Mchungaji Msigwa kuongoza maandamano kumng'oa Kamanda Kamuhanda

BongoNewz
Tukio la kuuawa kwa mwandishi huyo bado limevuta hisia za wananchi wengi ambapo shinikizo linaelekezwa kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, likimtaka ajiuzulu kama sehemu ya uwajibikaji.

Akihutubia wananchi hao, Mchungaji Msigwa, alilaani kitendo cha kuuawa kwa Mwangosi na kusema kuwa hatatoa kauli yoyote isipokuwa atafanya kazi kwa vitendo na kuhakikisha Kamanda Kamuhanda anaondoka. “Hatuwezi kulinda ujinga huu uendelee, mimi sitatoa tamko ila nitaanza kwa vitendo. Hatuwezi kuuacha uozo huu. Kamuhanda lazima aondoke,” alisema.
Alilitaka jeshi la polisi kumuogopa Mungu na kutenda haki badala ya kutii amri zinazohatarisha usalama wa raia na kuwakatisha uhai. “Nalaani vitendo vyote vya jeshi la polisi vinavyohatarisha usalama wa raia. Na wale wote wanaotoa amri kwa askari kwa ajili ya kuwapiga na kuwaua wananchi washindwe na walegee kwa jina la aliyehai Yesu Kristo, Iringa hatukuzoea matukio haya, sasa basi Kamuhanda lazima aondoke,” alisema Msigwa.

Aliwataka wananchi wa Iringa kushiriki katika maandamano ya amani yatakayofanyika leo kuanzia ofisi yake kuelekea katika ofisi ya Kamanda Kamuhanda kushinikiza aondoke Iringa.
“Nyumbani kwetu kuna nyoka, huyu nyoka lazima aondoke. Kila Ijumaa tutakuwa na maandamano ya amani kumng’oa huyu nyoka na lazima polisi walinde maandamano hayo. Kamuhanda ni nyoka lazima aondoke,” aliongeza.

Polisi chupuchupu kupigwa na wananchi mkutanoni Iringa Mjini
MAUAJI ya mwandishi wa kituo cha runinga cha Channel Ten, marehemu Daud Mwangosi, aliyeuawa kwa kufyatuliwa bomu na polisi kijijini Nyololo mkoani Iringa, yameendelea kuliandama jeshi hilo, ambapo wananchi mjini hapa nusura wampige askari aliyevamia mkutano wa mbunge juzi.

Katika mkutano huo wa mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA), uliofanyika katika eneo la Soko Kuu mkabala na kituo cha polisi, askari mmoja alijitokeza na kutaka kuwapiga wananchi kwa virungu bila sababu. Wakati Mchungaji Msigwa akiendelea kuhutubia, askari huyo alitokea kituoni hapo na kwenda kutembeza virungu kwa watu, lakini kabla ya kuanza kazi yake, sauti za wananchi zilipazwa zikisema, “Muacheni huyo ndiye atakayetuonyesha Mwangosi leo hii.”

Wakati zogo hilo likiendelea, kundi la vijana lilianza kumsogelea huku likisema: “Hatuogopi mabomu wala bunduki za polisi.” Purukushani hizo, ziliwafanya askari wenzake kufika na kumvuta huku wakimkimbizia kituoni kumnusuru na uamuzi waliotaka kuuchukua wananchi dhidi yake.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs