HII NDIO KASHFA YA VYETI VYA ELIMU YA NAIBU WAZIRI WA ELIMU, MULUGO
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo
Philipo Augustine Mulugo ndiyo jina lake halisi ambalo
alilisomea mpaka alipohitimu darasa la saba kwa mara ya kwanza 1988,
lakini kutokana na kwamba hakufaulu kwenda sekondari alirudia darasa
hilo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa takriban miezi mitatu sasa
umebaini kuwa 1989, Mulugo alirudia darasa la saba katika Shule ya
Msingi Rukwa ya mkoani Mbeya akitumia jina la Hamimu Hassan.
Imebainika kuwa kabla ya kuhitimu darasa la saba kwa mara ya
pili, alibadili jina hilo (kutoka Hamimu Hassan) na kuwa Hamimu
Augustino ambalo aliendelea nalo wakati akisoma elimu ya sekondari
katika Shule ya Sekondari kutwa ya Mbeya (Mbeya Day) mwaka 1990.
Hata hivyo, Mulugo mwenyewe akizungumza na gazeti hili jijini
Dar es Salaam alipuuza tuhuma hizo kwa kusema kuwa ni njama za kisiasa
zinazofanywa na maadui zake. Mulugo anasema madai hayo yamekuwa
yakitolewa mara kwa mara na amekuwa akiyajibu kwa kuwaonyesha vyeti
vyake halali vya shule.
“Hayo madai ni ya muda mrefu, wewe sijui utakuwa mtu wa 20
kuuliza swali kama hilo. Mimi vyeti ninavyo na hata ukitaka ushahidi
nitakuonyesha,” alisema Waziri Mulugo na kuongeza:
“Haya mambo kabla hata sijachaguliwa kuwa Mbunge, tulivyokuwa
bado kwenye mchujo wa ndani, usiku wa manane watu walisambaza huu uvumi
na nilivyoenda kwenye kikao nikatoa vyeti vyangu, wakaviona.”
Waliomfundisha
Baadhi ya walimu waliomfundisha Mulugo, watu waliofanya kazi
naye pamoja na wakazi wa Kijiji cha Udinde alikozaliwa, maelezo yao
yanathibitisha mabadiliko ya majina ya Mulugo kwa nyakati tofauti pia
ngazi mbalimbali za kielimu.
Uchunguzi unabainisha kuwa baada ya kuhitimu kidato cha nne,
alifaulu kwenda Shule ya Sekondari ya Wavulana, Songea ambako alisoma
kati ya 1994 na 1996 akiendelea kutumia jina la Hamimu Mulugo.
Baada ya kuhitimu kidato cha sita, uchunguzi ulibaini kuwa
Mulugo alirejea Mbeya na 1998 alilazimika kubadili tena jina pale
alipotumia cheti cha mtu aitwaye Dickson Mulungu, kuombea kazi ya
kufundisha katika Shule ya Sekondari ya Southern Highlands.
Habari zinasema Mulugo alichukua hatua hiyo ili kumshawishi
mmiliki wa shule hiyo mfanyabiashara, Gulnoor Dossa (sasa ni marehemu),
kumpa nafasi ya kufundisha shuleni hapo.
“Mulugo alilazimika kutumia cheti cha rafiki yake aliyekuwa akiitwa
Dick Mulungu ambaye alipata daraja la pili katika Shule ya Sekondari ya
Songea Boys, hivyo ikawa rahisi kwake kupata kazi ya ualimu katika shule
hiyo,” alisema mmoja wa waliofanya kazi naye shuleni hapo (jina
tunalihifadhi kwa sasa).
Aliongeza kuwa Mulugo alianza kama mwalimu wa kawaida, lakini
baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa Shule (headmaster) wakati hakuwa hata na
cheti cha ualimu. Alichukua nafasi hiyo ya ukuu wa shule baada ya
aliyekuwapo kufariki dunia.
“Unajua wale wahindi (wamiliki) walikuwa ni wafanyabiashara kwa
hiyo hawakufuatilia kiwango cha elimu ndiyo maana walimpandisha tu
madaraja bila kujali kuwango cha elimu,” alisema rafiki yake huyo na
kuongeza:
“Nilimshauri aachane na cheo hicho kwani kama ungefanyika
ukaguzi wa Serikali na kumkuta bila vyeti vya ualimu angechukuliwa
hatua, hivyo alinisikiliza na akaachia nafasi hiyo na kujipa cheo cha
umeneja wa shule.”
Chanzo: mwananchi.co.tz
Chanzo: mwananchi.co.tz
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII