KIGWANGALA: NITAJIUZULU UBUNGE ENDAPO CCM TAIFA ITAKAA KIMYA


SAKATA la makada wa CCM, Hussein Bashe na Dk Hamis Kigwangala kutoleana bastola, limechukua sura mpya baada ya Jeshi la Polisi kuingilia kati na kumnyang’anya bastola Kigwangala huku likianza kuwahoji wapambe wa mahasimu hao.

Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, (RPC) Antony Lutta zilieleza kuwa jeshi hilo linaishikilia silaha ya Dk Kigwangala hadi hapo uchunguzi utakapokamilika.

Kauli hiyo ya polisi imekuja siku moja baada ya uongozi wa chama hicho Wilaya ya Nzega, kutaka suala hilo liondolewe polisi ili walishughulikie kimyakimya ndani ya chama.



Akizungumza na gazeti la Mwananchi Jumapili, Dk Kigwangala ambaye pia ni Mbunge wa Nzega na kumuuliza kuhusu suala hilo alisema: “Bastola yangu mbona ninayo, hilo halina ukweli, bastola ninayo hapa.” Wakati hayo yakiendelea, uongozi wa CCM wilayani humo umempa onyo kali Dk Kigwangala ukieleza kwamba endapo ataendeleza msimamo wake wa kukataa kuhojiwa na chama, atachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa kadi ya uanachama.

ASEMA ATAJIUZURU UBUNGE
Hata hivyo, mbunge huyo alisema kuwa hana imani na uongozi wa CCM wilayani Nzega na kwamba iwapo CCM mkoa na taifa hautaingilia kati mgogoro huo, yuko tayari kujiuzulu ubunge.

Bashe na Dk Kigwangala ambao ni mahasimu wa siku nyingi katika medani za siasa wilayani Nzega walidaiwa kutoleana bastola Alhamisi iliyopita walipogongana katika ofisi za CCM wilayani humo, wakati wakirejesha fomu za kuwania Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia wilaya hiyo. Hata hivyo, pamoja na taarifa hizo kuthibitishwa na viongozi wa CCM wilayani humo na RPC Lutta, kila mmoja alikanusha madai hayo akimtuhumu mwingine kuwa ndiyo chanzo cha ugomvi huo.

Wakati Bashe alisema Dk Kigwangala ndiye aliyetoa bastola kumtishia wakiwa ndani ya Ofisi ya CCM Wilaya, Dk Kigwangala alieleza kuwa walinzi wa Bashe ndio waliomtishia yeye bastola na kwamba tayari amelifikisha suala hilo polisi na wanalifanyia kazi.

SOURCE: MCL
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII

Copyright © 2013. ArtAfropixels Media.com - All Rights Reserved
Customized by: IT XPERTTZ ONE | Powered by: BS
Designed by: Tilabs