Mh. Sumaye awaonya Polisi


WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuacha kutumia silaha za moto au nguvu ya ziada linapokabiliana na raia, badala yake litumie busara kutatua migogoro.Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro, baada ya kufunga mafunzo wa wahariri wa vyombo vya habari yaliyohusu utawala, Sumaye alisema kufa mtu katika mapambano ya polisi na raia siyo kitu kidogo.

Kauli hiyo ya Sumaye inaonekana kuwalenga polisi ambao wanadaiwa kusababisha kifo cha aliyekuwa mwandishi wa habari wa Televisheni ya Channel Ten mkoani Iringa, David Mwangosi. Mwandishi huyo aliuawa Jumapili iliyopita katika Kijiji cha Nyololo, Iringa kwa kulipuliwa na kitu kinachodhaniwa kuwa bomu, wakati polisi walipokuwa wakiwazuia viongozi na wanachama wa Chadema kukusanyika wakati wakifungua tawi la chama hicho kijijini hapo.

Mheshimiwa Sumaye alisema kuwa katika siku za karibuni, polisi wamekuwa wakikimbizana na raia mara kwa mara pamoja na kutumia silaha na nguvu isiyo ya kawaida hata pale pasipostahili. Jambo ambalo alisema siyo sahihi kwa mustakabali wa jeshi hilo.

“Si lazima sana kwa polisi kutumia silaha hasa za moto kila wakati. Nimekuwa nikitazama kwenye televisheni mara kwa mara na kuona polisi wakitumia silaha, hata sehemu za kuvunja nyumba tu huko vijijini. Nawashauri watumie busara,” alisema Sumaye na kuongeza:

“Tusidhani risasi inaweza kutatua migogoro wakati wote. Risasi inaweza kuharibu kila kitu, zitumike pale inapokuwa ni lazima kwani Watanzania siku zote si watu wa fujo.”

Alisema kutokana na tukio la hivi karibuni la kuuawa kwa mwandishi wa habari, Serikali, Polisi na vyombo vingine vya usalama, watakuwa wamejifunza kitu katika kutatua migogoro na migongano baina yao na wananchi wanaowaongoza.

Alisema kwamba Jeshi la Polisi nchini linapaswa kutambua kuwa matumizi ya nguvu kupita kiasi ikiwa ni pamoja na kutumia risasi kutawanya raia, si suluhisho la migogoro baina yake na wananchi, bali kinachohitajika ni busara zaidi, ili kuepusha maafa.

Akizungumzia suala la polisi kupambana na wanasiasa alisema, mazingira ya siasa kwa sasa yamechangamka zaidi ikilinganishwa na yale ya zamani na kwamba wakati mwingine wanasiasa wamekuwa wakichangia vurugu na hivyo kulilazimisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu ya ziada.

“Sisi wanasiasa tusiwe kichocheo cha kuleta vurugu na badala yake tutumie njia za kistaarabu na si kuchokoza vyombo vya usalama. Kinachotakiwa busara zitumike pande zote, vinginevyo tutaendelea kuumiza watu,” alisema.

Kuhusu uhusiano baina ya Serikali na waandishi wa habari, Sumaye alisema kinachoathiri hali hiyo katika nchi za Afrika ni kutokana na baadhi ya Serikali kutotaka mambo yake yawe wazi. Alisema katika mazingira mengi hata pale unapokuwapo uhusiano huo unakuwa wa kinafiki usioleta tija kwa pande zote.

Alisema iwe ni polisi na wananchi au polisi na waandishi, busara zitumike zaidi badala ya nguvu katika kutafuta suluhisho kwani siku zote mapambano hayatatui na badala yake, yanaweza kuharibu kabisa amani iliyopo. Akifunga mafunzo hayo ya siku nne yaliyohusu utawala, Sumaye alisema vyombo vya habari ni sehemu ya maisha ya kila siku katika jamii kwa kuwa vina habarisha mambo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Alisema vinatoa taarifa ya nini Serikali zinawafanyia watu wake na nini hazifanyi ili wananchi waweze kudai haki zao na hata kuikumbusha wajibu wake pale inapojisahau. Muda mwingine vyombo vya habari vimekuwa kisu kikali kwa sababu si Serikali zote zinazopenda kukosolewa, kukumbushwa na kupewa changamoto kwa yale zilizoyafanya na zinayopaswa kuwafanyia wananchi wake.

“Vyombo vya habari ni kama kioo tunachojitazama kila asubuhi kabla kutoka nyumbani kwenda ofisini au kuhudhuria mikutano muhimu, ili kujua kama umevaa uhusika wa kile unachokwenda kukifanya au kukizungumza mbele ya jamii. Huwezi kuvunja kioo kama kitakuonyesha kitu ambacho huhitaji kukiona kwenye mwonekano wako.

Hivyo si sahihi kuvilaumu au kuviadhibu vyombo vya habari pale vinapokosoa na badala yake ni kujirekebisha,” alisema Sumaye.

Watuhumiwa wa mauaji ya Iringa
Katika hatua nyingine askari watano wanaoshikiliwa Iringa wanaendelea kuhojiwa, huku taarifa zikieleza kuwa wanaweza kufikishwa mahakamani Jumatatu, kutokana na kushindikana jana. Jana, taarifa zilisambaa kwamba askari hao walikuwa wafikishwe katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, lakini hadi jioni, walikuwa hawajafikishwa. Pia hakukuwa na taarifa zozote za nini kilikuwa kinaendelea.

“Ni kweli walitakiwa wafikishwe leo, lakini hadi sasa hawajafika, wakifika nitawaeleza,” alisema mmoja wa wafanyakazi wa mahakama hiyo jana.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda hakutaka kueleza lini watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa kile alichosema kwamba kwa sasa yeye siyo msemaji wa jambo hilo.

“Hapa alikuja IGP (Said Mwema), na sasa yuko DCI (Robert Manumba). Kwa mazingira haya uhuru wangu wa kuzungumza uko limited, (una kikomo),” alisema.

Alipoulizwa watuhumiwa hao wako mahabusu ipi, alihoji... “Wapi?” Aliendelea kusema, “Nashindwa kusema wapo au hawapo kwa kuwa mimi siyo msemaji wa jambo hilo, ila nawashauri m-cross-check (kuthibitisha), vizuri vyanzo vyenu vya habari.”
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs