PRECISION AIR YAZINDUA NDEGE YAKE MPYA AINA YA ATR 42-600
Waziri wa Uchukuzi (wa tatu pichani) kutoka kulia,Mh.Dkt Harisson Mwakyembe akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wakuu wa Shirika la Ndege la Precision,wakati wa uzinduzi wa ndege yao mpya aina ya ATR 42-600.
Waziri wa Uchukuzi (wa tatu pichani) kutoka kulia,Mh.Dkt Harisson Mwakyembe akikata keki kuashiria uzinduzi wa ndege yao mpya aina ya ATR 42-600la fu,kwenye hafla fupi iliyofanyika jijini dar,kulia kwake ni Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika hilo, Michael Shirima na shoto kwake ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Alfonse Kioko kwa pamoja wakishuhudia tukio hilo adhimu.
Baadhi ya wadau mbalimbali walioshiriki uzinduzi wa ndege hiyo mpya aina ya ATR 42-600 wakiipanda.
======= ======== ========
Shirika la Ndege la Precision limezindua
ndege yake mpya aina ya ATR 42-600,
ikiwa ni hatua ya mwendelezo wa maboresho ya miundombinu ya shirika hilo kwa
maslahi ya wateja wake. Hata hivyo uzinduzi huu
ni sehemu tu ya mkakati wa miaka mitatu, ambapo katika kipindi hicho, shirika
limepanga kuongeza aina kama hii ya ndege za (ATR) hadi kufikia idadi ya ndege
5, mradi utakaogharimu kiasi cha Dola milioni 95.
Mwenyekiti wa Bodi wa
Shirika hilo, Michael Shirima, alipongeza hatua ya uzinduzi huo, ambapo alisema
itasaidia kwa kiasi kikubwa kuleta mapinduzi katika sekta ya usafirishaji wa
anga. “Ndege hii mpya na ya kisasa ya ATR 42 - 600 ina zaidi
ya viwango vinavyohitajika katika huduma ya usafiri wa anga, ina muundo wa
kipekee uliotengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu, na inaweza kufanya huduma zake hata kwenye
maeneo ya miundombinu duni,” alisema Shirima.
Katika mwendelezo wa
uboreshaji wa huduma zake, Precision imeendelea kupeleka ndege zake ndogo
mikoani na kuahidi kuendeleza azma yake ya kuwa kitovu cha utoaji wa huduma
bora za anga nchini.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika hilo, Alfonse Kioko, alisema upanuzi wa wigo wa huduma za
anga katika shirika hilo, ni miongoni mwa mikakati ya kuhakikisha wateja wake
wanafurahia ufanisi na huduma za usafiri huo,
sanjari na kupunguza adha na usumbufu kwa wateja . “Ni fahari kubwa kwa
Tanzania kupitia shirika la ndege la Precision kuwa taifa la kwanza katika bara
la Afrika kuingiza ndege hii ya kisasa na iliyotengenezwa kwa teknolojia ya hali
ya juu,”alisema Kioko.
“ATR 42-600 inakidhi
matakwa na mazingira ya ukuaji wa miundombinu katika maeneo mengi barani Africa
jambo ambalo linatupa hamasa ya kuongeza masafa na uboreshaji wa huduma zetu
katika hali ya ufanisi zaidi.” Precision Air ina wigo
mpana na imejiimarisha zaidi katika kuhakikisha inafikisha huduma zake katika
mikoa yote. Shirika hilo ni la kwanza kati ya mengi yaliyopo nchini,
kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam, DSE.
Aina hiyo ya ndege
itasaidia kupanua wigo wa usafiri wa anga unaofanywa ndani ya shirika hilo kwa
safari za ndani na nje ya Tanzania. Hata hivyo shirika liko mbioni kuanzisha
safari zake katika mikoa inayokua kwa kasi kama Mtwara.
“Maeneo mengine
tunayoyatazama ni mkoa wa Mbeya punde tu uwanja wake mpya utakapozinduliwa
mwakani, Bukoba na Kigoma ambapo viwanja vyake bado vipo kwenye matengenezo.”
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII