Dr.Slaa & Sitta Wazidi Kulushiana Maneno


MALUMBANO ya kisiasa baina ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa yameendelea safari hii waziri huyo akisema, Chadema ni dhaifu hakina watu makini ndiyo maana kinahangaika kusaka watu wa kushika nafasi za juu hasa urais inapofika nyakati za uchaguzi.

Kauli hiyo ya Sitta imekuja ikiwa ni siku zisizozidi sita, baada ya kusema kuwa Chadema kina mtu mmoja tu mwenye sifa za kuwania urais, ambaye Dk Slaa huku akidai kwamba Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ana sifa za kuendesha vitega uchumi vya burudani na kumbi za starehe. Lakini baada ya kauli hiyo, Dk Slaa aliitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini Iringa na kusema kuwa Sitta ni mnafiki, mwongo na msaliti na asiyefaa kuongoza umma wa Watanzania.

Jana, Sita alitoa taarifa kwenye vyombo vya habari kuhusu madai hayo ya Dk Slaa akisema: “Dk Slaa ni dikteta. Hana uvumilivu. Ana hulka ya kujisikia kwamba mawazo yake hayapingwi. Ni mzushi asiyeogopa kusema na kupindisha mantiki ya jambo ili tu kushinda hoja. Iweje mtu aliyenibembeleza nigombee uraisi kupitia chama chake mwaka juzi, leo aseme sifai kuongoza hata kata kwa sababu tu nimetamka ukweli juu ya udhaifu wa chama chake cha siasa?” Awali, Sita alikaririwa akizungumza katika Kituo cha Redio One jana asubuhi kuwa chama hicho kama kingekuwa na watu wenye sifa za kushika dola, wasingethubutu kutafuta watu akiwamo yeye ili kuwania urais kwa tiketi ya chama chao.
“Ni kweli kabisa Chadema walinifuata na kuanza kunishawishi kuwania urais kwa tiketi ya chama chao, wakanipa miongozo yao ya chama, nikaisoma nikaona hakuna kitu, nikaamua kubakia kwenye chama changu.” “Kama kingekuwa na watu makini wasingekuwa na sababu ya kuhangaika kutafuta watu waje kwenye chama chao, hiyo ina maana kuwa ndani ya Chadema hakuna watu na wanafanya kazi ya kuja CCM kutafuta watu kwa ajili ya nafasi za juu,” alisema Sitta. Alijigamba kwamba yeye ni kiongozi makini, mtu wa watu na anakubalika katika mapambano ya ufisadi na ndiyo maana Chadema walimfuata kumshawishi kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2010.

Kuhusu madai kwamba alikuwa mmoja wa waasisi wa Chama Cha Jamii (CCJ), Sitta ameendelea kukanusha kuwa si mwasisi wake akisema, chama hicho pamoja na Chadema walimfuata kwa ajili ya kujiunga nao kwa nafasi ya urais kwa uchaguzi wa 2010, lakini akaona sera zao hazitoshi ndiyo maana akaamua kubaki CCM... “Walikuja CCJ, walikuja Chadema, wote hao waliniona mimi ni mtu wa watu, lakini sera zao hazina uzito...” Dk Slaa alikiri kumfuata Waziri Sitta kwa kuwa alikuwa anakubalika, mpambanaji dhidi ya mafisadi na mtetezi wa watu wa kawaida. Lakini baada ya kukataa hawakuwa na mpango naye tena na kuendelea na michakato mingine. Hata hivyo, Dk Slaa hivi karibuni alisema kuwa Sitta anauhadaa umma wa Watanzania kuwa hakuwahi kufikiria wala kutaka kujiunga na upinzani, kwani waliwahi kukaa meza moja kujadili jinsi gani ya kuweka mikakati ya kuimarisha ngome ya upinzani.

“Mimi nina ushahidi wa kila kitu, Sitta akanushe kama hakuwahi kuwa kwenye mchakato wa kuanzisha CCJ, mimi na yeye pamoja na Mbowe tuliwahi kukaa meza moja kufanya haya, lakini namshangaa leo anakanusha...” alisema.

Mgeja ampongeza Dk Slaa kumshukia Sitta
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja amesema kitendo kilichofanywa na Dk Slaa dhidi ya Sitta ni kizuri kwa kuwa kimeonyesha jinsi gani waziri huyo alivyokisaliti chama hicho.

Alisema kutokana na hilo, ni muhimu CCM ikawatosa watu wa aina hiyo kwa kuwa kusaliti chama ni kosa kubwa. Akizungumza na waandishi wa habari Mwanza jana, Mwenyekiti huyo alimpongeza Dk Slaa na kudai kuwa kauli aliyoitoa ni msaada mkubwa kwa chama chake kwa vile inafunua usaliti ambao Sitta aliutenda. “Ukweli mimi binafsi ninatofautiana na Dk Slaa kwa masuala mengine ya kiitikadi, lakini kwa hili la kumwelezea Sitta ninampongeza na kumuunga mkono, ameeleza mambo ambayo chama chetu kinapaswa kuyafuatilia na kuyafanyia kazi,” alisema Mgeja.

Alisema ameamua kumpongeza Dk Slaa kutokana na kuanika ukweli wa mambo yaliyo nyuma ya Sitta na kubainisha kuwa alikuwa akitumia ofisi yake ya uspika kukihujumu CCM. Mgeja alisema ameamua kutoa kauli hiyo kutimiza moja ya ahadi za mwanachama wa CCM inayosema: “Nitasema ukweli daima na fitina kwangu mwiko” na kusema yupo tayari kwa lolote kutokana na kauli hiyo hata kama chama chake kitamtosa kwa kutoa kauli ya kumpongeza Dk Slaa.
Source: MCL


TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs