akidai kwamba atajiunga na chama hicho mpaka pale atakapokwenda jimboni kwake Urambo na kutangaza rasmi kujiondoa CCM. Alisema kiongozi huyo aliyekuwa akitaka msaada wa viongozi wa Chadema ili afanikiwe kujiunga na chama hicho na hatimaye kupewa nafasi ya kuwania nyadhifa alizokuwa akitaka ameanza kuwatusi hadharani viongozi hao akiwemo Menyekiti wake Mbowe.

Alisema kauli inayotolewa na Sitta kwamba Mbowe ni mchezesha disco inadhihirisha jinsi asivyo makini jambo linalowafanya waanze kuitilia shaka elimu na uzoefu alionao katika kuendesha shughuli za serikali. Mbowe anazo biashara ikiwemo ya kumbi za burudani ambayo anaziendesha kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi.
“Sita anataka kutuambia kwamba watu wanaocheza disco wakiwemo mawaziri wengi tu wanaokutwa kwenye kumbi za burudani wanatenda dhambi na ni uhalifu kufanya hivyo?,” alisema. Alisema kama biashara hiyo ya Mbowe inafanywa kinyume na sheria za nchi, serikali inasubiri nini kufuta leseni yake.
Kuhusu uongozi na namna ya kupata viongozi ndani ya chama hicho, Dk Slaa alisema sio kazi ya Sitta akuwapangia utaratibu.

“Sitta hajui kwamba duniani hakuna chuo cha kusomea uwaziri, ukatibu mkuu, na hajui kwamba Mwalimu Julius Nyerere hakuwa na uzoefu wakati akipewa madaraka ya kuongoza taifa hili na kwamba hata wasaidizi wake nao walipata uzoefu baada ya kupata madaraka,” alisema. Alisema Sitta ni kiongozi mnafiki na atakumbukwa zaidi alipokuwa Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwasababu kuna hoja mbalimbali zilizowasilishwa na wabunge wa upinzani kuhusu ufisadi alizizima.
Alisema kuzimwa kwa hoja hizo ikiwemo ya Mkataba uliogubikwa na utata wa Buzwagi, unadhihirisha jinsi naye alivyotumia madaraka yake vibaya kwa kujenga ofisi ndogo ya Spika ambayo yeye aliita ya mbunge jimbo kwake Urambo.
Alisema wakati serikali imeridhia ofisi za wabunge zijengwe kwa kiasi cha fedha kisichozidi Sh Milioni 40 kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha, ofisi hiyo ya Urambo ilijengwa kwa Sh Milioni 350.
“Kauli zinazotolewa na Sitta kuhusu chama chetu zinadhihirisha jinsi alivyomnafiki na asivyofaa jambo lililosababisha hata CCM wamemnyime nafasi ya kuwania kugombea kwa mara nyingone tena nafasi ya Uspika,” alisema.
Dk Slaa na viongozi mbalimbali wa chama hicho wako mkoani hapa, wakisubiri waanza mikutano yao ya vugugugu la mabadiliko walilolipa jina la M4C baada ya kuzuiwa na jeshi la Polisi kufanya mikutano yao katika kipindi chote cha sensa.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs