HUSEIN BASHE & KIGWANGALA WADAIWA KUTISHIANA BASTOLA


VITA ya mahasimu wa siku nyingi katika siasa wilayani Nzega, Hussein Bashe na Dk Hamis Kigwangallah imechukua sura mpya, baada ya makada hao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufikia hatua ya kutishiana kwa bastola hadharani.Hata hivyo, pamoja na taarifa hizo kuthibitishwa na viongozi wa CCM wilayani humo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Bashe na Kigwangallah kwa nyakati tofauti kila mmoja amekanusha madai hayo akimtuhumu mwenzake kuwa ndiye aliyekuwa na silaha.

Wakati Bashe akisema Dk Kigwangallah ambaye pia ni mbunge wa Nzega ndiye aliyetoa bastola kumstishia wakiwa ndani ya ofisi ya ya CCM Wilaya, Dk Kigwangallah anaeleza kuwa walinzi wa Bashe ndio waliomtishia yeye bastola na kwamba tayari amelifikisha suala hilo polisi ambao wanalifanyia kazi


Dk Kigwangallah na Bashe walizua tafrani hiyo juzi wakati wakirejesha fomu za kuwania nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia Wilaya ya Nzega.
Upinzani baina ya wanasiasa hao vijana, ulianza 2010 baada ya Kigwangallah kupitishwa na CCM kugombea ubunge katika jimbo hilo licha ya kushika nafasi ya tatu katika kura za maoni, ndani ya chama hicho.

Bashe ambaye aliibuka kidedea katika mchakato huo wa kura za maoni alitoswa na chama hicho kwa maelezo kuwa hakuwa raia wa Tanzania, huku aliyeshika nafasi ya pili, Lucas Selelii ambaye alikuwa kinara wa kupambana na mafisadi wa chama hicho naye akitoswa. Baadaye Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Lawrence Masha alisema Bashe alikuwa raia halali wa Tanzania. Vita hiyo ilionekana kuendelea juzi baada ya kudaiwa kutishiana bastola huku kila mmoja akitoa maelezo ya kumrushia lawama mwenzake.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs