VIGOGO WA BANDARI WALIOKWEPA KUHOJIWA NA WAKABIDHIWA KWA MWAKYEMBE
BONGONEWZ BLOG

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, amekabidhiwa ripoti ya
uchunguzi wa utendaji kazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), huku
akitoa onyo kali kwa vigogo waliokwepa kuhojiwa na kamati kwa visingizio
mbalimbali akisema ni lazima watahojiwa tu. Dk. Mwakyembe alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kukabidhiwa
ripoti hiyo yenye kurasa 285 na Mwenyekiti, Wakili Benard Mbakileki, na
kuongeza kuwa kama suala analotaka kuhojiwa mhusika linahusu polisi,
atapelekwa mbele ya jeshi hilo.
Waziri Mwakyembe alitoa kauli hiyo baada ya Wakili Mbakileki kueleza
kuwa baadhi ya watu muhimu TPA waliotakiwa kuhojiwa walikwepa kwa
visingizio mbalimbali ikiwamo kuuguliwa, kufiwa na wengine kuzima simu
kabisa. Akijibu hoja hiyo, Dk. Mwakyembe alisema: “Kama walidhani kukwepa
kamati ndio mambo yameisha, wanajidanganya. Watakuja kujibu mbele yangu
na kama mambo yanahusu polisi tutawapeleka, hatutaacha mtu.” Aliongeza kuwa kamati hiyo imefanya kazi ya kizalendo na kuahidi
mambo yote iliyopendekeza watayafanyia kazi hatua kwa hatua, ili
kuboresha bandari hiyo.
“Niwahakikishie hii kazi mliyoifanya haitakwenda bure, hadi kufikia
Desemba mwaka huu, tutakuwa tumeyafanyia kazi mambo yote mliyopendekeza.
Tutataka kuipa bandari sura mpya, kwa sasa inakosa ufanisi…tutakuja na
uamuzi ambao hakitadokolewa kitu, kwani watakaodokoa, nao watadokolewa,
kwani tusipofanya uamuzi huo hatutaikomboa nchi yetu,” alisema.
“Tulikuwa tunasikia habari za Twiga kusafirishwa kwenye ndege watu
wakashangaa, lakini pale bandarini kontena na ukubwa wake linayeyuka.
Mwaka juzi yaliyeyuka makontena 10, mwaka jana 26 na mwaka huu mawili na
mambo yanatufanya tusiaminike,” alisema. Waziri Mwakyembe alibainisha kuwa kutokana na hali hiyo, watafanya
kazi kwa gharama yoyote, bila kumwonea mtu, ili kurekebisha bandari hiyo
aliyoeleza kuwa iwapo ingesimamiwa vizuri nchi ingeweza kuendesha mambo
mengi.
Aidha, alibainisha kuwa tangu kamati hiyo ilipoanza kufanya kazi,
baadhi ya nchi jirani zimeanza kurejesha imani na bandari hiyo zilikemo
Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Rwanda na Burundi.
Aliongeza kuwa iwapo baadhi ya watu wanakerwa na mabadiliko ndani ya TPA, waondoke kwani mjini kuna kazi nyingi za kufanya. Pamoja na mambo mengine, Mwakyembe aliomba wapatiwe muda wa kuipitia
ripoti hiyo kwa umakini na kwamba kila hatua watakuwa wakitoa taarifa
kwa umma.
Kamati yanena
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbakileki, alisema katika kutekeleza
uchunguzi waliwahoji watu 116 wakiwamo baadhi ya wajumbe wa Bodi na
Wafanyakazi wa TPA pamoja na uongozi wa Vyama vya Wanyakazi (Dowuta),
Mamlaka ya Mapato (TRA) Makao Makuu na kuonana na Kamishna Mkuu.
“Pia tulionana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA) na
maofisa wengine, eneo la Upakuaji na Upakiaji Mafuta (KOJ), Ticts na
kuonana na Meneja Mkuu na maofisa wengine pia kujionea utendaji kazi.
“Polisi Chang’ombe tulikutana na Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Temeke,
Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Temeke na maofisa wengine, kuzungumzia
kukamatwa kwa magari yanayobeba mafuta machafu bandarini pamoja na
jaribio la wizi wa kompyuta lililofanywa katika kituo cha WMA bandari
kwa lengo ovu la kupoteza ushahidi,” alisema.
Alieleza kuwa wadau wengi walijitokeza bila kutarajia, wengi wao
wakiwa na hamu ya kurudia mara mbili na pia mahojiano kwa mtu yalichukua
muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa ambapo mtu mmoja alihojiwa kati ya
dakika 50 hadi 180, hali iliyochangia mahojiano kufanyika hadi saa sita
usiku.
Pia alieleza kuwa walipitia nyaraka mbalimbali zikiwemo sheria
mbalimbali au Katiba ya nchi, Sheria ya TPA, sheria ya Mashirika ya Umma
na mikataba mbalimbali. Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni Ramo Makani (Makamu Mwenyekiti),
John Wanga, Halima Mamuya, Saidi Sauko, Richard Kasesela na Bernardina
Mwijarabu.
Alisema katika utendaji wao kazi walisimamia nguzo moja kuwa ‘Ukweli
na haki ndio utakaotuweka huru’ katika kulinda na kuendeleza rasilimali
muhimu kwa maendeleo ya taifa. Agosti 23, mwaka huu, Mwakyembe alitangaza kumsimamisha kazi
Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraim Mgawe, na viongozi wengine watatu, ili
kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za ufisadi zinazowakabili. Nafasi
ya Mgawe kwa sasa inakaimiwa na Madeni Kipande kutoka Wizara ya Ujenzi.
Mbali ya Mgawe, vigogo wengine waliosimamishwa kazi ni wasaidizi wake
wawili, Julius Mfuko na Hamad Koshuma pamoja na Meneja wa Bandari ya
Dar es Salaam, Casian Nghamilo.
Baada ya kuwasimamisha viongozi hao, waziri huyo aliunda kamati hiyo
na kuipa hoja 34 ambazo ziliundiwa hadidu za rejea tisa, ili kuchunguza
chanzo cha kuzorota huduma TPA, hali inayochangia kukimbiwa na wateja wa
ndani na nje ya nchi.

0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII