Mtihani Mwingine kwa LOWASA ndo Huu..

BongoNewz
WAKATI baadhi ya vigogo wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), kama Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrodi Mkono, wakitishia vikao vya juu vya chama hicho kwamba majina yao yasipopitishwa kutachimbika, Raia Mwema limeelezwa kuwa waliopita bila kupingwa katika kinyang’anyiro cha uongozi ndani ya chama hicho, hasa katika ujumbe wa Halmashauri Kuu, wanaweza kuchunguzwa.
Mbali na uwezekano wa kuwachunguza waliopita bila kupingwa, katika baadhi ya maeneo mchakato huo unaweza kurudiwa upya, na hasa pale itakapothibitika wamehusika kuminya demokrasia ndani ya chaguzi hizo za ndani ya chama.
Ni dhahiri sasa kuwa kati ya watakaoguswa endapo mchakato huo utachunguzwa na hata kurudiwa ni pamoja na Mke wa Mwenyekiti wa CCM na Rais Jakaya Kikwete, Salma, na mwanaye, Ridhiwani ambao wamepita bila kupingwa katika maeneo yao.

Taarifa, hata hivyo, zinasema hakuna malalamiko rasmi yaliyotolewa dhidi yao katika maeneo walikopita.
Raia Mwema limeambiwa kwamba hata kama kunaonekana ya kuwa kuna unafuu kidogo kwa Ridhiwani na mamaye, hali ni tofauti kwa wabunge kadhaa, baadhi wakiwa wamewahi kuwa katika Baraza la Mawaziri na wajumbe wa NEC inayomaliza muda wake.

Ridhiwani amekuwa akitajwa sana katika siasa za ndani ya CCM, na hasa ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ambako ni Mjumbe wa Baraza Kuu na Kamati ya Utekelezaji ya umoja huo aliojunga nao akiwa kijana wa sekondari.

Kwa upande wake, Salma alianza kuonekana katika harakati za siasa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2005.
Taarifa zinasema kinachowabana wabunge hao na viongozi wengine waliopita bila kupingwa ni kuhusishwa kwao na matumizi ya fedha, vitisho na mizengwe ya aina mbalimbali katika vikao vya uchaguzi kwenye maeneo walikogombea ili kuhakikisha wanapita bila kupingwa.

Taarifa zaidi kutoka wilayani Hanang, zinasema Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, amemuweka katika wakati mgumu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwezeshaji, Dk. Mary Nagu, wote wakiwania nafasi ya ujumbe wa NEC kupitia wilaya hiyo.
Taarifa zinasema awali Dk. Nagu alikuwa hakupendekezwa na Kamati ya Siasa ya Wilaya kwa sababu ya kuwa tayari ana nyadhifa nyingi kwa kuwa yeye ni mbunge na waziri.

Uamuzi huo kwa mujibu wa taarifa hizo, ulifikiwa kwa wajumbe kupiga kura matokeo yakawa ni kura saba zilizokubali aaachwe hbuku tano zikimuunga mkono.
Taarifa zinasema zaidi kwamba baada ya hapo muhtasari uliandaliwa na Katibu wa Wilaya kuelekeza kwamba Dk.Nagu aachwe, lakini katika mazingira tatanishi muhtasari huo unadaiwa kuchakuliwa na hatimaye jina la Dk. likarejeshwa huku hatua hiyo ikiacha sintofahamu kubwa miongoni mwa wafuasi wa CCM wilayani Hanang.

Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa msimamo wa kurejea mchakato wa upitishaji majina katika vikao vya ngazi ya wilaya na mikoa kwa wadhifa wa NEC unaungwa mkono na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maadili ya CCM ambayo inaundwa na watu wazito kwenye chama hicho kikongwe nchini.
Wajumbe wa kamati hiyo ya maadili ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Tanzania Bara, Pius Msekwa, Makamu Mwenyekiti Zanzibar-Aman Abeid Karume, Katibu Mkuu, Wilson Mukama, Abdulrahaman Kinana, Samia Suluhu Hassan, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara- John Chiligati na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar- Vuai Ali Vuai.

Katika mazingira hayo, Katibu wa Halmashauri Kuu -Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ameliambia Raia Mwema ya kuwa ni utaratibu wa kawaida wa vikao vya chama hicho kuamua tofauti na inavyotarajiwa, hasa pale ambapo demokrasia inaonekana kuchezewa ndani ya chama chake.
Kwa mujibu wa Nape, uchaguzi unaweza kurudiwa endapo vikao vitaridhika kuna juhudi za kukandamiza demokrasia zilifanyika ili watu fulani wapite bila kupingwa.

“Vikao vitaamua hasa pale vitakapojiridhisha kwamba kuna baadhi ya maeneo demokrasia haikupewa nafasi. Ni mambo ambayo yamewahi kuamuliwa huko nyuma katika chaguzi zilizowahi kufanyika ndani ya chama. Kuna maeneo mchakato ulirudiwa baada ya kuona demokrasia ndani ya chama imefinywa,” anasema Nape Nnauye alipoulizwa kwa njia ya simu na mwandishi wetu kuthibitisha taarifa zilizotufikia kwamba kuna baadhi ya maeneo uchaguzi utarejewa ndani ya chama hicho.

Tayari Sekretariati ya CCM chini ya uongozi wa Katibu Mkuu Mukama imefanya kikao chake mjini Dodoma ambacho kinafuatiwa na kikao cha Kamati ya Maadili na baadaye kikao cha Kamati Kuu na kukamilisha kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho.

Endapo uamuzi wa kurudia uchaguzi hasa wa nafasi ya NEC ngazi ya wilaya utafanywa na vikao vya chama hicho, miongoni mwa viongozi wanaoweza kuathiriwa ukiondoa wale ambao ni kutoka katika familia ya Kikwete (Salma na mwanawe Ridhiwani) ni pamoja na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge.
Kwa upande wa Lowassa, mizengwe inadaiwa kufanyika japo haikufanikiwa huku malengo ya mizengwe hiyo yakitajwa kuwa ni kuhakikisha Lowassa anapita bila kupingwa.

Mizengwe hiyo wilayani Monduli hata hivyo inadaiwa kufanywa na watu ambao wanadhaniwa kuwa watiifu kwa Lowassa na kusababisha mshindani wake mkuu, Dk. Salesh Toure, ambaye amewahi kuwa Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha kuchukua fomu ya kuwania kutoka wilaya nyingine.
Inadaiwa kuwa licha ya kuchukua fomu kutoka wilaya nyingine na kuijaza na kisha kuwahi ndani ya muda kuirejesha fomu hiyo ofisi ya CCM wilayani Monduli, mizengwe ilizidi kufanywa dhidi yake hadi malalamiko kutoka kwa mgombea huyo yalipofikishwa makao makuu ya CCM ofisi ndogo Lumumba na viongozi wa Monduli kuamriwa wapokee fomu hiyo.

Kutoka Bariadi, Andrew Chenge naye anahusishwa kwa mbinu zilizo nje ya mfumo wa uchaguzi wa chama hicho akidaiwa kutia mizengwe dhidi ya baadhi ya washindani wake ambao inadaiwa walikuwa 11 na wote walijitoa kwa nyakati tofauti.

Mbali na viongozi hao, hali ya vitisho na mizengwe kuhakikisha majina ya wagombea fulani yanapitishwa na vikao vya uamuzi imejitokeza katika uchaguzi wa kupitisha majina ya wagombea katika jumuiya za CCM.
Jumuiya ya Wazazi, ambamo mgombea Nimrodi Mkono amekwishatoa vitisho kwamba jina lake likikatwa na vikao vya juu vya CCM basi patachimbika, huko nako hali si shwari.

Taarifa zinazotarajiwa kujadiliwa katika kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM zinatajwa kugusa hali ya mizengwe, rushwa na mbinu nyingine chafu zilizojitokeza si tu katika Jumuiya hiyo ya Wazazi bali pia katika Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT) ambako mchuano mkali ni kati ya anayetetea kiti hicho, Sofia Simba na Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango Malecela.

Mbali na Kilango na Simba, wagombea wengine UWT ni pamoja na Waziri wa Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk. Terezya Huvisa.
Akizungumia michakato hiyo, mtaalamu wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana anasema: “Kinachopaswa kufanywa na CCM katika vikao vyake ni kufanya uamuzi utakaokubaliana na saikolojia ya wapiga kura, ambao wengi ni vijana.”

Dk. Bana anaongeza: “Uongozi wa CCM bado haujafanikiwa kutawanya makundi hasa yanayolenga urais 2015. Kwa bahati mbaya makundi haya yanaangalia namna ya kupata uongozi badala ya masuala ya kisera na itikadi.
“Sasa vyama vingi tawala Afrika vimeng’olewa madarakani na saikolojia ya wapiga kura imebadilika, kuna wapiga kura ambao wao wanatamani tu mabadiliko ya chama madarakani bila kujali kitakacholetwa na mabadiliko hayo. Sitashangaa kuona 2015 chama kingine kinaingia madarakani kama CCM wakishindwa kutumia mtihani huu wa uchaguzi wa ndani kukipanga chama chao.

“Tumeanza kuona political work (kazi ya kisiasa) katika CCM inafanywa na mtu mmoja, Nape Nnauye, hii ni hatari kwa chama kikubwa, kazi ya siasa ni lazima ifanywe na mtandao wote wa chama,” alisema Dk. Bana.

Hotuba ya Kikwete Mwanza
Katika hotuba yake wakati wa maadhimisho ya miaka 35 ya CCM yaliyofanyika jijini Mwanza Februari, mwaka huu, Rais Kikwete aliwaambia wanaCCM wenzake; “ ...hatuna budi kutambua kuwa ili chama chetu kiendelee kupata ushindi na kuongoza taifa letu kwa miaka mingi zaidi, hatuna budi kwenda na wakati.

“Ni ukweli ulio wazi kuwa uhai na uhalali wa chama chetu kushika hatamu za dola unategemea ridhaa ya wananchi. Hisia zao na mtazamo wao juu ya chama chetu ndizo zinazowafanya waamue kutupatia au kutunyima ridhaa hiyo.

“Kamwe tusikubali sisi viongozi kuwa chanzo cha kuipoteza tunu hii ya Watanzania kwa kushindwa kuchukua hatua sahihi. Tukichelea kufanya hivyo, tutachekwa na kulaumiwa sana na kamwe historia haitotusamehe.”

Kikwete na watuhumiwa wa ufisadi
Aliendelea kusema; “Halmashauri Kuu ya Taifa ilikubaliana kwamba sifa na sura ya chama katika macho ya jamii imeathiriwa sana na kuwa na viongozi wanaonyooshewa vidole na kutuhumiwa kwa mwenendo mbaya hasa vitendo vya rushwa, wizi, utovu wa nidhamu na ubadhirifu.

“NEC iliamua kuwa viongozi wa namna hiyo hawafai kuwamo katika safu za uongozi wa chama chetu.
Ikaamuliwa wapime, watafakari na kuamua kujiondoa katika uongozi na wasipofanya hivyo waondolewe.”

Kauli hiyo ya Kikwete bado inaelekea kuwa mzaha wa kisiasa hasa baada ya kuonekana baadhi ya watu waliotajwa tajwa katika tuhuma mbalimbali za ufisadi kuendelea kushika nyadhifa mpya za kisiasa na katika jamii, huku wakiendelea kugoma kuachia nafasi walizokuwa nazo kabla ya kutakiwa kujiondoa.

Mwanasiasa pekee aliyeachia nafasi zake zote ni aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, ambaye pamoja na kuachia nyadhifa zake ndani ya chama, alijiuzulu hata ubunge, huku watuhumiwa waliotajwa pamoja naye, wakionekana kutoa hadi vitisho kwa uongozi wa juu wa CCM na kuendeleza mikakati michafu dhidi yao.

Hali hiyo, imezidisha ufa mkubwa ndani ya CCM na kuathiri hata utendaji kazi wa serikali na kuvipa nguvu vyama vya upinzani, hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho, taarifa zisizo rasmi zinaeleza kuwa baadhi ya wana CCM wamekuwa wakikisaidia kwa ‘hali na mali’ wakiwekeza kujihami na upepo wa mabadiliko usije kuwaathiri.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs