WAGOMBEA URAIS KENYA KUFANYA MDAHALO LEO SAA MOJA....UTARUSHWA LIVE CHANNEL 10


MDAHALO mkubwa wa wagombea Urais nchini Kenya unafanyika leo na hapa nchini utaonyeshwa moja kwa moja kupitia Kituo cha Channel 10, kwa kushirikiana na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).
MCL ndio inayomiliki gazeti hili pamoja na yale ya Mwananchi Jumapili, Mwanaspoti, Citizen na Citizen on Sunday.
Watakaoshiriki katika mdahalo huo ni wagombea wa Urais wa nchi hiyo, Raila Odinga, Uhuru Kenyatta, Musalia Mudavadi,  Peter Kenneth, James Kiyiapi, na Martha Karua.
Mdahalo huo utafanyika katika Ukumbi wa Shule ya Kimataifa ya Brookhouse jijini Nairobi kuanzia saa moja usiku.
Mada kubwa zitakazongumziwa ni pamoja na usalama,huduma za kijamii (elimu na afya) na usimamizi wa rasilimali.
Wagombea hao watapata fursa ya kumwaga sera na kujitengenezea mazingira mazuri kabla ya uchaguzi utakaofanyika Machi 4, 2013 mwaka huu.
Uchaguzi huo unaotazamiwa kuwawa  kihistoria, utasimamiwa kwa mara ya kwanza na Tume Huru ya Uchaguzi ya Kenya (IEBC).
Mkurugenzi wa Kamati ya Maandalizi ya Mdahalo huo, Francis Munywoki alisema wamepanga kuandaa midahalo miwili kabla ya uchaguzi huo.
Munywoki alisema mdahalo wa pili umepangwa kufanyika Februari 25 na utajikita zaidi katika ardhi, uchumi na uhusiano wa kimataifa.
Mmoja wa wasimamizi wa mdahalo huo, Linus Kaikai alisema kuwa mdahalo utarushwa hewani na vituo vinane vya luninga na 34 vya redio za Kenya. Vyombo vya habari vya kimataifa kama vile CNN na Reuters vitapeperusha pia mjadala huo.
Kaikai, ambaye pia ni Mhariri Mkuu wa Utangazaji wa Kampuni ya Nation (NBD), alisema kuna watu maalumu wamechagulia kuingia kwenye mdahalo huo na watapewa nafasi ya kuwauliza maswali wagombea hao.
Watu hao wamechaguliwa kwa kuzingatia umri, jinsia, tabaka, mashirika, makanisa, wanasiasa, wawakilishi wa vikundi, na pia wasomi.
Uchaguzi wa Rais wa Kenya unasubiriwa kwa hamu na wafuatiliaji wa mambo ya siasa na mchuano mkali unatazamiwa kuwa kati ya Waziri Mkuu, Odinga na Naibu wake Kenyatta. Uchaguzi wa mwisho uliofanyika mwaka 2007 ulikumbwa na ghasia na mauaji ya kikabila.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs