TUNDULISU AFUNGUKA KUHUSU SAKATA LA KUJIFUNGIA CHOONI
ZIPO taarifa
kwamba Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, wiki
iliyopita alijifungia chooni kukwepa waandishi wa habari waliotaka kauli
yake juu ya video hatari ambayo inadaiwa Mkurugenzi wa Ulinzi na
Usalama wa chama hicho, Wilfred Rwakatare, alirekodiwa akieleza njama za
uhalifu.
Tundu ambaye ni Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, amesema kuwa
maelezo yaliyotolewa kwamba alijificha chooni kwa muda wa saa mbili si
kweli, kwani hawezi kufanya hivyo.
“Jamani mimi na umri wangu huu nawezaje kuwakimbia waandishi wa habari? Siku zote mimi nafanya kazi na waandishi wa habari,” alisema Lissu na kuongeza:
“Ofisi yangu pale Ofisi Ndogo za Bunge, Dar es Salaam ina choo ndani, nikiwa ofisini kama mtu yupo nje wala hawezi kujua kama mimi nipo chooni. Nadhani hizo taarifa za kusema nilijifungia chooni ni za upotoshaji.
“Halafu haiwezekani mimi nikimbie suala la Rwakatare kwa sababu tayari nilishalitolea maelezo. Mpaka sasa, mimi kama mmoja wa mawakili wanaomtetea, nina maswali yangu kwa jeshi la polisi, kwani ile video haioneshi uhalifu wowote ambao umetendeka.
“Ni kweli niliweka miadi ya kuzungumza na waandishi lakini nilisahau. Nakumbuka jioni kabisa ya siku hiyo, nilipokea SMS ya mwandishi, akiniambia alikaa sana Ofisi Ndogo za Bunge, Dar es Salaam mpaka akachoka, kwa hiyo alishindwa kuniona.”
Wikiendi iliyopita, iliripotiwa na mitandao mbalimbali pamoja na gazeti moja la kila siku kwamba Lissu alijificha chooni kwa saa mbili kukwepa kuonana na waandishi wa habari, waliotaka ufafanuzi wake kuhusu kile kinachoendelea juu ya kesi inayomkabili Rwakatare ambaye ni Kiongozi Mstaafu wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII