CHADEMA YAMTAKA MAKINDA ATOE RIPOTI YA TUME YA RUSHWA ZA WABUNGE

BongoNewz
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemtaka Spika wa Bunge, Anne Makinda atoe hadharani ripoti ya uchunguzi inayowahusisha baadhi ya wabunge kujihusisha na rushwa ili iweze kujadiliwa.Wakati wa Bunge la Bajeti, Spika wa Bunge aliunda Kamati ya Bunge ili kuchunguza tuhuma za rushwa zinazowakabili wabunge kadhaa ikiongozwa na Mbunge wa Mlali (CCM), Hassan Ngwilizi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara, katika Uwanja wa Michezo Karatu, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe alisema wamepata taarifa kuwa tayari kamati hiyo imemaliza kazi lakini kuna mpango wa kutoipeleka kwenye Bunge zima.

“Tumepata taarifa kuwa kuna mpango wa kuipeleka taarifa ya Ngwilizi kwenye kamati ya Uongozi ya Bunge, Chadema hatukubali, tunataka taarifa hiyo ipelekwe kwa Bunge zima na tuitolee maazimio,” alisema Zitto huku akishangiliwa na umati wa watu waliohudhuria mkutano huo.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alisema wabunge wote ambao wametajwa kuhusika katika taarifa hiyo ya Bunge wanapaswa kuwajibishwa, kwani haiwezekani kila siku Watanzania kusoma habari za ufisadi na watuhumiwa hawachukuliwi hatua.
“Tunataka taifa zima lijue kilichotokea kwa wabunge wao, hivyo Chadema hatutakaa kimya, tunataka taarifa iwe wazi,” alisema Zitto.

Alisema ni aibu viongozi wa kitaifa kila siku kulalamika taifa ni maskini, wakati nchi ina rasilimali nyingi ambazo zinafaa kuwakomboa Watanzania kujiondoa katika umaskini.
“Watu wanazalisha tani hadi 50 za dhahabu, halafu tunaambiwa taifa ni maskini, hapana tuna tatizo la viongozi wetu, taifa hili linapaswa kuwa tajiri,” alisema Zitto.

Hivi karibuni Mbunge Ngwilizi alikaririwa akisema kuwa kamati yake imekamilisha ripoti yake na kwamba imeikabidhi kwa Spika wa Bunge kwa hatua zaidi.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya kamati hiyo zinaeleza kuwa ripoti hiyo imewatia hatiani baadhi ya wabunge waliokuwa wakituhumiwa kuhusika katika kashfa ya kuikwamisha kwa njia ya rushwa, Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, Raia Mwema.

Fedha zilizofichwa Uswis
Kuhusu fedha zilizofichwa Uswis na baadhi ya watu nchini, Zitto alisema wanaiomba Serikali izirejeshe fedha hizo na kwamba Chadema inapanga kupeleka bungeni azimio la kuomba taarifa rasmi juu ya fedha hizo.
Alisema kati ya hizo wamebaini kuna ofisa mmoja mkuu wa jeshi mstaafu anamiliki zaidi ya Sh50 bilioni, hivyo Chadema inataka fedha zote kurejeshwa.

Lissu aonya Katiba Mpya
Naye Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu alionyesha wasiwasi kwa Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba Mpya inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba kuwa inaweza kuhujumiwa na CCM.
Alisema ni vyema wananchi wakajitokeza kutoa maoni yao kwa wingi kwani katiba inahitaji kuwatumikia wananchi na siyo Katiba ya sasa.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs