CUF yawanasa live CCM wakinunua vipande vya kupigia kura BUBUBU

Jana tarehe 14/9/2012 ikiwa zimebaki siku mbili kabla ya siku ya upigaji kura kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu, CCM wanaonekana kutegemea rafu na michezo michafu kama mtaji wa kutafutia ushindi.

Kikosi Maalum cha Operation na mipango ya Uchaguzi wa Bububu cha CUF kilipokea taarifa jana kiasi cha saa 2 usiku kutoka kwa mmoja ya wanafamilia ambae baba yake mzazi alikataa katakata kumuuzia Mgombea wa CCM (Bhaa) kipande chake cha kupigia kura kwa thamani ya shilingi laki moja.

Baada ya kupokea taarifa hizo, kikosi hicho Maalum kilianza operation yake ya kumsaka kila kipembe mgombea wa CCM na wenzake ambao kwa usiri na ustadi mkubwa walikuwa kazini kununua vipande vya kupigia kura. Mara taarifa kuhusu sehemu ambayo zoezi la kununua vipande vya kupigia kura linaendelea ilipatikana.

Gari la CUF lenye kikosi hicho Maalum lilivamia kwa ghafla eneo la tukio kiasi cha saa 5 na dakika kadhaa usiku na kumfuma mgombea wa CCM, mlinzi wake na dereva wakiwa wote wamesimama pembeni ya gari lao wakiendelea kupatana mpiga kura kura (jina linahifadhiwa) ili kununua kipande chake.

“Vamia, kamata wote, haraka haraka, piga picha piga picha, watie katika gari!!” Kauli ya kamanda wa kikosi hicho maalum ilisikika. Kishindo hicho cha ghafla kiliwashtua wote waliokuwa wakiuziana vipande vya kupigia kura na kupatwa na mfadhaiko mkubwa wakiwa hawaamini kinachotokea.

Mgombea wa CCM, mlinzi wake na dereva kwa haraka mno walijilenga katika gari , wakawasha na kukimbia huku wakimuacha mteja wao peke yake akifadhaika na kujikuta mikononi mwa wana operation wa CUF. Haya yakitendeka mpiga picha maalum wa operation hii akiendelea na kazi yake. Kijana huyo aliingizwa katika gari la CUF na kuelekea kituo cha Polisi. Hata hivyo baada ya kusikiliza maelezo ya mpiga kura huyo, wana operation wa CUF walimsamehe na kumpa onyo kali.

CCM wamefadhaika na hawana imani wala matumaini ya kuweza kuutumia mchezo wao wa wizi wa kupigisha kura kumi kumi na kuleta watu kutoka maeneo mengine kuja kupiga kura. CUF wameapa kumkata kichwa mtu yeyote atakaethubutu kusogea kituoni kwa ajili ya kupiga kura na ilhali si mpiga kura wa jimbo hilo.

Jambo hili limewatia hofu wapiga kura hewa waliopangwa kwa kazi hii wakiwemo wale waliotumika kusaidia kuiba jimbo hilo katika uchaguzi wa 2010. Vijana hao kutoka nje ya Bububu wanaohofia kupoteza maisha yao wamekataa kata kata kusogea kituoni kwa ajili ya kusaidia wizi wa jimbo hilo.

Baada ya kufeli kwa mikakati iliyozoeleka CCM sasa wameamua kuupa nguvu kubwa mpango wa kununua vipande vya kupigia kura. Kiasi kikubwa cha fedha kimetengwa kwa ajili kufanikisha ununuzi wa vipande vya kupigia kura kwa bei ya shilingi laki moja kwa kipande kimoja. Uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu unatarajiwa kufanyika kesho Jumapili tarehe 16/09/2012, huku kampeni za CUF zikifungwa rasmi leo na Mwenyekiti wa CUF Taifa Mhe Profesa Ibrahim Haruna Lipumba.

SOURCE: JF
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs