HATIMAYE MBOWE AWASILISHA USHAHIDI POLISI KUHUSU MLIPUAJI WA BOMU ARUSHA....SOMA ZAIDI HAPA
HATIMAYE Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, jana amewasilisha kwa maandishi ushahidi wake makao makuu ya Jeshi la Polisi mjini Dar es Salaam. Maelezo ya Mbowe ambayo jana yaliwasilishwa, yamekuwa siri nzito, kwani yanatokana na msimamo wa CHADEMA kudai wana ushahidi na tukio la mauaji ya mlipuko wa bomu lililotokea Juni 15, mwaka huu mkoani Arusha.
Wakili wa Mbowe, Peter Kibatala alilithibitishia MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, kuwa aliwasilisha saa 5 asubuhi ambapo alipokelewa na Mkuu wa Idara ya Operesheni za Upelelezi Tanzania (CID), Kamishna Advocate Nyombi.
Baada ya kuwasilisha maelezo hayo, Wakili Kibatala alikataa katakata kuzungumzia kilichomo ndani ya maandishi hayo, kwa madai kuwa ni siri yao na polisi.
“Nathibitisha bila shaka, nimewasilisha majibu kwa niaba ya Mbowe leo (jana), makao makuu ya polisi kama tulivyokubaliana, lakini yaliyoandikwa humo ni siri…siwezi kuzijadili tusubiri kutoka kwao,” alisema Kibatala.
Hatua ya kuwasilisha majibu hayo kimaandishi, ilifikiwa Jumatano wiki hii katika mahojiano baina ya Polisi na Mbowe.
Siku hiyo, Mbowe aligoma kuwasilisha ushahidi wake polisi kama alivyotakiwa kwenye barua aliyoandikiwa na jeshi hilo Julai 17, mwaka huu, kwa kile alichosema hadi Rais Jakaya Kikwete atakapounda tume ya kijaji kuchunguza tukio hilo.
Katika barua hiyo, Mbowe alitakiwa kufika bila kukosa akiwa na ushahidi wa mauaji ya mlipuko wa bomu hilo.
Hata hivyo, Mbowe aliripoti kuitikia wito wa barua hiyo, lakini aliendelea kushikilia msimamo wake wa kutowasilisha ushahidi huo kwa polisi.
Jeshi la Polisi, limekuwa katika mvutano na Mbowe likimtaka kuwasilisha ushahidi kuhusu mlipuko wa bomu hilo, katika Uwanja wa Soweto wakati wa mkutano wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata nne na kuua watu wanne na kujeruhi wengine 70, katika uwanja huo ushahidi ambao alidai anao.
Endapo Mbowe atakutwa na hatia ya kutokuwa na ushahidi huo, atakumbwa na adhabu ya miaka mitatu jela au faini ya Sh 500,000.
Hii ni kwa mujibu wa Jeshi la Polisi katika barua yake kwa Mbowe, ikunukuu kifungu cha sheria ya kifungu cha 10(2) na (2A) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai nchini, sura ya 20, kama ilivyorekebishwa mwaka 2002.
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII