Tanzania yasaini kupokea Bilioni 352/- (EURO 176) kutoka Ujerumani
Waziri
wa Fedha Dkt. William Mgimwa (kushoto) na Balozi wa Ujerumani nchini
Kluas Peter Brandes (kulia) wakisaini mkataba wa msaada wa miaka mitatu
leo mjini Dar es Salaam ambapo Ujerumani itaipatia Tanzania msaada wa
Shilingi bilioni 352. Msaada huo utasaidia kuboresha utawala bora katika
serikali za mitaa, sekta ya afya , nishati , maliasili, maji, mfuko wa
bajeti ya Serikali na kuboresha programu ya usimamizi wa fedha za umma.
Habari imeandikwa na Tiganya Vincent-MAELEZO-Dar Salaam
Ujerumani imetoa jumla ya shilingi bilioni 352( euro milioni 176) kwa
Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo
katika kipindi miaka mitatu ijayo.
Makubaliano ya msaada huo yamesaini leo jijini na Waziri wa Fedha Dr.
William Mgimwa kwa upande wa Tanzania na Balozi wa Ujerumani nchini
Kluas Peter Brandes.
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo kwa niaba ya Tanzania
Waziri wa Fedha dr. Mgimwa alisema kuwa fedha hizo zitasaidia shughuli
mbali za maendeleo katika kipindi cha mwaka 2012/13- hadi 2014/15.
Alisema kuwa msaada huo unalenga maeneo ya kuboresha utawala bora katika
serikali za mitaa, kusaidia sekta ya afya , nishati , maliasili, maji,
na kuboresha programu ya usimamizi wa fedha za umma.
Dr. Mgimwa aliongeza kuwa eneo jingine ambapo hizo zitaelekezwa ni
pamoja na kusaidia mfuko wa bajeti kwa kipindi miaka mitatu hiyo na
kusaidia ofisi ya Taifa ya Mkaguzi wa hesabu za serikali .
Alisema kuwa miradi hiyo itasaidia kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kukuza
Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA) na hivyo kuboresha hali ya
uchumi na kijamii ya wananchi.
Aidha Waziri huyo wa Fedha alimuhakikisha Balozi wa Ujerumani nchini
kuwa , Serikali itahakikisha fedha za msaada zinatuma katika maeneo
yalipangwa kwa manufaa ya wananchi ili matokeo yake yaweze kuonyesha
thamani ya fedha waliyotoa.
Naye Balozi Brandes alisema kuwa Nchi yake itaendelea kuimarisha
ushirikiano wa muda mrefu na Tanzania ili kufikia malengo ya kupambana
na umaskini na hivyo kuboresha maisha ya Watanzania hasa waishio
vijijini.
Aliongeza kuwa msaada waliotoa utasaidia wakazi wa mijini kupata maji
safi na salama kwa ajili ya kujikinga na magonjwa yatokanayo na maji
yasiyo salama.
Waziri
wa Fedha Dkt. William Mgimwa (kushoto) na Balozi wa Ujerumani nchini
Klaus Peter Brandes (kulia) wakibadilishana hati za makubaliano ya
mkataba wa msaada wa miaka mitatu leo mjini Dar es Salaam.
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII