Mbio za Uchaguzi ndani ya CCM ni MOTO, Sumaye amkaba Koo Nagu
MBIO za uchaguzi ndani ya CCM zimefikia patamu, baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk Mary Nagu kuenguliwa kugombea nafasi ya Ujumbe wa Nec kupitia Wilaya ya Hanang', huku Mke wa Rais, Salma Kikwete akiwa mgombea pekee wa nafasi hiyo Lindi Mjini.
Mkoani Dar es Salaam, mbio hizo zimeonekana kuwaweka pabaya Mwenyekiti wa UWT wa mkoa huo Zarina Madabida na Katibu wake, Tatu Maliaga baada ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa, John Guninita kueleza kuwa viongozi hao watafikishwa kwenye kamati ya maadili kueleza kwa nini wamesitisha uchaguzi wilayani Kinondoni.
Habari kutoka Hanang' zimeeleza kuwa Kamati ya Siasa ya CCM ya Wilaya hiyo imemwengua Dk Nagu na kuwabakiza wagombe wawili, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Leonsi Marmo. Taarifa kutoka kwenye kikao hicho kilichofanyika juzi katika Ofisi ya CCM ya wilaya hiyo na kuhudhuriwa na wajumbe 12 zimeeleza kuwa Dk Nagu ameenguliwa kutokana na maelezo kuwa kanuni hazimruhusu kugombea.
Chanzo cha habari kimeeleza kuwa kanuni iliyomwondoa Dk Nagu kwenye kinyang’anyiro hicho ni ile inayowataka viongozi wenye kazi za kila siku; ubunge na uwaziri kutogombea.
Imeelezwa kuwa jitihada za wajumbe watano waliojipambanua katika kikao hicho kumtetea Dk Nagu ziligonga mwamba, baada ya wenzao saba kuunga mkono uamuzi huo.
Kuenguliwa kwa Dk Nagu kunatokana na sababu za kuwa na kazi za muda wote kumeibua hofu kuhusu hatima ya viongozi wengine waliochukua fomu ambao kwa mujibu wa kanuni iliyomwondoa Dk Nagu nao hawakupaswa kugombea.
Hao ni pamoja na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk Abdallah Kigoda, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk Emmanuel Nchimbi.
Wengine ni Wabunge Deo Filikunjombe (Ludewa), Mussa Azzan Zungu (Ilala), Dk Hamis Kigwangalla (Nzega) na Andrew Chenge (Bariadi Magharibi).
Salma akosa mpinzani Lindi
Katika hatua nyingine Mke wa Rais, Salma Kikwete amerudisha fomu ya kuwania ujumbe wa Nec Taifa kupitia Wilaya ya Lindi Mjini. Katibu wa CCM Wilaya ya Lindi Mjini Mohamed Kateva, alisema jana kwamba Salma ni mgombea pekee aliyejitokeza kuwania nafasi hiyo katika wilaya yake. Kateva alisema mwisho wa kurudisha fomu ilikuwa Agosti 28, mwaka huu na mpaka tarehe hiyo hakukuwa na mtu mwingine aliyekuwa amejitokeza kuwania nafasi hiyo.
Madabida kiti moto
Katika Mkoa wa Dar es Salaam, Madabiba na Maliaga watahojiwa kwa kukiuka uamuzi ya Halmashauri Kuu ya Mkoa.
Viongozi hao wanadaiwa kusimamisha uchaguzi wa UWT Wilaya ya Kinondoni ambao ulipangwa kufanyika Agosti 31, mwaka huu.
Guninita alisema jana kuwa kikao hicho cha Nec mkoa kiliagiza uchaguzi wa jumuiya zote ufanyike kuanzia Agosti 31 hadi Septemba 2, mwaka huu lakini UWT Wilaya ya Kinondoni haikufanya uchaguzi huo.
Alisema katika kikao chake cha Agosti 29, mwaka huu Nec Mkoa kilipitisha wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika wilaya zote tatu na kuagiza uchaguzi ufanyike.
“Mwenyekiti wa UWT na katibu wake kwa sababu zao binafsi walisimamisha uchaguzi na kwa mujibu wa katiba yetu hili ni kosa,” alisema Guninita.
Alipotakiwa kuzungumzia madai hayo Madabida alisema: “Nipo kikaoni. Lakini ndani ya chama chetu cha CCM hakuna mtu anayeweza kuusimamisha uchaguzi peke yake.”
0 comments:
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII