Wasiwasi wa mikopo wakumba wanafunzi vyuo vikuu

BongoNewz
Wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini, wako hatarini kuchelewa kupata fedha za mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutokana na mchakato wa kutoa mikopo hiyo kuchelewa kuanza.

Hali hiyo inatokana na vyuo hivyo kuanza kufunguliwa mwishoni mwa mwezi huu na mwanzoni mwa mwezi ujao.

Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini kuwa wanafunzi katika vyuo hivyo walioomba mikopo toka HESLB, bado hawajaanza kupata hatua ambayo imeanza kuwapa shaka kama wataripoti vyuoni kwa wakati kutokana na kutegemea fedha za mikopo kwa ajili ya ada ya masomo na mahitaji mengine.

Kutokana na ucheleweshaji wa mikopo hiyo, gazeti hili lilishudia wanafunzi kadhaa ambao wamedahiliwa kujiunga vyuo vya elimu ya juu mwaka huu, wakimiminika katika ofisi za HESLB makao makuu jijini Dar es Salaam kuulizia hatma ya mikopo waliyoomba.

“Unavyoniona hapa ni wiki ya tatu nimekuwa nikija hapa ofisi za Bodi ya Mikopo kuulizia kama mikopo imeanza kutolewa, lakini tunaelezwa tuendelee kusubiri wakati vyuo vimekaribia kufunguliwa,” alisema mwanafunzi mmoja aliyetoka Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro.

Hata hivyo, Afisa mmoja wa HESLB, aliyejitambulisha kwa jina moja la Venelanda, alisema mchakato wa kuandaa mikopo ya wanafunzi bado unaendelea na kwamba zoezi hilo linachukua muda kidogo kutokana na mikopo hadi kukamilika kwake hupitia maeneo mengi.

Venelanda ambaye hata hivyo, hakutoa jibu la moja kwa moja kama mikopo kwa wanafunzi hao itaanza kutolewa lini, alisema HESLB itahakikisha mikopo hiyo inatolewa kwa wanafunzi hao kabla ya kufunguliwa vyuo hivyo.

Mkuu wa Idara ya Habari Wizara ya Fedha, Ingiahedi Mduma, alipoulizwa na gazeti hili kama fedha za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu zimeshapelekwa HESLB, alisema suala hilo waulizwe Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

“Bajeti ikishapitishwa bungeni, kinachobakia ni kwa wizara husika kushughulikia mipango yake, hivyo hata suala la fedha za mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu wenye majibu ni Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,” alisema Mduma.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Phillipo Mulugo, alipoulizwa na NIPASHE, alisema kimsingi mikopo bado haijaanza kutolewa kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na kufafanua kuwa kuanzia wiki hii wizara yake itaangalia uwezekano wa kushughulikia suala hilo ili wahusika wapewe mikopo hiyo.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Bhokombe Itembe, alisema wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanatarajia kuripoti chuoni hapo Oktoba Mosi, mwaka huu.

Alisema wiki iliyopita uongozi wa chuo na Daruso, walitaka kupanga vyumba katika hosteli kwa ajili ya wanafunzi, lakini zoezi hilo lilishindikana kwa sababu bado haijafahamika idadi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza watakaoripoti chuoni hapo.

Itembe alisema tatizo la kuchelewa kwa mikopo linatokana na sababu kadhaa, ikiwemo kutokuwepo kwa ushirikiano kati ya HESLB na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

“Mwanafunzi anapodahiliwa bila TCU kumuamulia ataenda chuo gani, huwezi kwenda na wakati huo huo bila HESLB kukupatia mkopo, vile vile huwezi kwenda chuoni,” alisema Itembe.

Rais wa Chuo Kikuu cha Usimamizi wa Fedha IFM, Michael Chazy, alisema chuo hicho kitafunguliwa Oktoba 8, mwaka huu na kwamba hadi sasa bado wanafunzi wanaoendelea na wale wa mwaka wa kwanza hawajaanza kupatiwa mikopo.

Naye Rais wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Paul Yunge, alisema suala la mikopo katika chuo lina utata hasa kwa wanafunzi wanaoanza mwaka wa kwanza ambapo baadhi yao wamejaza fomu vibaya na hivyo taasisi husika zinashughulikia tatizo hilo.

Rais wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Amos Chakushemeire, alisema utoaji wa mikopo hauridhishi kabisa katika chuo hicho ambapo wanafunzi walioanza muhula Julai, mwaka huu, wamelipwa robo ya mkopo wakati kiasi kingine cha mkopo hawajalipwa hadi sasa, hali ambayo imesababisha ukata mkubwa kwa wanafunzi.

“Chuo chetu ni tofauti na vingine, kina mihula mitatu, wanafunzi walioanza muhula wa Julai hawajalipwa sehemu nyingine,. Hivi karibuni uongozi wa chuo ulilazimika kuwakopesha Sh. 50,000 wanachuo hao ili kuwatuliza wasigome,” alisema Chakushemeire.

Rais wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Frank Nkinda, alisema mikopo ni changamoto kubwa katika chuo hicho ambapo wanafunzi wa mwaka wa kwanza hawajapata mikopo hadi sasa.

Alisema kutokana na hali hiyo, hivi karibu Mwenyekiti wa HESLB alifika chuoni hapo kuzungumza na uongozi, serikali ya wanafunzi na wanachuo ambapo alitoa ahadi kutoa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika mwaka huu wa 2012/2013.

Mwaka jana serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilitangaza utaratibu mpya wa utoaji wa mikopo ambapo badala ya fedha hizo kutolewa kwa waombaji na HESLB, sasa fedha hizo zinapelekwa vyuoni ambako menejimenti za vyuo zinawajibika kuzisimamia na kuwapa waombaji.

Hatua hiyo ilifikiwa ili kurahisisha mchakato wa kuwapatia fedha waombaji na pia kuepusha usumbufu kwa HESLB kutokana na wanafunzi kutoka vyuoni kuvamia ofisi hizo kwa lengo la kushinikiza wapewe fedha.

Taarifa iliyotolewa na HESLB na TCU Agosti 10 na 12, mwaka huu ilieleza kuwa zaidi ya wanafunzi 3,074 walioomba mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2012/13, wameenguliwa katika maombi yao kutokana na dosari mbalimbali.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa HESLB pekee iliorodhesha zaidi ya wanafunzi 2,649 ambao ilibaini kuwa na mapungufu kadhaa katika maombi yao ya kupewa mikopo.
Miongoni mwa makosa ama dosari ambazo HESLB ilizibaini kwa walioenguliwa ni pamoja na kukosekana kwa vyeti vya kuzaliwa kwa muombaji, sahihi ya mdhamini/muombaji, kukosekana kwa picha ndogo ya muombaji/mdhamini, kukosekana kwa sahihi za viongozi wa serikali za mitaa/vijiji kwa waombaji na nyaraka nyingine muhimu kwa waombaji.

Kwa upande wake TCU, iliwaengua jumla ya waombaji 425 kwa dosari na makosa mbalimbali.

Miongoni mwa dosari ambazo zilitajwa na TCU ni pamoja na baadhi yao kukosea namba za vyeti vya masomo kwa vidato vya nne na tano, miaka ya kumaliza masomo, mawasiliano sahihi kwa muombaji pamoja na uchaguzi wa masomo.

Hata hivyo, taasisi hizo mbili zimetoa muda kwa walioenguliwa sasa kutokana na dosari hizo kurekebisha na kutuma tena maombi yao kupitia mitandao kwa mujibu wa maelekezo waliyotoa.

Kwa mwaka huu wa fedha 2012/13, serikali imeiongezea fedha HESLB kwa kuitengea Sh. bilioni 326 kwa wanafunzi 98,772.

Mwaka jana, serikali iliitengea HESLB Sh. 91,722,783,264 kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Ucheleweshaji wa fedha za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu umekuwa ukisababisha wafanye migomo, vurugu na maandamano mara kwa mara kushinikiza walipwe.

SOURCE: NIPASHE
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs